http://www.swahilihub.com/image/view/-/4842778/medRes/2160906/-/x0xp8dz/-/makonda.jpg

 

Wadau wamuweka njia panda Makonda

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda  

Na Elizabeth Edward, Mwananchi

Imepakiwa - Thursday, November 8  2018 at  16:04

Kwa Muhtasari

Analaumiwa na baadhi kuwa amekuwa na kiburi; anafanya anavyotaka huenda kwa sababu anajua haguswi.

 

eedward@mwananchi.co.tz

SIKU chache baada Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kueleza kuwa kampeni ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutokomeza vitendo vya ushoga si msimamo wa serikali, wadau mbalimbali wameeleza namna walivyopokea uamuzi huo.

Walidai baadhi ya kauli na uamuzi wa mkuu huyo wa mkoa umekuwa na maswali yasiyo na majibu na wakati mwingine kuiweka nchi njia panda hususani katika mahusiano ya kimataifa.

Hatua hiyo imetokana na kampeni yake ya hivi karibuni ya kupambana na ushoga ambapo aliwataka wakazi wa mkoa wake kumtumia majina ya watu wanaojihusisha na vitendo hivyo.

Makonda aliitisha mkutano na vyombo vya habari na kuelezea namna alivyojipanga kutekeleza kampeni hiyo huku akitaja baadhi ya majina ya watu wanaodaiwa ni mashoga na kusisitiza mkoa wake hautaruhusu vitendo hivyo.

Vyombo vya habari vya kimataifa viliripoti kuhusu kampeni hiyo huku vikionyesha hatari ambayo itawakabili wanaojihusisha na ushoga.

Hata hivyo, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ilikana kuhusika na kampeni hiyo na kueleza kuwa inafanywa na Makonda kwa utashi wake na si msimamo wa nchi.

Msimamo huo wa Serikali unaashiria kuwa Makonda anaelekea kukwama kwenye kampeni hiyo na huenda ukawa mwendelezo wa kushindwa kutekelezeka kwa mipango yake mbalimbali anayoipanga.

Akizungumza na Mwananchi mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa Gaudence Mpangala alisema anashangazwa kuona Makonda akiendelea kutoa kauli na kuendesha operesheni zenye utata ambazo zinaweza kuigharimu nchi kimataifa.

“Binafsi naona uongozi wake una udhaifu, anavuruga katika mambo mengi ingawa ameendelea kuwepo. Kuna mambo ya msingi ambayo yanahitaji msimamo wa Serikali si kwa sababu wewe ni mkuu wa mkoa ufanye kila uamuzi kwa utashi wako,” alisema.

Kauli hiyo iliungwa mkono na mwanaharakati Dk Hellen Kijo Bisimba aliyeeleza kuwa Makonda anafanya anavyotaka kwa kuwa hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yake.

Alisema mambo yanayofanywa na Makonda sasa yanaenda kugusa masuala muhimu ambayo yanaweza kuiweka nchi katika wakati mgumu mbele ya jumuiya za kimataifa.

“Amekuwa kiburi anafanya anavyotaka huenda kwa sababu anajua haguswi,” alisema Bisimba.

Wakili Fatma Karume alisema tatizo la Makonda ni kuamini anaweza kufanya mambo bila kufuata sheria na matokeo yake mengi yanashindwa kufanikiwa na kuiweka nchi njia panda.

“Pale ofisini kwake kuna wanasheria awe anaomba ushauri wa kisheria, nchi haiendeshwi kwa kukurupuka au matakwa ya mtu mmoja. Kabla ya hajafanya chochote aombe ushauri wa kisheria maana tumechoshwa na vilio vyake vya kanisani. Akiendelea kufanya mambo bila ushauri wa kisheria ataishia kulia kanisani,” alisema Fatma.

Alisisitiza kuwa mamlaka za uteuzi zinaweza kuendelea kumuacha Makonda kwenye nafasi hiyo hadi muda zitakapoona inatosha, ila ni muhimu kwa kiongozi huyo kuzingatia sheria kwa kila analofikiria kulifanya.

Februari 28, 2016 akiwa mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Makonda alitangaza habari njema kwa walimu wa mkoa wa Dar es Salaam kwamba wangepanda bure kwenye daladala ndani ya mkoa wake.

Kwa mujibu wa tangazo hilo huduma hiyo ilipaswa kuanza rasmi Machi 3, mwaka 2016 ikiwahusisha walimu wote wa shule za msingi na sekondari kwa kile alichodai kundi hilo muhimu linastahili fursa hiyo.

Kwa kiasi fulani mpango huo ulifanikiwa ingawa walimu wenyewe waliacha kuitumia fursa hiyo kutokana na changamoto wanazokutana nazo ndani ya madaladala ikiwemo kudhalilishwa na makondakta.

Februari 3, 2017 alitangaza majina 12 wakiwamo wasanii maarufu aliowataka kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kuhojiwa kuhusu mihadarati.

Februari 8, mkuu huyo wa mkoa alitangaza orodha nyingine ya watu 65 ambayo safari hii iliwajumuisha wafanyabiashara, viongozi wa dini na wanasiasa. Makonda alidai uamuzi wa kutaja majina ya watuhumiwa wa biashara na utumiaji wa dawa za kulevya hadharani ulitokana na maombi ya Watanzania wakati wa uongozi wa Serikali ya awamu ya nne.

Mtindo huo wa kutaja majina uliibua mjadala katika jamii wengi wakiupinga kabla ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuufunga kwa kupiga marufuku kutaja majina ya watuhumiwa hadharani.

Katika kampeni hii watu wachache walisota mahabusu na kufikishwa mahakamani akiwemo msanii Wema Sepetu, mwanamuziki TID na mfanyabiashara Yusuph Manji na tayari kesi zao zimekwisha ila hadi sasa haijulikani nini kinaendelea kwa wengine waliotajwa.

Aprili 9, aliibuka na kampeni ya kuwasaidia wanawake waliotelekezwa kwa kuwaruhusu kukusanyika ofisini kwake na kukutana na wanasheria. Kampeni hiyo ilidumu kwa siku saba ikilenga kuwabaini wanaume waliowatelekeza wanawake waliowazalisha.

Maelfu ya wanawake kutoka katika kila pembe ya jiji la Dar walifurika ofisini kwa Makonda wakiwania kupata msaada wa kisheria. Kwa amri ya ofisi yake barua ziliandikwa na walalamikiwa walianza kuitikia wito na kwenda kujieleza.

Wanaharakati walipiga kelele kuhusu mtindo uliotumika na hatimaye ndani ya Bunge Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakakosoa kampeni hiyo.

Kwa mujibu wa mawaziri hao, kampeni hiyo ilipaswa kufanywa kwa faragha na si kuanikwa hadharani. Makonda pia alipiga marufuku uvutaji wa shisha hadharani, akatangaza vita na watakaobainika kuendelea kutumia ulevi huo.

Akaenda mbele zaidi kwa kuwatuhumu aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Simon Sirro (sasa Mkuu wa Jeshi la Polisi) na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi Suzan Kaganda, kulegalega kusimamia suala hilo huku akihofia wanaweza kuwa wamehongwa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema wazi kuwa angemwajibisha Makonda iwapo hatasimamia ipasavyo kukomesha matumizi ya shisha. Opereheni zote hizo hakuna iliyoendelea baada ya muda mchache tangu itangazwe.