http://www.swahilihub.com/image/view/-/3149788/medRes/1297446/-/132ql9l/-/viti.jpg

 

Uchambuzi: Viongozi wa kidini waongoze vizuri waumini

Viti vya Kanisa

Viti vya Kanisa. Picha/HISANI 

Na JONATHAN MUSA

Imepakiwa - Friday, February 1  2019 at  11:05

Kwa Muhtasari

Viongozi kwenye taasisi za dini wana jukumu la kulinda, kuelekeza, kufundisha na kutoa miongozo kwa waumini wao ili mambo yaende vizuri.

 

KWA kawaida, kwenye taasisi za dini kuna waumini na viongozi mbalimbali.

Viongozi hawa wana jukumu la kulinda, kuelekeza, kufundisha na kutoa miongozo kwa waumini wao ili mambo yaende vizuri. Kupitia maelekezo hayo, waumini wanapata ‘chakula cha kiroho’ na pia kuishi kimaadili kwa mujibu wa maagizo ya Mungu.

Kama ilivyo kwa wasanii nchini, hufundwa na huangaliwa mienendo yao na Baraza la Sanaa Tanzania (Basata).

Mwaka 2018 tuliona baraza hilo likifungia kazi za wasanii kwa kutunga nyimbo zisizo na maadili katika jamii.

Hata hivyo, mbali na onyo hilo, sijawahi kuwasikia Basata kutoa zawadi kwa wasanii wa muziki wanaofanya vizuri katika kazi zao kama kuwatunza ala za muziki, vyeti na vitu vingine.

Wasanii wengi wanachukulia kazi zao kama sehemu ya kuwafurahisha mashabiki wao, hivyo hawajali kuhusu utunzi wa nyimbo husika kama unaelimisha jamii au la.

 

Maadili

Nchi zingine mfano Ghana, Botswana, Zimbabwe na hata Uganda mamlaka husika zina utaratibu maalumu wa kuwakosoa, kuwatunza na kuwapiga msasa wasanii kupitia semina mbalimbali kwa lengo la kuendana na maadili.

Pia, nchi hizo zinatambua kila kitu kinaenda na wakati uliopo hasa kutokana na utunzi, hivyo utaratibu mwingine hufuatwa kwa kuwa wasanii hao wanachangia pato la Taifa la nchi zao.

Kwa hapa nchini imekuwa kama mchezo wa paka na panya. Nafahamu kuwa kuna wasanii wanaofanya kazi ili ziendane na zile za kimataifa, lakini wapo wanaofanya makusudi kwa kukiuka maadili ili waone Basata watafanyaje.

Hata hivyo, Basata wamekuwa wakiingilia kati pindi wanapoona wimbo hauna maadili kwa kuwatoza wasanii faini na wakati mwingine kufungia nyimbo.

Binafsi, naishauri Basata ijenge mustakabali wa kutoa mafunzo kwa wasanii kuhusu namna ya kufanya kazi zao badala ya kuzifungia bila kurekebisha chanzo.

Kwa mfano, mwaka jana wasanii Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz na Raymond Mwakyusa (Rayvanny) walifungiwa wimbo wao huko Mwanza kutokana na kutokuwa na maudhi yenye maadili katika jamii.

Wimbo huo ulifungiwa hadi kwenye televisheni na mtandao wa kijamii wa Youtube hapa nchini ili usitazamwe na usisikilizwe kwenye redio.

Wasanii hao walidaiwa kuuimba wimbo huo mkoani Mwanza katika Tamasha la Wasafi Festival na kubainika kwamba wamekiuka taratibu kwa mujibu wa Basata.

Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Basata kuwafungia wasanii kwenye baadhi ya nyimbo zao.

Pia, Januari 22, Basata iliwafungulia wasanii hao (Diamond na Rayvanny) kuendelea na kazi zao za sanaa huku ikiwata wafuate taratibu zilizoweka ili wafanye kazi zao bila kubughudhiwa.

Suluhu siyo kuwafungia wasanii hawa tu, bali ujengwe uhusiano mwema baina yao na baraza na kuwapa elimu.

Wasanii wana haki ya kushauri na kuzungumza na Basata kama mtu na rafiki yake.

Hata hivyo, sitaki kuamini kama Basata wana uwezo wa kupitia kazi zote za wasanii nchini na kuziweka wanavyotaka, hakika hicho ni kibarua maana wasanii ni wengi.

Kitendo cha Basata kuhakiki nyimbo zote Tanzania kabla ya kwenda hewani ni mtihani, jambo la msingi ni wao kujigawa na kuanza kutoa elimu pamoja na kuwatuza waliofanya vizuri katika utunzi ili kuhamasisha wengine kuiga.

Kama hakutakuwa na njia mbadala ya kuwafunda wasanii zaidi ya kufungia nyimbo, kuna hatari ya wasanii wakubwa kuhamia nchi zingine ili kuwa huru kufanya kazi zao huko.

Mabadiliko

Kwa sasa mambo yamekwishabadilika na ili upate kipato kizuri, sharti la kwanza lazima uendane na kinachofanyika kimataifa.

Mifano ya wasanii wakubwa ipo na kwa hakika mara kadhaa wanapiga ‘shoo’ zao Nigeria, Kenya na kwingineko.

Ni wakati sasa wasanii wajenge uhusiano bora na mamlaka husika ili waboreshe kazi zao pamoja na kufanya majadiliano na sababu kuntu za kutoa aina fulani ya kazi (wimbo), kabla haujaenda hewani (redioni, kwenye televisheni na Youtube).

Basata nao waangalie namna ya kukabiliana na aina ya kazi potofu ambazo baadhi ya wasanii huzifanya kwa makusudi.

Wito wangu kwa nguzo hizi mbili ni kukaa pamoja na kuzungumza ili wapate suluhu ya kudumu kuepuka kufungia nyimbo za wasanii ambazo wanakuwa wametumia gharama kubwa kuzirekodi.

 

Jonathan Musa ni mwandishi wa “Mwananchi” mkoani Mwanza, anapatikana kwa simu namba +255744-205617