http://www.swahilihub.com/image/view/-/4533542/medRes/1955242/-/ysnh24/-/magufulia.jpg

 

Watendaji wanajisahau vipi mpaka Rais awasaidie?

John Pombe Magufuli

Rais John Pombe Magufuli apungia umma Desemba 9, 2017, Dodoma katika sherehe za maadhimisho ya miaka 56 tangu Tanzania ipate uhuru. Picha/AFP 

Na MHARIRI – MWANANCHI

Imepakiwa - Monday, September 10  2018 at  08:39

Kwa Muhtasari

Kila anakokwenda Rais John Magufuli amekuwa akipata malalamiko ambayo kiuhalisia ama yalipaswa kutatuliwa na wasaidizi wake au hayakupaswa kabisa kuwapo kutokana na uwepo wa watendaji katika maeneo hayo.

 

RAIS John Magufuli anaendelea na ziara yake katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa na tayari ametembelea Mwanza, Mara na Simiyu ambako amezindua na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mbali ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo, lakini kuna jambo moja ambalo limeendelea kujitokeza katika ziara hiyo ya mkuu wa nchi, nalo ni malalamiko ya wananchi kuhusu mambo mbalimbali wanayoona hayatekelezwi ipasavyo.

Kila anakokwenda amekuwa akipata malalamiko ambayo kiuhalisia ama yalipaswa kutatuliwa na wasaidizi wake au hayakupaswa kabisa kuwapo kutokana na uwepo wa watendaji katika maeneo hayo.

Mathalan, akiwa Mwanza mjini alilazimika kuwaagiza mawaziri wa Wizara ya Ujenzi na ile ya Fedha kukaa pamoja kutatua kilio cha kodi katika vifaa vya ujenzi, suala ambalo limekuwa likiathiri miradi ya maendeleo ambapo vifaa hivyo vinatozwa kodi kubwa na kukwamisha ukamilishaji wake.

Ni vifaa hivyo pia ambavyo kwa upande wa wananchi imebakia kuwa kilio cha muda mrefu, lakini hakuna hatua zinazofanyika kuhakikisha vinashuka bei na hivyo kuwafanya washindwe kujijengea makazi bora.

Akiwa mjini Bunda katika siku yake ya kwanza ya ziara mkoani Mara, Rais Magufuli aliwabana viongozi wa mkoa huo baada ya kuelezwa kuwa mradi wa maji Bunda haujakamilika tangu ulipoanzishwa miaka minane iliyopita.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Simon Mayaya alimwomba Rais kuingilia kati tatizo hilo ombi ambalo aliliridhia na kuahidi kumtuma waziri wa maji na katibu mkuu wa wizara hiyo. Rais aliagiza hatua zichukuliwe kama ambavyo pia aliagiza zichukuliwe dhidi ya mkandarasi wa aina hiyo mjini Musoma, baada ya kuelezwa na wananchi kuwapo kwa tatizo.

Ni hapohapo Musoma pia alipokea kilio cha wananchi juu ya mmiliki wa hoteli moja iliyopo ufukweni mwa Ziwa Victoria anayewazuia kufika eneo hilo licha ya kwamba ndipo wanapopata huduma ya maji.

Kutokana na kadhia hiyo aliagiza ikiwezekana mmiliki huyo apokonywe hata hoteli hiyo kwani licha ya matatizo yaliyopo pia hajaiendeleza kwa muda mrefu baada ya kubinafsishiwa na Serikali miaka mingi.

Si hayo tu, lakini pia katika ziara hiyo amepokea malalamiko kadhaa juu ya ardhi, maji, nishati, miundombinu na hata huduma za jamii. Yote haya yalipaswa kumalizwa na watendaji walio chini yake.

Juzi akihutubiwa wananchi mjini Tarime, Rais aliwataka watendaji wa Serikali kushughulikia matatizo ya wananchi kwa wakati ili kudumisha amani hasa eneo hilo ambalo lina historia ya migogoro.

Rais aliwataka viongozi wa Serikali kuacha kufanya kazi kwa kutaka sifa, badala yake wawe na mikakati endelevu itakayowawezesha kuwahudumia wananchi.

Wakati tukimpongeza Rais Magufuli kwa kushughulikia kero ambazo hakupaswa kukutana nazo kwa kuwa ana wasaidizi wengi, swali letu linabaki juu ya hao wasaidizi wake iwapo kweli wanamsaidia ipasavyo.

Tunasema hivyo kwa sababu haiwezekani wananchi walilie maji miaka mingi, mkandarasi alipwe lakini asimalize kazi ili wapate huduma hiyo huku watendaji wanaopaswa kumbana wapo. Hata hili la wananchi kuzuiwa kufika ufukweni mwa bahari na mtu haliingii akilini kama watendaji wapo ambao walipaswa kuwa wamelitatua siku nyingi. Tunachokiona ni kuwapo kwa tatizo mahali fulani katika utekelezaji wa majukumu yao na ni hilo linatushawishi kuhoji zaidi kulikoni.

Ni vyema watendaji wajitume kufanya kazi ipasavyo ili kumsaidia Rais kwa kuwa amewaamini na kuwapatia majukumu hayo. Kamwe hatukubaliani na utendaji wa mazoea ambao unasababisha vilio vya muda mrefu kubaki vilivyo.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647