http://www.swahilihub.com/image/view/-/4645942/medRes/2032608/-/godciw/-/papatia.jpg

 

Jinsi ya kuandaa vipapatio vya kuku vilivyopakwa mayai

Vipapatio vya kuku

Vipapatio vya kuku vina ladha tamu sana vikitayarishwa na mpishi mbobevu. Picha/HISANI 

Na MARGARET MAINA

Imepakiwa - Wednesday, July 4  2018 at  11:14

Kwa Mukhtasari

Vipapatio vya kuku vina ladha tamu sana vikitayarishwa na mpishi mbobevu.

 

KUKU ni miongoni mwa nyama nzuri sana kwa afya zetu. Unaweza kula nyama ya kuku ambayo imeandaliwa kwa kufuata utaratibu wa mapishi mbalimbali na mitindo mbalimbali kwa kutegemea wewe mwenyewe unatakaje. Unaweza ukachemsha, kukaanga, kuchoma, kupika na kadhalika na ukapata ladha nzuri na virutubisho vya kutosha mwilini. Kumbuka kwamba nyama ya kuku ina kiasi kingi cha protini na vitamini ‘Niacin na Vitamini B6’.

 

Kuandaa: Dakika 15

Mapishi: Dakika 45

Walaji: 2

Hizi chicken wings unachovya kwenye mayai kisha unazikaanga kwa muda mfupi kwenye siagi. Baada ya kukaanga vipapatio hivi unafaa kuvichovya kwenye sauce na kisha kuvioka.

 

Vinavyohitajika

  • Vipapatio vya kuku kilo moja
  • Yai moja
  • Kikombe kimoja cha unga wa ngano utakaotumia kuweka utando (layer) juu ya kuku
  • Kikombe kimoja cha siagi

Mahitaji ya sauce

  • Vijiko vitatu vikubwa vya soy sauce
  • Vijiko vitatu vikubwa vya maji
  • Kikombe kimoja cha sukari
  • White vinegar nusu kikombe
  • Kitunguu saumu cha unga katika kipimo nusu kijiko kidogo
  • Chumvi kijiko kimoja kidogo

Maelekezo

Washa ovena kwenye nyuzijoto 175°C, acha ipate moto.

Kata vipapatio vya kuku (chicken wings) katikati, chovya kwenye mayai na kisha chovya kwenye unga. Hakikisha mayai na unga umeenea vizuri.

Bandika chombo mekoni kwenye moto wa wastani, acha kipate moto kisha weka siagi. Acha iyeyuke. Weka vipapatio ya kuku na kanga hadi vibadilike rangi. Epua na weka kwenye waya wa kuokea.

Kwenye bakuli la wastani, changanya soy sauce, maji, sukari, vinegar, kitunguu saumu, na chumvi. Koroga vizuri hadi mchanganyiko uwe sawia. Nyunyizia sauce juu ya vipapatio vya kuku.

Weka vipapatio kwenye ovena, oka kwa muda wa dakika 30 hadi 45. Weka sauce juu ya vipapatio mara kwa mara. Vikiiva epua na weka pembeni.

Mlo uko tayari. Unaweza kupakua na wali, pasta au ugali na mboga za majani.