http://www.swahilihub.com/image/view/-/4609586/medRes/2006823/-/14xmn5hz/-/oshaso.jpg

 

Utaratibu wa kusafisha uso

Mwanamke wa Kiafrika aosha uso wake

Mwanamke wa Kiafrika aosha uso wake. Picha/MAKTABA 

Na MARGARET MAINA

Imepakiwa - Wednesday, June 13  2018 at  09:45

Kwa Muhtasari

Kuna njia nyingi za kuufanya uso wako uvutie na kupendeza.

 

USAFI wa uso ni mojawapo ya mambo muhimu sana kwa mwanamke au mwanamume yeyote yule ambaye anapenda kuwa nadhifu na mwenye mvuto.

Unapokutana na mtu sura yako na mwonekano wa sura yako ndio kitu cha kwanza kinachokutambulisha kwamba wewe ni nani na upo kwenye hali gani.

Kuna njia nyingi za kuufanya uso wako uvutie na kupendeza.

Leo tunajadili zaidi jinsi ya kusafisha uso kwa njia ya asili. Mimi hupenda kutumia njia ya asili sababu ni kando na kwamba ni rahisi, mtu anaweza kuitumia kwa mazingira yoyote yale. Na matumizi ya vitu vya asili kwenye mwili husaidia kupunguza sumu mwilini kwani kitumia vipodozi vyenye kemikali husababisha miili yetu kujaa sumu.

Njia ya asili ya kusafisha na kupendezesha mwili inahitaji vitu vinnne vikuu: asali, sukari, maziwa, na limau.

Haijalishi ni aina gani ya ngozi unayo; njia hii ya asili inaweza kutumika kwa aina yoyote ile ya ngozi ama iwe ngozi yenye mafuta au ngozi kavu.

 

Vinavyohitajika:

  • Kijiko kimoja cha asali

  • Kijiko kimoja cha sukari

  • Kijiko kimoja cha maziwa

  • Kijiko kimoja cha limau

 

Utaratibu wa kusafisha uso

Mimina asali, sukari, maziwa na limau kwenye chombo kilicho safi; vichanganye mpaka vilainike.

Viache kwa muda wa dakika 10 ili viweze kuchanganyikana vizuri na sukari iyeyuke.

Baada ya mchanganyiko wako kuwa tayari, chukua kipande cha pamba kilicho safi na utumia kupakia mchanganyiko wako usoni.

Kumbuka kwamba ni vizuri kufanya hivyo wakati uso ungali mchafu na hupaswi kuosha uso kwanza kabla ya shughuli hii.

Baada ya kupaka mchanganyiko wako usoni, kaa kwa dakika 15.

Baada ya hapo chukua maji ya fufutende, kitaulo kisafi na sabuni ya kipande. Ni vizuri kutumia sabuni ya kipande maana haina kemikali nyingi.

Tumia kitambaa kuoshea uso wako pamoja na sabuni.

Pangusa uso wako na upake mafuta.

Kumbuka njia hii haina madhara yoyote na haibadilishi rangi au muonekano wa ngozi yako na unashauriwa kuitumia mara kwa mara ili uwe na mvuto zaidi.