Idara ya uvuvi iangalie njia bora ya kudhibiti uvuvi haramu

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Thursday, June 7  2018 at  09:28

Kwa Muhtasari

Maofisa wa Idara ya Uvuvi katika mikoa ya Mwanza, Geita na Mara wameanza kutoa vibali kwa wananchi wanaotaka kusafirisha samaki wa kitoweo kwa familia, ndugu na jamaa kama moja ya njia za kukabiliana na uvuvi haramu.

 

MBINU hii mpya ya kupambana na uvuvi haramu inawahusu wasafirishaji wa samaki kwa ajili ya matumizi ya familia au zawadi kwa ndugu na jamaa zao. Vibali hivyo, vinavyotolewa bure, vinalenga kuwaondolea usumbufu wananchi wakati wa ukaguzi kwenye vyombo vya usafiri vya majini, angani na nchi kavu.

Vibali hivyo vinatolewa kwa samaki wasiozidi kilo 15 wanaosafirishwa nje ya wilaya kwa ajili ya kitoweo ili kuwaondolea usumbufu njiani.

Si lengo letu kupinga juhudi za Serikali za kupambana na uvuvi haramu, lakini ni vyema jitihada hizo zisiwaumize wananchi wasio na hatia, kama wajasiriamali na watumiaji wa kitoweo hicho.

Tunaunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali, hasa waziri mwenye dhamana na uvuvi, Luhaga Mpina ambaye wakati akijibu hoja za wabunge waliolalamikia awamu ya kwanza ya operesheni Sangara mwaka 2018, alisisitiza kuendelea kupambana na uvuvi haramu.

Hata hivyo, dosari tunayoiona ni mkakati mpya ulioanzishwa na maofisa wa idara hiyo wa kutoa vibali vya samaki wa kitoweo. Wengi wanaosafirisha samaki kwa ajili ya matumizi ya majumbani au zawadi ni wasafiri na mara nyingi huwanunua muda mfupi kabla ya kuanza safari.

Kwa maana hiyo, muda huo wa kuomba vibali hadi kukubaliwa unaweza kuwa mdogo kwa kuwa huenda mikoa hiyo kwa shughuli nyingine za kikazi na si kufuata samaki.

Pia, hofu yetu ni kwamba nia nzuri ya Serikali inaweza kutumika vibaya kwa vibali kuchelewa kutolewa au kuwakatisha tamaa wanunuzi. Wanunuzi wengi hasa wasafiri wa anga huwanunua alfajiri ya siku ya safari kwa hiyo ni vigumu kwao kutafuta vibali na kuvipata katika muda huo mfupi. Hofu nyingine ni wauzaji wa samaki ambao wengi ni kinamama kupungukiwa wateja.

Ombi letu kwa wizara ni kuangalia njia bora zaidi ya kudhibiti uvuvi haramu, lakini bila ya kuathiri wajasiriamali, walaji na kuua utamaduni wa Watanzania wa kuchukuliana zawadi wakati wa safari.

Tunaamini Serikali inaweza kutoa mwongozo mzuri wa namna ya kuondoa usumbufu kama huo.

Pia, tunauona ugumu huu kwa upande wa Serikali kwamba itakuwa na kazi ya ziada kuweka maofisa wake kwenye kila kituo cha usafiri, kwanza gharama na vilevile idadi ya maofisa. Hivyo ni vyema vibali hivyo vikaondolewa kama ilivyoruhusiwa kusafirisha tani moja ya mazao ya kilimo bila kulipa ushuru.

Hata hivyo, kama Serikali ina maofisa wa kutosha kuwekwa kwenye kila kituo cha usafiri, ni vyema ikafanya hivyo, lakini uwezo huo kama haupo itafutwe njia rafiki itakayoondoa usumbufu na hali kadhalika kutimiza lengo lililokusudiwa la kudhibiti uvuvi haramu.

Wakati akijibu hoja za wabunge, Mpina alisema katika Operesheni Sangara walikamata magari ya baadhi ya wabunge, wenyeviti wa halmashauri, vijiji, madiwani na watendaji yakiwa na samaki waliotokana na uvuvi haramu. Hao ndio wa kuanza nao kama mfano.

Tunachokiona hapa kabla ya kuanza na mkakati mwingine ni vyema wizara ikapima mafanikio ya operesheni hiyo kwanza, ili kupata picha ya hatua gani zifuate kuboresha zaidi vita dhidi ya uvuvi haramu bila ya kuathiri maisha ya wakazi.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647