http://www.swahilihub.com/image/view/-/1637070/medRes/410202/-/vov216/-/sheriaa.jpg

 

USINGIZI WA KUTOSHA, UTULIVU NI HAZINA MUHIMU KABLA YA, WAKATI WA NA BAADA YA MTIHANI

Mtihani

Wanafunzi wa shule ya msingi ya Royal International Academy Githurai wasomea mtihani wa KCPE. Picha/ANTHONY OMUYA  

Na HENRY MOKUA

Imepakiwa - Tuesday, October 31  2017 at  13:48

Kwa Muhtasari

Mahangaiko ni sehemu ya maisha ya binadamu ambayo ina mfanyiko wake katika maumbile. Binadamu hahitaji kufanya mazoezi ili kujua kuhangaika bali hulazimika kuhangaika pindi hitaji fulani linapomsukuma.

 

Uhitaji ni mojawapo ya vichocheo vikuu vya mahangaiko. Unapohitaji kitu fulani ambacho unajua kitakufaa, sharti ukihangaikie. Haya ndiyo maumbile.

Tunapokuwa na zoezi, tumejizoeza kungoja hadi siku chache kabla ya makataa ndipo tukalianza au kuzidisha juhudi zetu kwalo. Wakati mwingine tunakesha kwa siku kadhaa ili kufikia lengo mahsusi.

Aghalabu tunafanikiwa licha ya kufanya zoezi la mwezi nzima kwa siku chache, ila ufanisi wetu ni wa wastani tu. Tumewarithisha watoto wetu mazoea haya nao wakijua ndiyo msingi wa kuwakidhia mahitaji, wameyashikilia kwa dhati.

Licha ya kwamba mazoea haya yametukolea, imethibitika kwamba utulivu ni wa umuhimu mkubwa kila unapotaka matokeo bora hasa katika maswala ya kiakademia.

Inakupasa ewe mtahiniwa ujiaminishe kwamba umeyafanya yote yaliyokujuzu na sasa upo tayari kuukabili mtihani. Hata ambapo unajua vipo vipengele fulani ambavyo hukuvishughulikia kikamilifu, tulia.

Kukazana kusoma faslu zote katika siku chache zilizosalia kutakutia tu kiwewe na kuyadidimiza matokeo yako zaidi. Kadiria muda uliosalia na kuupangia kihalisia pasipo kujibana kupindukia.

Jihakikishie kwamba ijapo hujazipitia sehemu fulani yalivyokuwa matarajio yako, zipo ulizojiandaa kwazo vilivyo. Hatua hii itakuwezesha kuyatoa majibu faafu katika faslu ulizozielewa fika. Wahka na woga vitashirikiana tu kukupokonya ufanisi wako – katu usiviruhusu.

Umekuwa ukilala kwa saa tisa au kumi – katika hali halisi, ingawa ulitarajiwa kulala kwa saa saba hadi nane. Kugundua muda uliosalia ni mchache, umeamua kufidia muda ulioupoteza – sivyo ifanyavyo kazi akili ya binadamu.

Katika makala mojawapo ya awali nilieleza umuhimu wa usingizi wa kutosha na haja ya kudumisha saa ya kulala na kuamka. Ningependa kukukumbusha na kusisitiza katika makala haya kwamba kumbukumbu huimarishwa mno tunapokuwa usingizini.

Kuyaweka uliyoyasoma katika kumbukumbu ya kudumu hufanyika unapokuwa usingizini, kuyakumbuka yaliyowekwa katika kumbukumbu hiyo huhitaji utulivu.

Kwa jinsi hii, jiruhusu kulala kwa muda unaofaa; saa saba kwa wastani ili kumbukumbu yako ifanye kazi barabara. Aidha, jizoeze kadri iwezekanavyo kulala saa ile ile kila siku na kuamka saa mahsusi; mathalan, ukalala saa nne usiku na kuamka saa kumi na moja asubuhi.

Unapotoka darasani, maktabani au mahali pako pa kusomea, jiepushe na kelele. Kupiga kelele baada tu ya kusoma huyasababisha kutoweka uliyoyasoma.

Ili kujitenga na hali hii, tumia muda mchache baada ya kusoma kuyatafakari uliyoyasoma na kuyafumbata vilivyo. Sikusudii kwamba usicheze wala kushiriki mizaha na wenzio, waweza kufanya hivyo muradi umeyapanga akilini mwako uliyoyasoma.

Unaweza kutatizika mwanzoni; si wajua mazoea ni taabu, ila usiwe mwepesi wa kusalimu amri. Lazima ujitahidi, ujihini starehe ikibidi ili kuyapata matokeo yatakayokufaa.

Kinyongo na mizozo ni mambo yanayokubidi uyakome. Ikiwa yamekukolea kiasi kwamba ni namna mojawapo ya kukutambua, au watambuliwa kwayo, jitenge nayo katika kipindi hiki cha mtihani tu.

Ama kwa kweli, sidhani yatakufaa hata baada ya mtihani unaoendelea kuufanya au kutazamia kuufanya. Taaluma yoyote iwayo itahitaji utulivu, uzingativu, makini. Kujifunza mambo haya mapema ni kujiwekea hazina itakayokufaa sasa na kuendelea.