Wanasiasa waepuka kujadili athari hasi za miraa

Wakulima wa miraa katika soko la Laare

Wakulima wa miraa katika soko la Laare mnamo Machi 18, 2017. Picha/KENNEDY KIMANTHI 

Na AGNES ABOO

Imepakiwa - Sunday, March 19  2017 at  17:31

Kwa Mukhtasari

Wanasiasa katika Kaunti ya Meru wameepuka mjadala kuhusu athari hasi za miraa wakihofia kukosa kupigiwa kura na wakazi waokuza mmea huo.

 

WANASIASA katika Kaunti ya Meru wameepuka mjadala kuhusu athari hasi za miraa wakihofia kukosa kupigiwa kura na wakazi waokuza mmea huo.

Katika eneo la Nyambene ambapo miraa hupandwa kwa wingi wanasiasa wameogopa kujadili hadharani madhara yanayotokana na matumizi ya mmea huo licha ya madhara hayo kuongeza kila siku.

Ingawa wagombea wengi wanakiri kuwa eneo hilo linakabiliwa na changamoto si haba wamekosa kujitokeza wazi kuzungumza swala hilo.

Uchunguzi wa Swahilihub ulibaini kwamba ukuzaji miraa umesababisha ukiukaji wa haki za kijamii kama vile; ajira kwa watoto wadogo, migogoro ya kifamilia, mimba za mapema kwa wasichana wadogo na watoto kuacha shule maswala ambayo wanasiasa wamehepa kuyaguzia.

Malipo ambayo watoto wadogo katika eneo hilo wanalipwa kwa siku baada ya kuchuna miraa ni sawa na yale ambayo mfanyikazi wa wastani (an average adult) nchini anapata kwa siku tatu hali ambayo imewalazimu wengi wao kuacha shule na kujitosa katika biashara hiyo.

Watoto kati ya miaka 12 hadi miaka 17 wanapata pesa nyingi kila siku lakini kibunda kikubwa kinaiishia kwa ununuzi wa pombe na dawa za kulevya.

Dkt Rufus Miriti mmoja wa wagombea wa ubunge katika eneo la Igembe kusini anasema kuwa ajira kwa watoto ni tatizo kubwa akikiri kwamba viongozi wameshindwa kukabiliana na tatizo hilo.

"Watoto wadogo wamejitosa katika biashara ya miraa kutokana na umaskini. Watu wengi hawajui haki zao hii amewapa wanasiasa msingi wa kutumia wakulima wa miraa badala ya kutatua matatizo yao,” aliiambia Swahilihub.

Anaongeza kuwa marufuku ya miraa nchini Uingereza Juni 24, 2014 ilibadilisha umbo la siasa katika eneo hilo.

Wanasiasa hujaribu kuwarai wapiga kura jinsi watakavyotafuta soko ya mmea huo ikiwa watapewa nafasi lakini wameshindwa kutafuta suluhu ya matatizo yanayowakabili wakulima.

Mkazi Simon Kobia alisema kuwa licha ya kuwa na fedha nyingi katika eneo hilo kutokana na biashara ya miraa, watu wengi hawana elimu.

Aliongeza kuwa eneo hilo lina wapiga kura wengi ktika Kaunti ya Meru ikilinganishwa na maeneo mengine hatua inayo walazimisha wanasiasa kutumia miraa kutafuta kura ambayo ni mada rahisi ya kuuza kisiasa katika eneo hilo.

"Viongozi hao haiwezi kutatua masuala yanayozunguka mmea lakini baada ya kugundua zinagusa maisha ya wapiga kura ndani ya vijiji wanaitumia wakiahidi kutatua masuala ambayo kwa akili zao wanajua hawawezi," alisema.

Naibu Gavana wa Meru, Raphael Muriungi ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Igembe Kusini kwa miaka 15 kabla ya kujiunga na serikali ya Kaunti alisema kuwa miraa imekuwa chombo cha kutafuta kura kwa wanasiasa lakini wakulima bado wanakabiliwa na matatizo yale yale.

"Wakati mswada ulipitishwa kuwa sheria katika bunge la kitaifa wanasiasa hao walirudi wakijichocha jinsi wamesaidia wakulima licha ya kuchaguliwa kuwakilisha maslahi ya raia wa kawaida," alisema.

Mbinu za kidiplomasia

Aliongeza kuwa licha ya viongozi wa eneo lililoathirika kujaribu kugeuza biashara hiyo kwa mwelekeo wa kisiasa, suala zima linahitaji mbinu za kidiplomasia.

Alisema kuwa ukosefu wa haki za kijamii zimeongezeka kwa sababu ya mila na desturi ambayo hata viongozi wameshindwa kudhibiti.

"Tumejaribu kushinikiza mwisho wa ‘PangaJustice’ katika eneo hilo lakini utamaduni huo inachukua muda mrefu kuisha," aliongeza.

Naibu gavana ambaye anawania kiti cha eneo bunge la Igembe Kusini anasema kuwa wanasiasa wamegundua kuwa miraa ni doa laini la kisiasa wanayotumia kukusanya kura.

Hatua anayosema imelazimisha wanasiasa kueneza propaganda kuhusu miraa kwa sababu matatizo mengi yaweza tu kutatuliwa katika ngazi ya kitaifa.

Pia alikosoa serikali kwa kushindwa kuzingatia wakulima wa miraa wakati wa kijadili masuala yam mea huo lakini kutumia ‘technocrats’ kutatua matatizo hayo ambayo hawayajui.