Tahariri Tarehe 26th February, 2019 Madereva wa Serikali waheshimu sheria

 

Imepakiwa - Tuesday, February 26  2019 at  14:37

 

Masikio na macho ya Watanzania yamesikia na kuona tena habari ya kusikitisha, ikiwahusu maofisa tisa huku wanane kati yao wakiwa ni wa Serikali na mmoja wa asasi ya kiraia waliofariki katika ajali ya gari huko Morogoro.

Watumishi hao wa wizara ya ardhi kitengo cha upimaji ardhi, walikuwa wakirejea kutoka kwenye shughuli za kiofisi katika Kata ya Kiberege, wilayani Kilombero walikokwenda kugawa hati za ardhi za kimila.

Vifo hivyo ambavyo vinafanya idadi ya watumishi wa umma waliokufa katika ajali zilizohusisha magari ya Serikali kufikia 22, ndani ya miezi tisa, vinatonesha vidonda vya wapendwa wetu mbalimbali ambao sasa hatunao tena kutokana na ajali.

Kama ilivyokuwa katika baadhi ya ajali, hii nayo inaelezwa kuwa ilitokana na mwendo kasi wa dereva uliomfanya ashindwe kulidhibiti hivyo kugonga ukingo wa daraja kisha kutumbukia mtoni.

Sababu kama hiyo ya mwendo kasi imewahi kutolewa katika ajali nyingi huko nyuma, lakini inavyoonekana baadhi ya madereva wa Serikali ama wamekuwa wagumu kuelewa somo au kuna msukumo unaowachochea kuongeza mwendo na kupitiliza ule ulioelekezwa na kushauriwa kitaalamu kwa ajili ya usalama wa dereva, abiria na gari lenyewe.

Kujirudia mara kwa mara kwa ajali kwa magari ya Serikali kunapaswa kufikirisha zaidi, kuona chanzo ni nini. Je, madereva wake wanatii sheria za usalama barabarani kama miongozo inavyotaka kwani kwenda kinyume nayo kunaweza kuwa sababu.

Si hivyo tu, ni vyema pia kujua kama madereva wa Serikali wanapata muda wa kutosha wa kupumzika kwani wapo wanaoonekana wakitembea umbali mrefu bila ya mapumziko jambo ambalo linaweza kuchangia kinachotokea kwa magari ya Serikali.

Ni vyema pia kujiuliza kama askari wa usalama barabarani wanawakagua na kuwafuatilia madereva wa Serikali wanapopita katika maeneo yao kama wanavyofanya kwa madereva wa magari binafsi au yale ya taasisi zisizo za kiserikali, endapo mambo yanafanyika tofauti na hivyo tusishangae kutokea ajali za mara kwa mara kwa magari hayo kwani madereva wake hujihisi hawafungamani na sheria zilizopo.

Ajali za barabarani ni janga linalopaswa kupigwa vita na kila mmoja wetu ya kutoa fursa hata ya sekunde moja bila ya kujali chombo unachosafiria ni cha binafsi au cha umma.

Kwa viongozi na watumishi wa umma wanaosafirishwa na magari ya Serikali wanapaswa kuwa wadau wa kwanza kupinga, kukemea na kuzuia kiashiria chochote kinachoweza kusababisha ajali.

Iwapo abiria walioko katika gari la Serikali watafumbia macho na kuacha madereva wayatembeze kwa mwendo usio rafiki kwa usalama, watambue kuwa wanachochea kutokea kile kinachotokea sasa.

Aidha, madereva wapewe fursa ya kupumzika nao waitumie kikamilifu kwani inaelezwa wapo baadhi yao wako tayari kutembeza magari safarini hata wakiwa wamechoka kwa kutazama posho wanayopewa kutokana na safari husika.

Watu 22 kufariki dunia kutokana na ajali za barabarani zilizohusisha magari ya Serikali ndani ya miezi tisa pekee sio jambo la kufumbiwa macho, bali kila mmoja ahakikishe anatimiza wajibu wake kupambana na hali hiyo ili usafiri wa magari uwe salama na kusaidia maendeleo ya nchi.

Endapo tutaendelea kufurahia mwendo kasi na kuwafumbia macho madereva wa Serikali wanaokiuka sheria ni sawa na kutoa kibali cha kuendelea kutuweka hatarini tuwapo kwenye usafiri huo.

La msingi ni madereva wote; wa Serikali na magari binafsi waheshimu sheria.

Tunaamini iwapo sheria zitazingatiwa na kila mmoja akawa msimamizi ajali kwa magari ya Serikali zitapungua kama sio kumalizika kabisa.