http://www.swahilihub.com/image/view/-/4693604/medRes/2075024/-/q7vanb/-/dewa.jpg

 

Magufuli, Museveni wakubaliana kuhusu sukari, treni

John Pombe Magufuli

Rais John Magufuli akipeana mkono na mgeni wake, Rais Yoweri Museveni wa Uganda walipokutana na kufanya mazungumzo Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Museveni alikuja nchini katika ziara ya siku moja. Picha na Anthony Siame 

Na LAWRENCE ONGARO

Imepakiwa - Friday, August 10  2018 at  11:20

Kwa Muhtasari

Rais John Magufuli wa Tanzania na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni, walikutana Alhamisi jijini Dar-es Salaam kujadili biashara kati ya mataifa hayo jirani.

 

DAR/NAIROBI

RAIS John Magufuli wa Tanzania na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni, walikutana Alhamisi jijini Dar-es Salaam kujadili biashara kati ya mataifa hayo jirani.

Kwa muda mrefu kumekuwa na uhusiano usio bora kati ya nchi hizi mbili na kwa hivyo ilikuwa ni bora kuboresha uhusiano huo.

Hata hivyo, mazungumzo hayo yalizingatia maswala ya sukari inayopitishwa kwenye mipaka kwa njia isiyo halali.

Imedaiwa kuwa sukari nyingi kutoka Uganda imekuwa ikikataliwa isiingizwe Tanzania ikidaiwa kiwango kikubwa kinatolewa nchi jirani ya Kenya.

Kwa muda wa miezi kadha sasa biashara ya sukari ya kutoka  ng'ambo imefurika Kenya huku ikidaiwa ina madini yanayoweza kuhatarisha maisha ya binadamu.

Tayari serikali ya Tanzania imeweka kiwango cha asilimia 25 ya ushuru kwa sukari inayoingia huko kutoka Uganda; hatua ambayo limeleta malalamiko kwa wanaohusika na  usafirishaji wa bidhaa hiyo.

Afisa mmoja wa ushuru kutoka nchini Uganda alisema kuwa mnamo mwezi Mei sukari kiwango cha magunia 12,000 takribani tani 600 ilizuiliwa kuingia Tanzania na maafisa wa ushuru huku ikirejeshwa ilikotoka.

Katika mkutano huo wa Alhamisi katika Ikulu ya Dar es Salaam Rais Museveni alisema nchi hizo mbili zitaendelea kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu ili kudumisha maelewano katika Afrika Mashariki na Kati.

Aidha, viongozi hao walikubaliana kwamba bidhaa zitakuwa zikisafirishwa kwa treni kati ya Dar es Salaam na Jinja, Uganda.

Hatua hiyo, viongozi hao walisema inalenga kuondoa ugumu wa usafiri wa barabarani.

Kunawiri

Rais Museveni kwa upande wake alisema ni vyema kukuza udugu huo ili biashara izidi kunawira baina ya nchi hizo.

"Kukiwa na migogora ya kila mara hakuna biashara ya maana itashuhudiwa baina ya nchi za Afrika Mashariki na Kati," alisema Rais Museveni.

Kwa wakati huu kitendawili cha kuingizaji wa Sukari nchini kimezidi kulenga Kenya huku serikali ikijaribu kuchunguza uhalali wa bidhaa hiyo.

Kwa zaidi ya miezi miwili sasa mjadala wa sukari ilio na madini hatari umeendelea ambapo ukweli wa mambo bado haujajulikana kamili.

Alhamisi bunge la kitaifa Kenya lilitupilia mbali ripoti ya sukari.