http://www.swahilihub.com/image/view/-/4334614/medRes/1908622/-/nc0hqfz/-/lucia.jpg

 

Wakulima washauriwa kutumia mifuko ya kisasa kuhifadhi nafaka

Jean Njiru

Bi Jean Njiru mkurugenzi mkuu wa Pics Afrika Mashariki mnamo Machi 14, 2018, aonesha nafaka iliyohifadhiwa kwenye mifuko ya kisasa mwaka 2014 na ingali salama. Picha/SAMMY WAWERU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Wednesday, March 14  2018 at  13:26

Kwa Muhtasari

Sekta ya kilimo ni nguzo muhimu nchini Kenya kwa sababu huhakikishia taifa usalama wa chakula.

 

SEKTA ya kilimo ni nguzo muhimu nchini Kenya kwa sababu huhakikishia taifa usalama wa chakula.

Katika awamu yake ya pili na ya mwisho, Rais Uhuru Kenyatta ameweka wazi kuwa lengo lake ni kuafikia ajenda kuu nne, miongoni mwazo ikiwa sekta ya kilimo.

Baada ya kuapishwa Novemba 28, 2017, Rais alisema atafanya kila awezalo kuangazia usalama wa chakula.

Kufuatia shabaha ya kiongozi huyo wa taifa, wakulima nchini wameshauriwa kukumbatia mfumo wa teknolojia ya kisasa kuhifadhi mazao ya nafaka kupitia mifuko inayofahamika kama 'Purdue Improved Crop Storage' (PICS).

Kwenye warsha iliyoandaliwa na wazinduzi wa Pics jijini Nairobi wakulima wamehimizwa kuzingatia usalama wa chakula kwa msingi wa wanavyokihifadhi.

Mkurugenzi mkuu wa Pics ukanda wa Afrika Mashariki Bi Jean Njiru, amesema kuna haja ya kila Mkenya kula chakula kilichohifadhi kwa hali nzuri na kuwa salama kwa afya ya binadamu.

"Mifuko ya Pics inaboresha thamani ya mazao, afya na uhakika wa chakula," amesema Bi Njiru mapema Jumatano katika warsha hiyo mtaani Upper Hill.

Mifuko hiyo ilizinduliwa miaka 20 iliyopita katika Chuo Kikuu cha Purdue Amerika, na kufanyiwa majaribio nchini Cameroon.

Bi Njiru ameeleza kwamba inatumika kuhifadhi nafaka kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu ambapo imeundwa kwa malighafi yasiyo na kemikali.

Kulingana na wataalamu kutoka nchi mbalimbali Afrika, hasa waliofanya majaribio ya mifuko hiyo ni kuwa pindi nafaka inapotiwa na kufungwa vizuri wadudu wanaoishambulia kama vile kipukusa (weevils) hawana uwezo kuitoboa.

Bi Bernadette Majebelle ambaye ni meneja wa Pics Tanzania, amefichua kuwa ilizinduliwa Afrika Mashariki mwaka 2014.

"Ilipoingia Tanzania tuliifanyia majaribio na miezi sita baadaye nafaka tuliyotia ilikuwa imara, vipukusa wanaotiwa na mahindi hufa mara moja kwa sababu ya kukosa hewa ya Oksijeni ifungwapo," akaeleza Swahilihub, akionesha nafaka iliyohifadhiwa 2014 na ingali katika hali nzuri ilivyokuwa.

Bi Majebelle amefichua kuwa kufikia 2017, walikuwa wameweza kufikia wakulima 800,000 Tanzania waliokiri nafaka yao iko salama ikihifadhiwa kwa Pics.

Wakulima wa nafaka kwa miaka mingi wamekuwa wakipitia changamoto za mazao yao kuharibika, kushambuliwa na vipukusa na hata kuoza.

Ubora

Bi Lunah Njeri kutoka kampuni ya Bell inayounda mifuko hiyo nchini Kenya, amesema kuwa ladha, rangi na madini ya nafaka inahifadhiwa pasi kuhitilafiwa.

"Tunalenga kila familia iwe na mifuko miwili nchini ili chakula chao kiwe salama," amesema Bi Njeri.

Nchini Kenya wakulima wanaopanda nafaka huvuna karibu magunia milioni 14 ya mahindi kila mwaka. Kaunti ya Trans Nzoia na Uasin-Gishu ndio inaongoza katika zaraa ya nafaka hasa mahindi, ngano na maharage.

Bi Njeri amesema uhamasisho wa wakulima kutumia mifuko hiyo salama umeweza kufikia asilimia 80, huku asilimia 10 ikiona umuhimu wa kukumbatia matumizi yake.

"Wakulima wengi wako mashambani, kuwafikia ndio changamoto kuu. Wengine wanadhani Pics imeundwa kwa dawa lakini la," akafafanua.

Nchini Nigeria, mifuko hiyo ilizinduliwa 2008 na kulingana na maneja wa kampuni ya Lela Agro Bw Ahmed Adam Kaumi ni kuwa kufikia sasa wameweza kuhamasisha zaidi ya wakulima 800,000.

"Mwaka huu, 2018 tunapania kufikia wafanyabiashara wa nafaka na wakulima milioni 2," akaeleza.

"Tunaomba vyombo vya habari na serikali watusaidie kufikia wafanyabiashara wa nafaka na wakulima, ili chakula tunachokula kiwe salama," akaongeza.

Uundaji wa Pics unafadhiliwa na wakfu wa Gates kwa ushirikiano na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Aidha, hapa nchini mfuko mmoja wa Pics wa kilo 100 unauzwa kwa Sh250.

"Kuna hata mifuko ya kilo 50 na 25, na bei yake," akaeleza Bi Jean Njiru mkurugenzi mkuu wa Pics Afrika Mashariki, ambaye pia ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Purdue Marekani.

Mataifa 16 Barani Afrika yaliyokumbatia mfumo wa teknolojia hiyo mpya ya kuhifadhi nafaka, yamehudhuria warsha hiyo ikiwamo Kenya, Cameroon, Uganda, Burkina Faso, Niger, Senegal, Nigeria na Mali.