http://www.swahilihub.com/image/view/-/5119662/medRes/2346601/-/qx92rd/-/kesi+pic.jpg

 

Mashahidi kesi ya Zitto wafunguka

Na Pamela Chilongola,Mwananchi pchilongola@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Friday, May 17  2019 at  12:17

 

Dar es Salaam. Shahidi wa pili katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto, Kabwe ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi alivyolichukia jeshi la polisi baada ya kuona video kwenye mtandao wa kijamii wa you tube.

Akitoa ushihidi jana, shahidi huyo, Mashaka Juma ambaye ni msanii wa filamu alidai video hiyo ilikuwa ikimuonyesha Zitto akielezea kuwa polisi walienda kuwachukua watu hospitali na kwenda kuwaua.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahidi, Mashaka alidai Oktoba 29, mwaka jana akiwa eneo la Kimara Korogwe jijini Dar es Salaam na wenzake wakicheza drafti, alifika mwenzao aliyemtaja kwa jina la Frank Zongo na kuwauliza kama wamepata habari yoyote.

“Tulimweleza hatujui ndipo akatuambia Zitto ndie habari ya mjini na kututolea simu yake kisha akatufungulia na tukaangalia kwenye you tube.”

Alidai kwenye video hiyo walimwona Zitto akililaumu jeshi la polisi kwa mambo mbalimbali ambayo limefanya wilayani Uvinza Mkoa wa Kigoma.

Alidai katika video hiyo ilimuona Zitto akidai kuwa jeshi la polisi limewanyanyasa wananchi, kuteka watu akiwamo aliyemtaja kwa jina la Mo wa Simba na polisi walivyoenda hospitali kuwateka watu waliokuwa wakitibiwa na kwenda kuwaua.

“Video hiyo inamuonyesha Zitto akieleza jinsi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini alivyoshindwa kuwadhibiti askari wake,” alidai na kuongeza:

“Zitto namfahamu tangu akiwa Chadema na nikawa mfuasi wake hadi leo akiwa ACT- Wazaledo, binafsi nilimuamini kutokana na taarifa hiyo, nililiona Jeshi la Polisi halina thamani na kulichukia.”

Shahidi wa tatu, Shabani Hamisi mbaye ni mfanyabiashara wa Manzese, alidai Oktoba 29 mwaka jana akiwa anaenda kazini kwake aliwakuta watu wamekaa vikundi na alipowasogelea alisikia wakizungumzia polisi kuua watu maeneo ya Uvinza.

Alidai akiwa nyumbani kwake akiwaza Tundu Lissu alipigwa risasi nyingi na alimwamini Zitto aliyoongea na tangu siku hiyo alilichukia jeshi la polisi.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi leo itakapoendelea na ushahidi kwa upande wa mashtaka.

Katika kesi hiyo, Zitto anakabiliwa na mashtaka ya uchochezi, akidaiwa Oktoba 28 mwaka jana alitoa maneno hayo.