Matukio ya utekaji nchini hayapaswi kuzoeleka

Imepakiwa - Thursday, May 9  2019 at  11:07

 

Kati ya mambo yaliyoshtua Taifa mwaka 2018 ni matukio ya watu, kama wafanyabiashara, viongozi wa dini, wanafunzi na watoto, kutekwa na watu wasiojulikana au kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Kutopatikana kwa baadhi ya watu waliotekwa au kupotea kuliongeza hofu huku vyombo vya dola vikiapa kufanya kila linalowezekana kumaliza matukio hayo.

Kutokana na matukio hayo, vyombo vya dola, hususan Jeshi la Polisi, vilijikuta katika wakati mgumu baada ya kulaumiwa na wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu kwa madai kuwa wameshindwa kuwakamata wahusika au washukiwa.

Lakini matukio hayo yameendelea kutokea baada ya mkazi wa Mkoa wa Songwe, Mdude Nyagali kutoweka na kuzidisha taharuki kuhusu usalama wa watu.

Licha ya polisi kusema kuwa wanafanya uchunguzi, bado Watanzania wanahitaji uhakika kutoka kwa vyombo vya dola wa kumaliza uhalifu wa namna hiyo kwa kuwa unaonekana kama haujadhibitika tangu ulipoanza kuibuka mwaka 2016.

habari za Mdude kutekwa zimekuja wakati Watanzania wakiwa bado na kumbukumbu ya kutoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa mwandishi wa habari Azory Gwanda, Ben Saanane, Sheikh Bashir Gora na wengine wengi.

Kupotea kwa Watanzania hao na wengine ambao baadaye walipatikana, kunaliumiza Taifa ndani na nje.Uliacha matukio ya awali ambayo watekaji walikuwa wakishinikiza kupewa fedha, matukio ya hivi karibuni yamekuwa na sura tofauti kwa kuwa watekaji hawapatikani wala vidokezo kwamba ni watu gani, hazipatikani.

Lakini polisi imekuwa ikiendelea na majibu yaleyale kuwa “tunaendelea kuchunguza” na wakati mwingine kuwalazimisha kunyamaza wale wanaohoji sana.

Hatuna shaka na utendaji wa Jeshi la Polisi, lakini wananchi wangependa kuona matunda ya uchunguzi wao kuhusu matukio hayo kwa kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu maendeleo ya uchunguzi wao ili kuwapa imani wananchi na kuwafanya wajisikie wanawajibika kutoa ushirikiano.

Katika mazingira ya utekaji na ambayo wanaofanya matukio hayo hawatangazwi kwamba wamepatikana au kuna tetesi za wahusika, ni vigumu kwa wananchi wanaoweza kuwa na taarifa, kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kuwa hawajisikii kuwa salama.

Tunashauri Jeshi la Polisi liandae utaratibu wa kuwa linatoa taarifa za mara kwa mara kuhusu maendeleo ya upelelezi ili Taifa lijue kinachoendelea na kuondokewa na hofu.

Pia, kuna haja kwa wanasiasa kutoa kauli thabiti zinazoonyesha kuwepo kwa hatua madhubuti za kuwasaka wahusika na kukomesha uhalifu huo ambao unaonekana kama unazidi kukomaa katika Taifa lililojijengea heshima ya kuwa la amani na utulivu kwa kipindi chote cha miaka zaidi ya 50 ya uhuru ambao pia ulipatikana kwa njia ya mazungumzo na amani.

Wananchi pia wana wajibu mkubwa wa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kuviwezesha kufanikisha kuwakamata watekaji na hatimaye kuwafikisha mahakamani ili waadhibiwe na kukomesha vitendo hivyo.

Matukio haya hayajawahi kuzoeleka, hayazoeleki na wala hayatakiwi kuzoeleka na hivyo mamlaka husika hazina budi kuchukua hatua kuhakikisha hayazoeleki na hayaendelei kujenga hofu itakayozoeleka kwa wananchi.