Wizarani waache Watendaji waandamizi siasa

Maji

Maji kutoka kwa mfereji. Picha/HISANI 

Na TAHARIRI YA MWANANCHI

Imepakiwa - Saturday, October 7  2017 at  14:23

Kwa Mukhtasari

Mwishoni mwa wiki iiyopita Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo alikutana na wawakilishi wa viongozi wa mamlaka 19 za maji mjini Dodoma ili kujadiliana nao majukumu yanayowakabili.

 

MWISHONI mwa wiki iiyopita Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo alikutana na wawakilishi wa viongozi wa mamlaka 19 za maji mjini Dodoma ili kujadiliana nao majukumu yanayowakabili.

Tujuavyo, wizara hiyo ikisaidiana na mamlaka mbalimbali  za maji ndiyo yenye wajibu wa kusambaza majisafi na salama kwa wananchi wake.

Malengo ya usambazaji maji yamo kwenye ilani ya uchaguzi za vyama lakini kwa kuwa CCM ndiyo iliyoshinda, ilani yake ndiyo inayotumika.

Tunaamini Katibu Mkuu huyo aliwaita wawakilishi hao wa viongozi wa mamlaka hizo kuona namna bora ya utekelezaji wa ilani hiyo inayoeleza namna ya kuwaondolea adha na  kero wananchi hasa wa vijijini ambako baadhi ya maeneo hushirikiana maji na mifugo.

Maeneo mengine huko vijijini wananchi hutembea umbali mrefu kufuata maji ya visima ambayo si salama ingawa yanaonekana kuwa safi  na hata wanaopata maji ya bomba wapo wanaopata  mara moja au mbili kwa wiki.

Kwa hiyo jukumu kubwa la wizara hii  ni kuhakikisha kuwa majisafi na salama  yanatiririka hadi kwenye majumba ya watu au yanapatikana umbali ufupi.

Changamoto hii itaondolewa kwa kuhakikisha miradi mingi inaanzishwa na inasimamiwa kikamilifu.

Wakati kukazia mikakati hiyo katika mkutano huo, Profesa Kitila alizungumzia mambo mawili.

Kwanza uchaguzi wa mwaka 2020 na pili alikemea majungu.

Kuhusu uchaguzi mkuu, Profesa Kitila aliahidi kuwa waizara yake itakuwa mfano bora wa kumsaidia Rais John Magufuli kupata kura nyingi za kutosha bila kufanya kampeni mwaka 2020.

Kwamba ahadi yake haitakwenda bure kwa kuwa mwaka 2010 Rais Magufuli ataanzia Dar es Salaam hadi Kigoma akipunga mkono bila kusema neno lakini kura atakazopata zitakuwa za kishindo.

Katiku Mkuu huyo alisema Wizara ya Maji na Umwagiliaji ndiyo kila kitu kwa kuwa inagusa wananchi wa hali ya chini na juu na ndiyo maana kuna ulazima wa kuwa na usimamizi wa kutosha.

Wivu

Halafu alikemea tabia ya vyama vya wafanyakazi kutengeneza majungu ya wivu na kugeuza mamlaka za maji kuwa vichaka vya majungu na umbea na matokeo yake ni kuumiza na kuwabambikizia tuhuma viongozi hasa wakurugenzi wa mamlaka hizo.

Kisha aliwataka wafanyakazi kuopigania haki zao huku wakitimiza wajibu wao kwa kuwa bila kufanya kazi kwa tija hawawezi kuwa na haki ya kudai masilahi bora.

Hata changamoto kubwa ya madeni yanayofikia Sh 15 bilioni ambazo mamlaka  zinadai taasisi na mashirika ya umma haikupewa ufumbuzi isipokuwa siasa.

Tunamshauri katibu huyo mkuu na watendaji wake wengine wa ngazi yake kujiepusha na kauli zinazotafsiriwa kuwa ni za kisiasa  na kuibua malalamiko yasiyo ya lazima dhidi ya uendeshaji wa Serikali.

Mamlaka iliyomteua iliona anafaa kuwa mtendaji wa Serikali na si kuhubiri wa siasa   katika shughuli za utendaji.

Ilani ya chama tawala itapokewa vizuri kama watendaji watajikita katika majukumu yao ya utekelezaji badala ya kuwagawanya wananchi kwa kuingiza kauli za kisiasa.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au 0754780647