Uwekezaji maji safi na salama utaokoa maisha ya Watanzania

Maji

Maji kutoka kwa mfereji. Picha/HISANI 

Na TAHARIRI YA MWANANCHI

Imepakiwa - Thursday, October 5  2017 at  11:27

Kwa Mukhtasari

Katika siku tatu mfululizo tangu Jumatatu, gazeti la Mwananchi limekuwa likichapisha ripoti maalumu kuhusu afya hasa uhaba wa maji vijijini, hususan katika Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.

 

KATIKA siku tatu mfululizo tangu Jumatatu, gazeti la Mwananchi limekuwa likichapisha ripoti maalumu kuhusu afya hasa uhaba wa maji vijijini, hususan katika Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.

Nachingwea ambayo asilimia 55 ya wakazi wake wanaishi vijijini hawana majisafi na salama ikilinganishwa na asilimia 29 ya wenzao wanaoishi mijini.

Ni mfano tu wa maeneo mengi nchini ambao wananchi wake wanateseka kwa kutembea umbali mrefu kusaka huduma hiyo muhimu kwa afya ya binadamu.

Hii ni kuonyesha kuwa wastani wa asilimia 72 ya wakazi wa vijijini wanapata maji safi na salama.

Mbali na kuwapoteza muda wa kufanya kazi za uzalishaji mali, pia tunaona uhaba wa maji unavyohatarisha afya za watu kwa kusababisha magonjwa ya matumbo kwa kuwa wengi wanatumia vyanzo visivyo salama na hawatibu maji wakati wa kuyanywa.

Tunafahamu kuwa bado kuna watu wengi ambao hawana uelewa wa umuhimu wa kuchemsha maji ya kunywa kabla ya kuyatumia au kuyatibu kabla ya kuyatumia kwa kuweka dawa ya kuua vijidudu kama ‘waterguard’.

Wataalamu wanaeleza kuwa sehemu kubwa ya magonjwa ya kuhara yanasababishwa na watu kutumia maji machafu.

Kwa mfano takwimu za Halmashauri ya Nachingwa zinaonyesha kuwa kati ya Januari hadi Machi kuhara ulikuwa ni miongoni mwa magonjwa matatu makubwa yaliyowatesa zaidi wakazi wake.

Tunaamini kuwa watu hao huenda wasingeugua ugonjwa wa kuhara kama Serikali ingepeleka huduma ya maji safi na salama katika maeneo ya ndani ya mita 400 kutoka kwenye makazi yao kama sera ya Maji inavyeleza.

Pia, ufinyu wa bajeti nao ni tatizo.

Kwa mfano bajeti kwa mwaka wa fedha 2016/17 ilitengwa TSh 939 bilioni kwa ajili ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji lakini hadi Machi ilikuwa imetolewa TSh184 bilioni sawa na asilimia 19 tu ya fedha zote. Ikumbukwe kuwa hapa ilikuwa imesalia miezi mitatu kwa mwaka wa fedha kikamilika.

Japo Serikali inaendelea kuboresha huduma za majisafi na salama kama ambavyo viongozi wamekuwa wakieleza tunaona kuwa kasi ya uwekezaji wake haiendani na kiwango ha mahitaji.

Sio kuwa tunapuuza kinachofanyika, la hasha.

Tunataka kile kilichoahidiwa kitekelezwe kwa kuwa ni wajibu wa Serikali kutoa huduma kwa wananchi wake.

Tunachoona uwekezaji huu wa ahadi hauwezi kusaidia kumaliza tatizo la maji hasa kwenye maeneo yenye uhaba mkubwa wa maji  kama Lindi na Mtwara ambayo baadhi wanategemea maji ya ardhini  kutokana na kukosa vyanzo vya asili kama mito na maziwa.

Uwekezji huu wa kusuasua unaweza pia kukatisha tamaa wadau wanaoshirikiana na Serikali kuongeza upatikanaji wa maji vijijini kwa kuwa mwagiliaji mkuu hatekelezaji ahadi zake kwa wakati.

Ili kutokomeza umaskini na maradhi vijijini uwekezaji wa huduma za jamii  kama majisafi na salama na elimu ni muhimu iwapo kuna nia ya dhati ya kuwa na nguvukazi yenye afya bora itakayoipeleka Tanzania kwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au 0754780647