wazazi,walezi wasiwe chanzo watoto mitaani

Imepakiwa - Wednesday, May 15  2019 at  11:59

 

Kumekuwa na ongezeko lisilokuwa na udhibiti la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani hasa kwenye miji mikubwa hapa nchini.

Jiji la Mwanza mwaka 2017 lilikuwa na watoto wanaoishi katika mazingira magumu 800 idadi iliyoongezeka hadi kufikia 1,254 kwa mwaka 2018.

Mwanzoni mwa mwaka 2018, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alikiri kuwapo ongezeko la watoto hao hasa katika miji mikubwa huku akitaja takwimu za ongezeko hilo.

Mwalimu aliyekuwa anajibu swali la Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji alitaka kujua hatua ambazo zinachukuliwa na Serikali juu ya ongezeko hilo, alisema Serikali ina jukumu la kuhakikisha ulinzi na usalama wa watoto hao unapatikana pamoja na kushirikisha jamii kuwaokoa.

Alisema kwa utafiti uliofanyika 2012 ulibainisha kuwapo watoto 56,000 katika majiji ya Dar es salaam na Mwanza wanaotoka katika mikoa kumi ambayo ni Dar es Salaam yenyewe asilimia 28, Dodoma asilimia nane na Mwanza asilimia saba.

Mikoa mingine ni Morogoro asilimia saba, Tanga asilimia sita, Iringa asilimia tano, Pwani asilimia tano, Kilimanjaro asilimia tano na Arusha asilimia nne.

Kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la kutetea na kusaidia watoto wa mitaani la Railway Children Africa, ongezeko hilo linachangiwa na ukatili kwenye familia, ugomvi wa wazazi, watoto kutelekezwa na wazazi au walezi, umasikini, vifo vya wazazi, ushawishi wa makundi rika, matatizo ya kinidhamu kwa watoto na sababu nyingine za kimila.

Sababu inayoonekana kuchangia watoto wengi kukimbilia mitaani ni ukatili katika familia zao.

Wakitoa ushuhuda wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya watoto wa mitaani yaliyoandaliwa na Railway Children Africa na wadau wengine, watoto hao walisema wameondoka nyumbani kwa sababu ya kuteswa na wengine kufukuzwa.

Ilionekana licha ya umasikini na ushawishi wa makundi mabaya kwa watoto kuchangia kuingia kwa mitaani, wazazi ndio sababu kubwa zaidi inayowapeleka wengi wao mitaani.

Kutengana kwa wazazi kunasababishia watoto kwenda mitaani kwa kuwa usimamizi unakuwa hafifu hasa pale wanapobaki na baba pake yao.

Baba akiamua kuoa mwanamke mwingine, watoto hujikuta wanaenda mitaani kutafuta amani, furaha na upendo, mwishowe hujikuta wanakuwa wezi au kujiingiza kwenye biashara haramu za dawa za kulevya ili wapate chakula.

Meneja mradi wa Shirika la Railway Children Africa, Abdallah Issa alisema watoto wa mitaani wanakabiliwa na changamoto nzito sana mitaani.

Changamoto hizo ni pamoja na kuingiliwa kinyume na maumbile, watoto wa kike kuingiliwa kimwili, kutumikishwa kingono au kazi nyingine ngumu na kufanyishwa biashara zikiwamo haramu.

Issa anasema watoto hao wa mitaani wanakabiliwa na changamoto nyingine ya kupelekwa magerezani pale wanapofanya makosa, kitu kinachozidi kuwafanya wawe na maadili mabovu zaidi.

Anaitaka Serikali ijenge nyumba za mafunzo watakakokuwa wanapelekwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili kurekebisha makosa yao.

Jamii imekuwa ikiwatuhumu watoto hao na kuwapa majina ya kuwadhalilisha kama watoto wa mbwa, chokoraa na mengine mengi, lakini ukweli ni kwamba wazazi na walezi ndio vyanzo vikubwa kwa watoto hao kuwa mitaani.

Watoto hao wanapoingia mitaani wanakutana na watoto wenzao ambao wana tabia tofauti ikiwamo ya udokozi hivyo kutokana na njaa wanamua kuiba ili washibe na hatimaye kuwa wezi japo wengine hujiepushe na wizi kwa kufanya shughuli kama kuokota chupa na kuziuza. Wengine wanajiingiza kwenye ukahaba, uuzaji dawa za kulevya na hata kuingia kwenye matumizi ya dawa hizo.

Ifikie hatua jamii ione mtoto wa mwingine kama mtoto wake, wazazi wajitahidi kuwa kitu kimoja katika kulea watoto kwa maadili mema.

Watoto wasipewe adhabu kali kupitiliza pale wanapofanya makosa kama vile kupigwa na vyuma, kuchomwa moto na kufungiwa nje ya nyumba nyakati za usiku kwani kunapelekea woga kwa watoto na kulazimika kuishi mitaani.

Jamii iache ukatili kwa watoto hasa wa mitaani kwa kuwapa majina ya ovyo, lakini pia ijue watoto wa mitaani si tatizo la Serikali pekee, bali kila mzazi atekeleze majukumu yake kwa mtoto.

Pia ijulikane kuwa suala la watoto wa mitaani ni tatizo la jamii nzima kwa hiyo mwanajamii akikutana na mtoto wa mtaani ana tatizo lolote na anahitaji huduma fulani amsaidie kumwelekeza anapoweza kupata huduma; iwe polisi, ustawi wa jamii au kwenye mashirika yanayohusika na watoto hao.

0768920097