Uteuzi viongozi wa Haki za Binadamu muhimu

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Friday, November 30  2018 at  08:08

Kwa Muhtasari

Ni lini Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) nchini Tanzania itapata viongozi wapya?

 

TAKRIBAN mwaka sasa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) haina viongozi tangu alipostaafu aliyekuwa mwenyekiti wake, Bahame Nyanduga Desemba 2017.

Tangu kustaafu kwa viongozi wake, kimya kimekuwa kikubwa kiasi cha kuwaibua baadhi ya wadau ukiwamo Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), ambao hivi karibuni umemuandikia barua Rais John Magufuli kufanya uteuzi wa viongozi wa tume hiyo.

Umuhimu wa chombo hiki kilichoanzishwa kikatiba, ndio unaotusukuma nasi kuisihi mamlaka husika kuufanyia kazi ushauri huu wa wadau. Tusifike hatua wakajitokeza watu na kudai kuwa kwa hali ilivyo mamlaka zetu hazitaki kuheshimu matakwa ya kikatiba kwa kuchelewesha uteuzi wa tume hiyo.

Katika mazingira yaliyopo sasa ya baadhi ya watu wakiwamo watumishi wa umma na watendaji wa Serikali kukiuka haki za binadamu na misingi ya utawala bora, tunadhani ni wakati mwafaka kwa mamlaka ya uteuzi kufanya kazi ya kuteua watendaji wa tume.

Ni dhahiri kuwa kuwapo kwa tume kunaweza kusaidia kupunguza au kuondoa malalamiko yaliyopo sasa ya ukiukwaji wa haki mbalimbali na misingi ya utawala bora.

Lakini kibaya zaidi ni kuwa kutokuwepo kwake, kunawakosesha watendaji katika ngazi mbalimbali na mihimili ya uongozi fursa ya ushauri kuhusiana masuala mbalimbali ya haki na utawala bora.

Ikumbuke kuwa THBUB inayofanya kazi pande zote za Muungano, ni chombo huru cha Serikali kikiwa na majukumu ya kuhamasisha, kulinda na kutetea haki za binadamu kama zilivyoainishwa ndani ya Katiba yetu ya mwaka 1977 na mikataba mbalimbali ya Afrika na Umoja wa Mataifa ambayo Tanzania imeridhia.

Wengi ni mashuhuda wa namna tume kwa nyakati mbalimbali ilivyokuwa mstari wa mbele kukosoa, kuelimisha na kuelekeza kuhusu masuala mbalimbali ya ukiukwaji wa haki za binadamu na utawala bora. Matamko mengi ya kimdomo na kimaandishi yalizoeleka kutoka tume yakilenga kuturudisha Watanzania katika mstari wa kujali haki na utawala wa sheria.

Kasi ya kuirudisha Tanzania ya maadili hasa kwa viongozi kwenye mstari aliyoanza nayo Rais John Magufuli, inapaswa kupata usaidizi wa kutosha wa kimfumo na kitaasisi.

Moja ya taasisi inayoweza kumsaidia Rais katika dhamira yake ya kuisafisha Tanzania na kuwa na nchi yenye mwelekeo mpya, ni tume hii ambayo kimsingi ndiyo mhimili na msimamizi wa utekelezwaji wa haki na utawala bora nchini.

Tunapotambua kuwa Rais yumo bado kwenye mchakato wa kuunda Serikali yake kama taasisi makini na yenye watendaji mahiri na walio na utayari wa kufanyia kazi maono yake mema kwa Taifa, tunadhani mchakato wake wa kuteua watendaji katika maeneo mbalimbali utupie jicho kwenye tume hii.

Mwaka mmoja bila ya kuwapo kwa chombo kinachosimamia haki na utawala bora, ni pengo kwa Taifa ambalo pamoja na mambo mengine linafifisha dhamira za Rais kuelekea katika Tanzania inayozingatia usawa na haki kwa wote.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647