http://www.swahilihub.com/image/view/-/4132886/medRes/1776337/-/15rsroqz/-/maji.jpg

 

Vijana wa maji mitaani ni wajenzi wa kweli wa taifa

Toezz

Sammy Ng'ang'a huuza maji Toezz, Ruiru, Kaunti ya Kiambu. Assubiri wateja. Upungufu na ukosefu wa maji Nairobi na Kiambu ni fursa ya vijana kujipatia ajira. Picha/SAMMY WAWERU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Tuesday, October 10  2017 at  11:23

Kwa Mukhtasari

Mwaka mmoja sasa umekamilika tangu uhaba wa maji uanze kushuhudiwa katika Kaunti ya Nairobi.

 

MWAKA mmoja sasa umekamilika tangu uhaba wa maji uanze kushuhudiwa katika Kaunti ya Nairobi.

Kampuni inayosambaza maji ya Nairobi Water & Sewerage Company, Nairobi na katika kaunti jirani ilikuwa imefahamisha wateja wake kuwa maji yataanza kudhibitiwa na kusambazwa kwa awamu kuanzia Desemba 2016.

Uhaba wa maji Nairobi umekuwa ukishuhudiwa tangu miaka miwili iliyopita.

Upungufu wa raslimali hii unaonekana kukita mizizi ambapo baadhi ya sehemu zinamaliza wiki mbili pasi hata kupata tone la maji.

Je, unafahamu kwamba upungufu na ukosefu wa maji sasa umekuwa nafasi za ajira kwa vijana wanaochuuza kwa kutumia mkokoteni?

Taswira inayokukaribisha katika mingi ya mitaa Kaunti ya Nairobi na jirani yake ya karibu Kiambu, ni mikokoteni 'iliyopambwa' kwa mitungi ya rangi aina ya manjano, na iliyoegeshwa nje ya ploti nyingi.

Vijana wanaovuta ama kusukuma mikokotenj hiyo wakisuburi wateja wa kununua maji, ambayo yamekuwa kitega uchumi chao na kuwazimbulia riziki pamoja na familia zao.

Amini usiamini vijana hao wanatia mfukoni kitita kizuri cha pesa kupitia uchuuzi huo.

Ni majira ya saa sita za mchana tunapatana na Bw Sammy Ng'ang'a mchuuzi wa maji Toezz, Ruiru Kiambu, akisubiri wateja wake. "Nina wateja waaminifu ambao hawajawahi 'niangusha'. Nimekuwa nikichuuza maji kwa ipatanayo miaka miwili sasa iliyopita. Maji yana donge nono, yanapopungua tunasema kahawa yetu 'imeiva'," asema mfanyabiashara huyu kwenye mazungumzo ya kipekee na Swahilihub.

Nje ya ploti moja, Ng'ang'a ameegesha 'gari lake' aina ya mkokoteni lililojaa takriban mitungi 25 hivi, kando yake mingine karibu 40, yote ikiwa na maji ambayo ndiyo uhai kwa insi.

Baada ya kukamilisha mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) mwaka wa 2014, Ng'ang'a alihamia na kupiga kambi jijini Nairobi kutoka mjini Nyeri, kuenda kutafuta ajira, akishikilia kauli 'mwanamume ni bidii'.

"Uchuuzi wa maji ndio kazi ya kwanza iliyonikaribisha jijini. Niliifanya kwa miezi 6 pekee mwaka wa 2015. Niliweka akiba na zilipofikia sh1,500 zikawa mteja wangu wa kuwa mchuuzi binafsi wa maji. Nilinunua mitungi 15, kila mmoja ukiwa wa lita 20," aeleza.

Kila mtungi aliuziwa sh80, hii inamaanisha alisalia na sh600 ambazo aling'oa nanga nazo.

"Nilikuwa nimeshajuana na wauzaji wa maji ambao kiini chayo hakiishi. Waliniamini kiasi kwamba ningekuwa na deni walijua ningewalipa tu," akaeleza Ng'ang'a.

Mtungi mmoja wa maji kwa sasa unauzwa kati ya sh20-30, mchuuzi huyu hununua mmoja kwa Sh5.

Sh2,000 kwa siku

Kulingana na Ng'ang'a, 23, kwa siku huuza zaidi ya mitungi 100; hii inamaanisha hutia kibindoni Sh2,000 kwa siku.

"Kwa nini niasi kazi hii ama nikae bure bilashi nikiongoja serikali ibuni kazi, ilhali 'ofisi' hii inanipa hata zaidi ya sh3,000 kwa siku? Vijana hudunisha kazi za juakali na ndizo zenye pesa kuliko zile za ofisi," ashauri Ng'ang'a.

Kijana huyu asema awali alikuwa akikomboa mkokoteni, lakini kwa sasa ameweza kununua wake binafsi.

Hata hivyo anafahamu fika kuwa kila kazi ina pandashuka zake. "Kazi bila changamoto si kazi. Msimu wa mvua biashara huwa chini sana. Vile vile viongozi waliochaguliwa wakiangazia upungufu wa maji huenda ajira yetu ikaisha, kwa hivyo itabidi tujipange kwa ajira zingine," adokeza.

Baada ya kuapishwa kuchukua hatamu ofisi mwezi Septemba 2017, Gavana mpya wa Nairobi Mike Sonko na mwenzake wa Kiambu Ferdinand Waititu waliahidi kutatua upungufu na ukosefu wa maji.

Chanda chema huvishwa pete, juhudi za Bw Ng'ang'a ndizo zimemfanya kuangaziwa katika mtandao huu wa Swahilihub, kutoka kwetu tunamtakia kila la heri anapozimbua riziki.