http://www.swahilihub.com/image/view/-/1710778/medRes/471649/-/qmm93k/-/KuraNakuru.jpg

 

Utekelezaji wa kura, ugatuzi ulainishwe

Nakuru

Wakazi wa Nakuru wakiwa kwenye foleni shule ya msingi ya Koinange, Machi 4, 2013 tayari kupiga kura. Picha/SULEIMAN MBATIAH 

Na TAHARIRI YA TAIFA LEO

Imepakiwa - Thursday, December 28  2017 at  06:28

Kwa Muhtasari

Viongozi wa kidini nchini walitumia sherehe za Krismasi kuwahimiza viongozi wa mirengo yote ya kisiasa kutuliza joto la kisiasa kwa kuongea pamoja ili kuleta taifa pamoja.

 

VIONGOZI wa kidini nchini walitumia sherehe za Krismasi kuwahimiza viongozi wa mirengo yote ya kisiasa kutuliza joto la kisiasa kwa kuongea pamoja ili kuleta taifa pamoja.

Taifa hili limechukua muda mrefu kurejelea hali yake ya kawaida baada ya kugawanyika katika misingi ya kikabila kutokana na kipindi kirefu cha kampeni kilichotangulia uchaguzi wa Agosti na Oktoba 2017.

Tofauti za kisiasa zilizozuka miongoni mwa Wakenya zimesababisha chuki ambayo ilifikia viwango hatari.

Ijapokuwa uchaguzi umekamilika lakini bado hisia miongoni mwa wananchi zingali na chachu kote nchini.

Maswali mengi na magumu bado hayajapata jawabu. Kutoaminiana na kutovumuliana kumepenya mno.

Mnamo Jumanne, kwa mfano, Waziri wa Maji Eugene Wamalwa alitimuliwa wakati wa sherehe ya kijamii katika eneo la Mbale Kaunti ya Vihiga kisa na maana anahusishwa na mrengo fulani wa kisiasa.

Ijapokuwa ni kiongozi wa kitaifa na mwenye tajriba katika jamii, bado hakupokewa kwa vile yuko kwa Serikali na jamii iliyomtimua iko katika mrengo wa upinzani.

Viongozi wa dini wamekuwa katika msitari wa mbele wakisukuma mashauriano ya pamoja miongoni mwa viongozi wa mirengo yote ya kisiasa na washika dau kwa lengo la kurejesha uuwiano.

Ni wazi kuna masuala nyeti yanayochangia misimamo hii mikali ya kisiasa ambayo yanatakiwa kusuluhishwa ndipo matunda ya majadiliano yapatikane kisha amani na umoja zipatikane ndipo udhabiti wa nchi nao upatikane.

Maswala yanayopaswa kupewa kipaumbele kwa sasa ni ugavi sawa wa rasilmali za kitaifa, matumizi mema ya pesa za umma na uwajibikaji wa viongozi.

Kuna hisia kwamba kuna kutengwa kwa baadhi ya jamii, suala ambalo halipaswi kupuuza na walio mamlakani.

Ni matumaini yetu kuwa pande zote za kisiasa zitashiriki mdahalo wa kitaifa ili kujadili masuala nyeti yanayokera na kusumbua Wakenya.

Ni muhimu maswala ya uchaguzi na ugatuzi yazingatiwe ili kuhakikisha sauti za Wakenya wote zinasikika na mchango wao kutambuliwa katika viwango vyote vya uongozi wa nchi.

Haifai taifa hili kuingia katika kipindi kingine cha uchaguzi kukiwa na hiyo hali ya kutoaminiana.