http://www.swahilihub.com/image/view/-/3406064/medRes/1168738/-/3t9je1/-/MagufuliRais.jpg

 

Wakuu wa wilaya msikilizeni Rais

Rais John Magufuli akitoa hotuba

Rais John Magufuli akihutubu awali. Picha/AFP 

Na MHARIRI – MWANANCHI

Imepakiwa - Wednesday, January 30  2019 at  09:28

Kwa Muhtasari

Rais John Magufuli amewaapisha majaji sita wa Mahakama ya Rufaa na 15 wa Mahakama Kuu katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wakuu wa wilaya wawili pamoja na wakurugenzi watendaji wa wilaya 10 ambao pamoja na majaji hao, wote waliteuliwa Jumapili iliyopita kushika nyadhifa zao.

 

JUMANNE, Rais John Magufuli aliwaapisha majaji sita wa Mahakama ya Rufani na 15 wa Mahakama Kuu katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Sherehe hizo pia zilihudhuriwa na wakuu wa wilaya wawili pamoja na wakurugenzi watendaji wa wilaya 10 ambao pamoja na majaji hao, wote waliteuliwa Jumapili iliyopita kushika nyadhifa zao.

Rais baada ya viapo vya majaji hao alizungumzia masuala mbalimbali juu ya umuhimu wa mhimili huo wa sheria kutenda haki na kutumiza wajibu wake kwa kufuata misingi iliyowekwa. Pia, alizungumzia kukithiri kwa matukio ya wakuu wa wilaya kuwaweka ndani watu, wakati mwingine bila ya kuwafikisha mahakamani au kwa masuala ambayo yangeweza kumalizwa kwa maagizo.

Sheria ya Tawala za Mikoa ya 1997 inawapa wakuu wa wilaya na mikoa mamlaka ya kumweka ndani mtu au kundi la watu kwa muda usiozidi saa 24 au 48 ambao kubaki kwao nje kunaweza kusababisha madhara katika jamii.

Lakini, baadhi ya wakuu wa wilaya wamekuwa wakiitumia vibaya sheria hiyo kuwaweka watu ndani kila walipojisikia kufanya hivyo na mtindo huo umeendelea kushika kasi licha ya viongozi waaandamizi akiwamo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kukemea na kuonya tabia hiyo.

Mawaziri Selemani Jafo (Tamisemi), Ummy Mwalimu (Afya) na George Mkuchika (Utumishi na Utawala Bora) wameshaeleza namna wakuu hao wa wilaya wanavyopaswa kuzingatia misingi ya utawala bora na kuacha kuweka ovyo watu mahabusu.

Akizungumza katika mkutano wa mafunzo kwa wakuu wa mikoa na makatibu tawala ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi huko Dodoma, Waziri Mkuchika alisema imekuwa ni kawaida hivi sasa kwa baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa kuwaweka ndani watumishi wa umma hata kwa mambo ya kawaida kama kuchelewa kufika katika vikao vya kazi.

Pamoja na maelekezo ya viongozi hao na wadau wengine wakiwamo wananchi, bado tumeendelea kushuhudia matumizi ya nguvu kwa kisingizio cha sheria hiyo yakiwaweka watu wa kada mbalimbali mahabusu.

Wapo wenyeviti wa vyama vya siasa, wakurugenzi wa wilaya, katibu tawala wa wilaya, wawekezaji na wananchi wengine walioonja adha hii kwa makosa ambayo kama alivyoeleza Rais Magufuli, yangeweza kumalizwa kwa mashauriano tu.

Mkoa wa Kilimanjaro ndio uliotia fora kwa baadhi ya wakuu wake wa wilaya kutumia sheria hiyo utadhani walikuwa wanashindana. Hii ni hatari kubwa kwa mustakabali wa Taifa letu lililojengwa na waasisi katika misingi ya kusikilizana, kushauriana na kuambizana ukweli badala ya matumizi ya mabavu katika utendaji.

Katika kile kilichoonekana kwamba sheria hiyo imekuwa ikitumika kama adhabu badala ya malengo yaliyokusudiwa, zinapoisha saa 24 au 48 ni nadra kuona hatua nyingine zinazochukuliwa.

Tunaamini kwamba baada ya kauli hii ya Rais, wakuu wa wilaya na mikoa sasa watabadilika kufanya kazi zao kwa weledi zaidi badala ya kuumiza wananchi wa kawaida, wawekezaji na wasaidizi wao kwa kisingizio cha matumizi ya sheria hiyo.

Tunasisitiza hilo tukiamini kwamba kauli ya Rais wa nchi ni amri. Hivyo kuanzia sasa hatutasikia matukio ya ajabuajabu ya kuwakamata na kuweka watu ndani pasi na kufuata misingi ya haki na sheria.

Sheria hiyo itumike pale kunapokuwa na uvunjifu wa amani au kunapokuwa na tishio la usalama tofauti na sasa ambapo baadhi ya wakuu wa wilaya wamekuwa wakiitumia kwa ajili ya vitisho, visasi na ubabe tu.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647