Waliorejeshwa serikalini sasa wachape kazi

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Wednesday, April 11  2018 at  08:47

Kwa Muhtasari

Kwamba Serikali imewarejesha kazini watumishi 1,370 ambao walikuwa wameondolewa kwenye mfumo wa malipo ya mshahara kwa kukosa sifa ya cheti cha kufaulu mtihani wa elimu ya kidato cha nne, ni habari njema, ya faraja na matumaini makubwa si kwa watumishi tu, bali familia zao, ndugu, jamaa, watumishi wenzao na marafiki.

 

KWAMBA Serikali imewarejesha kazini watumishi 1,370 ambao walikuwa wameondolewa kwenye mfumo wa malipo ya mshahara kwa kukosa sifa ya cheti cha kufaulu mtihani wa elimu ya kidato cha nne, ni habari njema, ya faraja na matumaini makubwa si kwa watumishi tu, bali familia zao, ndugu, jamaa, watumishi wenzao na marafiki.

Tuna uhakika, baada ya kauli ya Serikali kuwarejesha kazini watumishi hao iliyotolewa bungeni juzi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), George Mkuchika, maelfu ya wananchi wakiongozwa na wale waliokuwa wakiguswa moja kwa moja na uamuzi wa awali wa kuwaondoa, walishangilia.

Kushangilia huko kuna sura nyingi; kwanza kwa wale waliokuwa wameondolewa, wamefarijika kwamba Serikali imesikia kilio chao na sio tu kuwarejesha kazini, bali kuwalipa haki zao zote walizokosa tangu wameondolewa.

Waziri Mkuchika alisema watumishi waliolegezewa masharti ya sifa za muundo kupitia barua ya katibu mkuu wa Utumishi Juni 30,2011, warejeshwe kazini mara moja, walipwe mishahara yao kwa kipindi chote ambacho walikuwa wameondolewa kazini na waendelee na ajira zao hadi watakapostaafu kwa mujibu wa sheria.

Baadhi yao, kama si wengi walishayumba kimaisha na walikuwa wakisononeka kila uchwao hasa wakikumbuka jinsi walivyolitumikia Taifa hili kwa moyo wao wote na kwa kadri ya uwezo na elimu yao. Hivyo kurejeshwa kazini kumewapa nuru mpya ya maisha, wao na familia zao.

Hata watu wa karibu wa baadhi ya watumishi hao watakuwa wamefarijika kwa kuwa kama tunavyojua maisha yetu ni ya kubebana na kusaidiana tunapokuwa na matatizo, hivyo ni dhahiri kwamba baadhi yao walishakuwa tegemezi hivyo kurejea kazini ni faraja ya kupunguza mzigo huo.

Tunapowapongeza watumishi hao kwa uvumilivu mkubwa waliouonesha katika kipindi chote walichokuwa nje ya ajira. Subira yao ndio imedhihirisha kwamba walikuwa waadilifu na ndiyo maana hawakukumbwa na kashfa ya kughushi vyeti vya kidato cha nne kama wengine walivyofanya na hivyo kutokuwepo katika msala huo.

Kwa kauli ya Waziri Mkuchika, uamuzi huo wa kuwarejesha kazini watumishi hao, hautawahusu wale waliowasilisha vyeti vya kughushi katika kumbukumbu za ajira zao; na waliokuwepo kazini kabala ya Mei 20,2004 lakini katika kumbukumbu zao walijaza taarifa za uongo kuwa ni kidato cha nne.

Wengine ambao waziri huyo alisema hawatarudishwa kazini ni walioajiriwa baada ya Mei 20,2004 na ambao hawakuwa na sifa za kufaulu mtihani wa kidato cha nne kwa kuwa walijipatia ajira kinyume cha maelekezo ya Serikali.

Wakati tukiipongeza Serikali kwa hatua hii ya kusikiliza kilio cha wanyonge, ni imani yetu kwamba watumishi hawa watarejea kazini na kutimiza wajibu wao kwa moyo mmoja na kusahau magumu waliyopitia.

Lakini pia tunaamini kwamba tukio hilo lina mafunzo makubwa kwa watumishi wote nchini na sio wa umma pekee, nalo ni kuwa waadilifu muda wote na kuachana na mambo ya kutafuta njia za mkato kutatua shida zinazowakabili. Pia ni somo kwa Serikali kuwa kunahitajika umakini na ushirikishwaji wananchi katika kufanya maamuzi makubwa.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647