Vita vya Kalamu

Kalamu

Kalamu. Picha/MAKTABA 

Na PHYLLIS MWACHILUMO

Imepakiwa - Wednesday, April 12  2017 at  17:10

Kwa Mukhtasari

Ni uwezo walionao wanafasihi kujieleza kwa kutumia kalamu zao.

 

NI uwezo walionao wanafasihi kujieleza kwa kutumia kalamu zao.

Wao huweza kutokeza wazi mawazo yao yakawa yenye kuufanya umma kuwaza zaidi juu ya hili na lile.

Ni vita ambavyo huwezesha watu kupigania haki zao bila ya kumwaga damu hata tone ingawa vita hivi pia huweza kuchochea umwagaji wa damu ya anayeviendeleza ikiwa wino wake hatauelekeza kufaako.

Wanafasihi, kupitia mashairi, tamthilia na kazi zao nyingine za kifasihi, huweza kuonyesha wazi (na kwa njia fiche), maovu na dhulma katika jamii.

Ni muhimu yale wanayoandika yaweze kusambaa zaidi miongoni mwa wanajamii wote. Lakini vipi?

Njia mojawapo ni elimu, elimu ya shule iendeleze usomaji wa kazi za fasihi kama ilivyo sasa hivi.

Usomaji huu huweza kuwafungua macho vijana katika taifa ili wajionee hali halisi katika taifa lao kwa nia ya kuwa pengine watakuwa na hamu ya kutaka kubadilisha hali.

Huenda kuwa haya hayatoshi kwani jamii inaendelea tu na hali yake ya kawaida hata baada ya mamilioni ya vijana kupitia mfumo huu wa elimu.

Pengine inahitajika watu waliokomaa zaidi wakumbushwe yale wanayotakiwa kuyapigania kupitia usomaji wa kazi za kifasihi.

Kuwafanya kuendeleza mabadiliko yafaayo bila kukata tamaa.


Dhima

Vita hivi vya kalamu hupigania mengi zaidi ya haki kupambana na maovu. Huweza kupigania mapenzi baina ya wawili.

Kuwakumbusha juu ya utamu wa mahaba kupitia ushairi mtamu na wenye faraja.

Hivi vyote ni vita vya kalamu vinavyostahili kuendelezwa na wote wawe wake au waume.

Ni vita vya kifahari vinavyohitaji mtu kujitia kwenye mizani ili aepuke kujipiga mwenyewe kwa kuwaudhi walewale anaowaandikia.

Vinahitaji makini na kujijua ili usije ukawa unauonyesha ujunga wako kupitia unayoyaandika.