http://www.swahilihub.com/image/view/-/4303072/medRes/1883889/-/ngmmohz/-/pica.jpg

 

Wiki ya kimataifa kwa Vijana

Stephene Mbithe

Stephene Mbithe alianza kazi ya sanaa akiwa shuleni; kwa sasa mapenzi yake katika sanaa ndiyo kitega uchumi chake. Picha/ SAMMY WAWERU  

Na SAMMY WAWERU na MASHIRIKA

Imepakiwa - Wednesday, August 8  2018 at  10:54

Kwa Muhtasari

Kati ya Agosti 6 hadi Agosti 12 kila mwaka, huwa wiki ya kuadhimisha Vijana kimataifa.

 

NAIROBI, Kenya

KATI ya Agosti 6 hadi Agosti 12 kila mwaka, huwa wiki ya kuadhimisha Vijana kimataifa.

Wiki hii hasa huwa nafasi kwa serikali na washikadau husika duniani kuangazia maswala yanayozingira vijana. Kilele chake huwa Agosti 12 inayofahamika kama International Youth Day (IYD) kwa Kiingereza, ambapo hukongamana kueleza kwa pamoja maswala hayo.

IYD isikukanganye na Siku ya Vijana Duniani (World Youths Day), kwa kuwa ni maadhimisho mawili tofauti.

Mwakilishi wa Vijana katika chama cha KANU Maureen Wanyonyi, kinachoongozwa na seneta wa Baringo Gedion Moi, anasema wiki ya vijana michezo ya kuigiza, warsha, tamasha za kitamaduni na mikutano inayohusisha serikali ya kitaifa, zile za kaunti na washikadau husika huandaliwa. "Madhumuni hasa huwa kuchanganua maswala ya vijana, kuanzia ajira, uwakilishaji wa vijana serikalini, nafasi ya vijana katika biashara na uwekezaji, athari za pombe na dawa za kulevya kwao," anaeleza.

Maadhimisho ya vijana kimataifa yana umuhimu mkubwa kwa nchi yoyote ile, na kulingana na Bi Wanyonyi ni kwamba kuna haja ya serikali kutilia maanani wiki hii ikizingatiwa kuwa vijana ndio wengi wakifuatwa na kina mama, watoto na wazee. Vijana wanakadiriwa kuwa wenye umri wa kati ya miaka 18-35.

Serikali, wanasiasa, jamii ya biashara na washikadau husika hufanya mikutano aina mbalimbali ili kutathmini mahitaji ya vijana. Sikukuu ya kuadhimisha siku ya vijana Kenya huwa Agosti 10.

Mada ya 2018 ni; Maeneo Salama kwa Vijana, japo nchini Kenya vijana wameonekana kutengwa hasa katika nyadhifa mbalimbali serikalini. Kwa mfano katika uteuzi wa baraza la mawaziri, mabalozi, makatibu na uongozi wa taasisi za kiserikali vijana hawajawakilishwa.

Kigezo kikuu cha kutoteuliwa husemekana kuwa ukosefu wa tajiriba ya kutosha, na kulingana na Bi Wanyonyi ni kwamba kuna haja vijana kuteuliwa kuwa manaibu wa vigogo hao au hata katika ofisi zao ili wapate tajiriba hiyo. "Wakikosa kuwa katika ofisi hizo tajiriba wataipata wapi?" ashangaa. 

Makampuni ya kibinafsi ndiyo yameonekana kutambua juhudi za vijana kwa kuwapa nyadhifa hizo, kinyume na taasisi za serikali. Sawa na wanapohitimu vyuo kwa stashahada, shahada, shahada za uzamili na vyeti vingine, kuna baadhi ya waajiri ambao mahitaji huwa tajiriba, mfano wa kuanzia miaka mitano.

Katika sekta ya biashara vijana wanafaa kuhusishwa kwa kiwango kikubwa. Kwenye ajenda kuu nne za Rais Uhuru Kenyatta uundaji na uimarishaji wa viwanda nchini ambayo ni moja ya ajenda, unahusisha kubuni nafasi za ajira kwa vijana. Mbali na ajenda hiyo, usalama wa chakula, matibabu bora na kuwepo kwa makazi bora ni miongoni mwa ajenda hizo.

Katika ajenda ya viwanda, Rais Kenyatta atathmini kwa kina kuhusu sekta ya biashara. Hata hivyo, serikali ya Bw Kenyatta kwa ushirikiano na Naibu wake William Ruto inapigiwa upatu hasa kwa utoaji wa mikopo isiyo na riba ya kuanzisha na kuimarisha biashara hasa kwa vijana na kina mama. Mikopo hiyo hutolewa kwa walio kwenye makundi.

Ingawa mikakati inafaa kuwepo kwa vijana katika biashara. Bw Stephen Njogu Mbithe ambaye hufanya kazi ya kuunda shanga, mikufu, herini, tai za shanga, na bidhaa zingine za mapambo anasema biashara zinalemazwa na ushuru unaotozwa na serikali za kaunti. Kijana huyo anayefanyia kazi yake eneo la Toezz, Githurai 45 kaunti ya Kiambu anapendekeza swala la utozaji ushuru hasa kwa biashara za vijana kutathmniwa. "Nikichukua mkopo huo, biashara inahitaji muda ili iimarike kikamilifu. Ushuru wa kiwango cha juu ukitozwa biashara tunazoanzisha zitafifia," asema Njogu.

Mfanyabiashara huyo alianza uundaji wa mapambo 2016 akiwa kidato cha nne, na ni kazi ambayo kwa sasa imekuwa kitega riziki chake. Njogu anasema maadhimisho ya IYD yaangazie biashara kwa vijana kwa kuwa nafasi za ajira zimekuwa finyu. "Vijana tumechukua mkondo wa kuwekeza katika juakali, hivyo basi serikali iangazie kwa undani biashara kwa vijana," aeleza.

Ulevi

Unywaji wa pombe na utumizi wa dawa za kulevya pia ni swala ambalo huangaziwa wakati wa kuadhimisha IYD.

Nchini Kenya, baadhi ya vijana wamekuwa mateka wa janga hilo. Kaunti ya Kiambu ni moja ya zilizoathirika pakubwa kwa unywaji wa pombe hasa ile haramu. Kaunti ya Mombasa nayo utumizi wa mihadarati na dawa za kulevya imekuwa ratiba ya kila uchao.

Changamoto hiyo imechangia kudorora kwa hali ya usalama, ambapo vijana wanajihusisha na visa vya uhalifu. Haja ipo kuwakomboa vijana kutoka kwa minyororo hiyo, isiwe hela kidogo wanazopata wanazielekeza kwa ununuzi wa pombe na dawa za kulevya. Ifahamike wazi bidhaa hizo zina athari kwa afya ya mtumizi. Maswala hayo yawe baadhi ya yatakayoibuliwa katika IYD, Kenya mwaka huu haswaa kwa kulenga vijana shuleni, vyuo na taasisi za juu za elimu kwa kuwa ndiko pombe na dawa za kulevya zimekolea.

IYD ilizinduliwa na muungano wa kimataifa UN 1999. Maadhimisho ya kwanza yalifanyika mwaka 2000. Mwaka jana mada ya IYD ilikuwa 'Vijana Kuangazia Umuhimu wa Amani'.