http://www.swahilihub.com/image/view/-/4752170/medRes/2105051/-/gsppf9z/-/mtaka.jpg

 

Viongozi, watendaji waige mfano wa Mtaka

Antony Mtaka

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka. Picha/MAKTABA 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Wednesday, September 12  2018 at  08:47

Kwa Muhtasari

  • Rais John Magufuli amemsifu Anthony Mtaka, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu
  • Wiki iliyopita, Rais Magufuli alimpongeza Mtaka kwa utendaji wake akisema kwa mujibu wa ripoti aliyonayo anakuwa mkuu wa mkoa namba moja au mbili, licha ya kwamba alikuwa ameshauriwa asimteue kwa madai kwamba hafai hata kuwa mkuu wa wilaya

 

MARA nyingi anapokuwa ziarani Rais John Magufuli tunamsikia akiwakosoa baadhi ya viongozi wa kisiasa na watendaji aliowateua kwa kushindwa kumsaidia kufanikisha malengo yake mbalimbali.

Hata hivyo, wapo ambao tumemsikia akiwasifia kwa kufanya kazi vizuri kulingana na mahitaji na maelekezo yake.

Miongoni mwa waliosifiwa katika siku za karibuni kabisa ni Anthony Mtaka, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

Akiwa mkoani humo wiki iliyopita, Rais Magufuli alimpongeza Mtaka kwa utendaji wake akisema kwa mujibu wa ripoti aliyonayo anakuwa mkuu wa mkoa namba moja au mbili, licha ya kwamba alikuwa ameshauriwa asimteue kwa madai kwamba hafai hata kuwa mkuu wa wilaya.

Kwanza sisi tunampongeza Mtaka kwa utendaji wake wa kazi ambao mbali na kuonwa na Rais mwenye vyombo vingi vya kumshauri, vilevile unaonekana na kuelezeka hata kwa watu wengine wa kawaida.

Pamoja na pongezi hizo tunamshauri asivimbe kichwa na kutoka ndani ya mstari kama ambavyo imewahi kutokea kwa baadhi ya watu waliowahi kusifiwa siku za nyuma.

Akiwa katika mkoa mpya ambao ameuanzisha, Mtaka amejipambanua kama kiongozi mwenye dira inayoeleweka na anayeisimamia utekelezaji wake bila kutafuta sifa binafsi au za kisiasa.

Mtaka ameonyesha njia ya kuelekea katika Tanzania ya viwanda inayopiganiwa na Rais Magufuli kwa vitendo, akiwa amesimamia kuanzishwa kwa viwanda vya chaki, maziwa, viatu na vingine vya kusindika nafaka. Yeye anapigania viwanda, hasa vile ambavyo vitapata malighafi kutoka katika eneo husika ambavyo vitaongeza ajira na kuinua uchumi wa wananchi wa Simiyu.

Ameonyesha mfano wa kuleta matokeo bora katika elimu kwa kuongeza udahili wa wanafunzi wa shule za msingi na kuanzisha makambi ya wahitimu wa madaraja mbalimbali ambayo tayari yameanza kuonyesha matunda mazuri.

Ni mkuu wa mkoa ambaye ameeleza wazi kuhusu umuhimu wa kuwaheshimu watendaji wa Serikali katika eneo lake akisema hataki kusikia wanawekwa ndani ovyo akisisitiza kuwa mamlaka za kinidhamu ziheshimike na kuzingatiwa.

Amesikika mara kadhaa akisema hataki kusikia wakuu wa wilaya walio chini yake wakiwaweka ndani watendaji hao, bali wajihusishe na shughuli za maendeleo, ikiwa ni kuzifanya wilaya kuwa zao maalumu linaloshawishi uanzishaji wa kiwanda.

Si hayo tu, hatujamsikia kiongozi huyo akijihusisha na masuala ya kupambana wazi na vyama vya siasa bila sababu za msingi, masuala ambayo yanajitokeza katika maeneo mbalimbali nchini.

Akiwa tayari ameandaa mwongozo wa uwekezaji katika Mkoa wa Simiyu, hivi karibuni amefanikisha shughuli za maonyesho ya Nanenane kitaifa, licha ya upya wa mkoa wake. Katika maandalizi yake alipanga kufaulu kuyafanya maonyesho hayo kuwa na sura tofauti iliyokuwa imezoeleka katika mikoa mbalimbali iliyowahi kuwa mwenyeji.

Pamoja na kwamba Rais ana aina ya vigezo vyake anavyovihitaji katika kupata watendaji, tunaamini mambo hayo aliyoyafanya Mtaka ni miongoni mwa mengi yaliyomfanya Rais Magufuli amsifie, hivyo yanapaswa kuigwa na viongozi wengine serikalini kwa kuwa pia yanakubalika na kusifiwa na wananchi, wakiwamo wanasiasa wa vyama tofauti.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647