http://www.swahilihub.com/image/view/-/4094064/medRes/1751432/-/3wt3psz/-/muhu.jpg

 

Magufuli awasubiri wabunge watatu CCM

Sospeter Muhongo

Profesa Sospeter Muhongo. Picha/MAKTABA 

Na KELVIN MATANDIKO

Imepakiwa - Wednesday, September 13  2017 at  12:00

Kwa Mukhtasari

Mwenyekiti wa CCM Rais John Magufuli anawasubiri wabunge watatu kujibu maswali kwa nini majina yao yamekuwa yakitajwa mara kwa mara katika ripoti  zinazohusu ufisadi katika nyadhifa walizowahi kusimamia serikalini.

 

DAR ES SALAAM, Tanzania

MWENYEKITI wa CCM Rais John Magufuli anawasubiri wabunge watatu kujibu maswali kwa nini majina yao yamekuwa yakitajwa mara kwa mara katika ripoti  zinazohusu ufisadi katika nyadhifa walizowahi kusimamia serikalini.

Hatua hiyo inawaweka wabunge hao kwenye wakati mgumu na kuna uwezekano wa kutopitishwa tena kwenye vikao vya juu ndani ya chama hicho katika  mchakato wa uchaguzi mkuu mwaka 2010 licha ya kukubalika majimboni.

Wabunge hao ni Andrew Chenge (Bariadi), William Ngeleja (Sengerema) na Sospeter Muhongo (Musoma Vijijini).

Wabunge hao walitajwa katika sakata la Tegeta Escrow kwa tuhuma tofauti huku Chenge alionekana tena katika sakata la ununuzi wa rada  alipolazimika kujiuzulu uwaziri  wa Miundombinu katika Serikali ya Awamu ya Nne iliyoongoza na Rais Jakaya Kikwete.

Kwa upande wao, Ngeleja na Profesa Muhongo wametajwa pia katika sakata la makinikia ya Madini kupitia nafasi zao kama mawaziri wa zamani wa Nishati na Madini. Hatua hiyo iko mbioni kuchukuliwa kama utekelezaji wa ahadi ya mwenyekiti huyo wa CCM.

Akizungumza wakati wa kukabidhi ripoti ya almasi na Tanzanite Spika wa Bunge, Job Ndugai alionyesha kusikitishwa kwake na wanasiasa hasa wabunge ambao wamekuwa wakitajwa katika ripoti nyingi za ufisadi lakini bado wanarejea katika Bunge kwa kuchaguliwa.

Alisema pamoja na wabunge hao kutajwa kwenye matukio ya namna hiyo wakirudi majimboni wanachaguliwa na wananchi kwa kuwa wao hawajui tabia zao.

“Vyama vya siasa vinawapitisha, wanashinda ubunge na wakija mimi nitawaapisha na juzi Profesa Lipumba kaniletea wapya nimewaapisha,” alisema Ndugai.

Baada ya kauli hiyo, Rais Magufuli alisema ni kweli kuna watu wametejwa kwenye ripoti nyingi na wakiwa bungeni wamekuwa wakichangia hoja kwa nguvu zote.

Rais Magufuli alimuuliza Ndugai kama bungeni hawana utaratibu wa kuwashugulikia watu wa namna hiyo au hata kubadili kanuni ili waweze kuwashugulikia.

Hata hivyo alisema kwa kuwa yeye ni mwenyekiti wa CCM anasubiri barua ya Spika na ikiwafikia watashughulikiwa kwa mujibu wa miiko ya chama hicho huku akiamini vyama vingine vitafanya hivyo.

Hoja ya kuwabana wanasiasa wenye tuhuma za ufisadi ziliibuka baada ya wanasiasa hasa wabunge kutajwa kwenye ripoti mbalimbali zilizochunguza tuhuma za ufisadi.

Wabunge wa CCM waliotajwa katika ripoti hizo na ambao hawana nafasi serikalini kwa sasa ni Ngeleja, Profesa Muhongo, na Chenge.

Wakati wa kashfa ya Escrow Ngeleja, Chenge na Victor Mwambalaswa (Lupa CCM) walilazimika kujiuzullu uenyekiti wa kamati mbalimbali za Bunge baada ya kutuhumiwa kupokea mgawo wa fedha za Escrow.

Ngeleja alidaiwa kupewa Sh 40.4 milioni, Chenge Sh 1.6 milioni na Mwabalaswa alidaiwa kuwa na mgongano wa kimaslahi.

Mbunge mwingine ni Profesa Anna Tibaijuka (Muleba Kusini) anayedaiwa kupokea Sh 1.6 milioni katika mgawo wa Escrow na kulazimika kujiuzulu uwaziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi.