http://www.swahilihub.com/image/view/-/3406064/medRes/1168738/-/3t9je1/-/MagufuliRais.jpg

 

Viongozi wasioweza kasi ya JPM wapumzike

Rais John Magufuli akitoa hotuba

Rais John Magufuli akihutubu awali. Picha/AFP 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Thursday, January 31  2019 at  12:07

Kwa Muhtasari

Shule kukosa vyoo sio tatizo la kumlazimu mkuu wa nchi aingilie kati.

 

KWA mara nyingine Rais John Magufuli amesikika akieleza namna alivyolazimika kuingilia kati kushughulikia kilio cha wananchi, licha ya kuwapo viongozi wa chini aliowateua kumsaidia.

Rais Magufuli alibainisha kwamba aliona habari kwenye televisheni iliyowaonyesha kinamama mjini Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa wakilalamikia kitendo cha kupewa dhamana mtu wanayemtuhumu kuwabaka mabinti zao.

Alisema kwa mujibu wa kinamama hao mtuhumiwa amebaka wasichana 11 na kila anapokamatwa walishangaa kumuona akirejea mtaani akiwa huru.

Rais Magufuli alisema baada ya kuona habari ile, aliwasiliana na Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda na kumuomba kwenda Mufindi kushughulikia tatizo hilo ili mtuhumiwa akamatwe na suala hilo lianze upya kushughulikiwa.

Tunachokiona hapa, uamuzi wa Rais Magufuli kumtuma Pinda kwenda kushughulikia tatizo ambalo liko chini ya uwezo wa viongozi wa wilaya au mkoa, maana yake ni kuwa kuna ombwe la kiuongozi katika ngazi za chini.

Kuna wakati Rais alipokuwa ziarani mkoani Morogoro, mwanafunzi wa kidato cha kwanza alijitokeza kwenye mkutano wake na kumweleza mkuu huyo wa nchi kwamba shule yao ina ukosefu wa vyoo, hivyo awasaidie.

Kukosa choo

Shule kukosa vyoo sio tatizo la kumlazimu mkuu wa nchi aingilie kati, hili ni jukumu linalopaswa kushughulikiwa na wasaidizi wake wakiwamo wakuu wa wilaya na mikoa, au wawakilishi wa wananchi kama madiwani, wabunge na watendaji wengine wa ngazi za mitaa na vijiji.

Ombwe hilo linajidhihirisha zaidi baada ya Rais Magufuli kumtumia Pinda, tena kiongozi mstaafu kutatua tatizo linalohusu jinai na sheria za kulishughulikia zikiwapo. Kilichokosekana ni utashi wa watendaji wa eneo hilo kulishughulikia suala hilo.

Hoja iliyopo ni kuwa, hali hii itaendelea hadi lini? Rais Magufuli ataendelea kufanya kazi za watendaji wake wa chini hadi lini?

 

Kero

Tunajiuliza viongozi wanaomwakilisha Rais kama vile wakuu wa mikoa na wilaya wanafanya kazi gani katika kutatua kero za wananchi? Kwa nini wanamuongezea mzigo Rais awafanyie kazi zao ambazo ni sehemu ya majukumu yao ya kila siku?

Rai yetu kwa wasaidizi wa Rais kwenye ngazi zote ni kuwa, fanyeni kazi kuwatembelea wananchi na muwasikilize matatizo yao ili kujua nini kinawasibu badala ya kutoa maelekezo na amri zisizokuwa na tija.

Hatuoni kama ni afya kwa Taifa ikiwa wananchi watakuwa wakihifadhi kibindoni kero zao hadi pale Rais anapofanya ziara katika maeneo yao au anapoona kwenye vyombo vya habari.

Tunajua kuna baadhi ya wakuu wa mikoa au wilaya wanafanya vizuri kwenye maeneo yao, wanawasikiliza wananchi, wanawatembelea na kuwafuatilia watendaji wengine serikalini wanaokwamisha juhudi za Rais Magufuli za kuwatetea wananchi wanyonge, lakini kwa nini wengine hawafanyi hivyo?

Kuna baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakisema yeyote anayejiona hawezi kwenda na kasi ya Serikali ni bora akae pembeni. Hii ni kweli, nasi tunakubaliana nao ili kutorudisha nyuma juhudi za maendeleo zinazofanyika.

Ni fedheha kwa kiongozi au mtendaji wa Serikali kuondolewa kwenye wadhifa wake kwa utendaji dhaifu, lakini ni ushujaa kuomba kupumzika na kuwapisha wanaoweza kulisukuma gurudumu la maendeleo kwa kasi inayotakiwa.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647