http://www.swahilihub.com/image/view/-/4880516/medRes/2188373/-/ydpk62/-/ikoko.jpg

 

Watendaji serikalini wasiwakwamishe wawekezaji

Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. Picha/MAKTABA 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Thursday, December 6  2018 at  08:38

Kwa Muhtasari

Mazingira ya urasimu mwingi hukwamisha juhudi za Serikali za kukaribisha wawekezaji nchini Tanzania.

 

ZIARA ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) juzi, ilikutana na mazingira ya urasimu yanayokwamisha juhudi za Serikali za kukaribisha wawekezaji nchini.

Majaliwa alikitembelea kituo hicho ikiwa ni mara ya kwanza tangu kihamishiwe chini ya ofisi yake kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Akiwa kwenye kituo hicho alipata taarifa za kusimama kwa mfumo wa utoaji vibali vya kazi kwa kile kilichodaiwa kuwa Kamishna wa Kazi, Gabriel Malata bado anajifunza kuhusu mfumo huo.

Maelezo hayo yalimkasirisha Majaliwa ambaye alitoa tamko la kuwataka watendaji wa Serikali kuondoa mazingira ya urasimu yanayosababisha kukwama kwa shughuli za uwekezaji.

Tunaunga mkono tamko la Majaliwa kwa sababu siku moja kabla ya ziara yake kwenye kituo hicho, Balozi wa China nchini, Wang Ke alitoa malalamiko kwa Serikali kuhusu ucheleweshaji wa vibali vya kuishi nchini.

Balozi huyo alitoa malalamiko hayo kwenye mkutano uliowakutanisha wajumbe wa Baraza la Uhamasishaji Wawekezaji kutoka China na viongozi wa Serikali ya Tanzania.

Alichokishuhudia Majaliwa kwenye ziara yake TIC na kilicholalamikiwa na Balozi Ke ni kielelezo kwamba bado kuna watumishi wa Serikali ambao ni wagumu kubadilika.

Serikali ya Awamu ya Tano imetimiza umri wa miaka mitatu na Watanzania wengi wanafahamu azma ya uongozi wa sasa ni kuendeleza uchumi wa viwanda kwa kutumia wawekezaji wa ndani na nje.

Hoja kwamba mtoa vibali ameacha kutimiza wajibu wake kwa kuwa yuko darasani anajifunza namna ya kutoa vibali, huko ni kukwamisha jitihada za Rais John Magufuli za kukaribisha wawekezaji.

Pia, TIC inapaswa kufahamu kuwa juhudi za kutafuta wawekezaji wa kigeni sio jambo rahisi, mabalozi wetu huko nje kazi kubwa wanayofanya ni kuhakikisha wanaleta wawekezaji kutimiza lengo la diplomasia ya kiuchumi. Haiwezekani juhudi zote hizi zikwamishwe na mtu mmoja kwa madai kuwa bado anajifunza namna ya kutoa vibali. Huu ni mzaha usiostahili kuvumiliwa.

Tunaamini yapo mambo hayaendi ipasavyo ndani ya TIC na ndio maana hivi karibuni Rais Magufuli alitangaza uamuzi mgumu wa kukiondoa kituo hicho Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na kukiweka chini ya ofisi ya Waziri Mkuu.

Ifahamike kwamba wawekezaji wa kigeni tunaowakaribisha nchini pia wanakaribishwa na nchi zingine. Mfano, Rwanda imerahisisha mazingira ya uwekezaji kiasi cha kuweza kutoa vibali kwa wawekezaji ndani ya saa 24.

Ni vyema watendaji ndani ya Serikali wakafahamu kwamba zama zimebadilika na mazingira ya utendaji nayo yamebadilika kuanzia teknolojia hadi mtazamo katika kushughulikia jambo lolote.

Kusimamisha kutoa vibali kwa maelezo tuliyoyasikia kutafukuza wawekezaji na tayari Balozi Ke wa China amelalamikia hilo. Wawekezaji wanapokuja nchini tunanufaika wananchi wote. Wapo wanaopata ajira, wakulima huuza mazao, kuongezeka mzunguko wa fedha na hata kijamii kuna wanaonufaika kwa kupata wachumba.

Rai yetu kwa watendaji wa Serikali wakubali ni kubadilika kwa kuondokana na urasimu usiokuwa na maana. Tujenge Taifa letu kwa manufaa yetu sote. Mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe na si vinginevyo.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam, Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647