http://www.swahilihub.com/image/view/-/2825996/medRes/1085533/-/rhyhap/-/DNChurchConflict0908.jpg

 

Watumishi wa Mungu waimarishe amani, sio migogoro

Polisi wakiwa katika kanisa la African Israel Nineveh

Polisi wakiwa katika kanisa la African Israel Nineveh baada ya vurugu kutokea Agosti 9, 2015. Picha/TONNY OMONDI 

Na TAHARIRI YA MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, February 6  2018 at  09:32

Kwa Muhtasari

Kwa miaka mingi kwenye nyumba za ibada ni mahali ambako waumini wanakwenda kuwa karibu zaidi na Mungu wao kusemezana naye, kutubu, kuabudu, kusifu na kuomba uponyaji, amani na faraja.

 

KWA miaka mingi kwenye nyumba za ibada ni mahali ambako waumini wanakwenda kuwa karibu zaidi na Mungu wao kusemezana naye, kutubu, kuabudu, kusifu na kuomba uponyaji, amani na faraja.

Matajiri, maskini, wake kwa waume, wenye shida za magonjwa mifarakano katika familia, ndoa na kero kazini hukimbilia kwenye nyumba za ibada kwa ajili ya kuomba faraja, utulivu wa mioyo, kuponya majeraha na kutubu  dhambi.

Viongozi wa siasa, Serikali au wa mashirika ya umma wanapojiona wamekwenda kinyume na utaratib na miongozo ya kazi hukimbilia nyumba za ibada kutubu wasiwe wajeuri   wala kiburi bali wawaheshimu walio chini yao.

Kwenye nyumba za ibada siyo mahali pa kuonyesha umwamba, umaarufu, kuzua mitafarakano na ugomvi wala kunyesha misimamo mikali. Ni mahali pa amani.

Hivi mtumishi wa Mungu anawezaje kuongoza nyumba ya ibada ambako kwa miezi, mwaka na hata miaka kadhaa waumini wake hawakai pamoja wala kungea lugha moja kuhusu masuala ya kiroho na kimwili?

Mtumishi wa Mungu anajisikiaje anapoongoza watu waliogawanyika katika makundi eti huyu wa huku na yule wa kule au huyu ni wa itikadi hii na yule ni wa itikadi ile?

Ndiyo maana tumefurahishwa na namna Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Mashariki Dk Lucas Mbedule alivyowaomba msamaha washirika wa Kanisa Kuu la Mtwara kwa nyenyekevu ili wasiliumize kanisa.

Huku akiwa amelala kifudifudi, askofu huyo katika ibada ya Jumapili aliwataka washirika wake kumaliza tofauti zao zilizodumu kwa miaka miwili na kukutana katika ibada wakiwa na mioyo minyenyekevu kumwomba Mungu.

Vilevile tumefurahishwa na tukio katika Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam ambalo Jumapili lilihitimisha mgogogoro wa miaka mingi kwa kumsimika Askofu Jackson Sosthenes.

Katika hafla ya kusimikwa kwa Askofu Sosthenes iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Albino, Rais Magufuli alipata fursa ya kumpa ushauri Askofu huyo mpya akimtaka awe kiongozi wa makundi yote na kuepuka kulipa kisasi.

Baada ya migawanyiko ya miaka mingi na kufikia kuandikwa sana kwenye vyombo vya habari, kanisa liliona njia pekee ni kubadili uongozi ili kiongozi mpya aweze kuyaweka makundi yote pamoja bila shaka akiwafundisha kusameheana.

Kusamehe ni jambo gumu lakini kwa kuwa mafundisho ya dini yanasisitiza mafundisho ya dini anafundisha kusameheana, kwa vyovyote askofu atabeba ujumbe huo ili kuliponya kanisa, jamii na taifa kwa jumla.

Watu wasiosameheana au jamii isiyoomba misamaha huweka kinyongo na kukaribisha migogoro.

Nyumba za ibada zinatakiwa kufanya kazi ya kuombea watu, kusuluhisha migogoro yao kwa amani na sio kuliita Jeshi la Polisi kuzima vurugu, fujo na machafuko ambayo huenda ni kwa sababu waumini hawataki kusameheana.

Tunawasihi viongozi wa dini zote kujikita katika maandiko ya vitabu vyao kuhubiri amani, kufundisha upendo, kujenga mazingira ya nyumba ya ibada kuwa kimbilio la wenye shida kuwaombea watu msamaha na kufundisha watu namna ya kuombana msamaha.

Tunahitimisha kwamba amani ni kitu cha thamani kubwa katika kanisa, familia, nchi na jamii isiyo na amani hukosa fursa ya kufanya ibada.

Haijui namna ya kuomba, ndoa zao huwa na mifarakano na nyumba za ibada hujaa vurugu ambayo isiposuluhishwa mapema hugeuka kuwa mgogoro wa kisiasa.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647