http://www.swahilihub.com/image/view/-/5026216/medRes/2281635/-/suqbvdz/-/mbunge+pic.jpg

 

Mbunge wa Chadema ang’olewa Ubunge

Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari 

Na Tausi Mbowe, Mwananchi tmbowe@mwananchipapers.co.tz

Imepakiwa - Friday, March 15  2019 at  08:57

 

Dar es Salaam. Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari amepoteza sifa ya kuendelea na ubunge baada ya kutohudhuria vikao vya mikutano mitatu mfululizo ya Bunge.

Taarifa iliyotolewa jana na Bunge, ilitaja mikutano hiyo kuwa ni wa 12 ulioanza Septemba 4 hadi 14 na Novemba 6 hadi 16, 2018 pamoja na ule wa Januari 29 hadi 9, 2019.

Taarifa hiyo ilisema Spika Job Ndugai amemuandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage kumtaarifu kuwa jimbo hilo lipo wazi kutokana na mbunge wake kupoteza sifa.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusiana na taarifa hiyo, Nassari alisema ameshangazwa licha ya kwamba ni kweli hakuhudhuria vikao hivyo, lakini alitoa taarifa.

“Huu mkutano uliopita (wa Januari 29 hadi Februari 9) nilikuwa nje ya nchi namuuguza mke wangu alikuwa na matatizo ya uzazi na nilimjulisha Spika kupitia barua niliyoituma kwa email (barua pepe),” alisema Nassari.

Alisema alifanya hivyo baada ya kuwasiliana na msaidizi wa Spika na kumshauri kuandika barua.

Kwa mujibu wa Nassari, katika barua hiyo ya Januari 29 kwenda kwa Spika, ilielezea kuwa asingehudhuria mkutano huo uliokuwa unaendelea kutokana na kuwa nje ya nchi akimuuguza mke wake aliyekuwa amejifungua siku mbili zilizopita.

Mwananchi lilipotaka kujua kama barua hiyo ilijibiwa, Nassari alisema, “haikujibiwa hadi leo na mimi nimerudi wiki mbili zilizopita, hapa ninapozungumza natoka kwenye kikao cha Kamati za Bunge ya Maliasili tulikuwa Chuo cha Usimamizi cha Wanyamapori, Mweka (Kilimanjaro).”

Mbunge huyo aliyeingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2012 baada ya kushinda uchaguzi mdogo, alisema atachukua hatua kwa kile alichodai tayari alishatoa taarifa kwa Spika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa NEC, Dk Athuman Kihamia alipoulizwa iwapo watatangaza uchaguzi mdogo kwenye jimbo hilo kwa muda uliobaki kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2020, alisema, “uchaguzi unafanyika kama kawaida, muda bado upo ili uchaguzi usifanyike ni miezi 12 kabla ya mkutano wa Bunge wa mwisho kufanyika kuelekea Uchaguzi Mkuu. Kwa kawaida mkutano wa mwisho huwa Julai mwanzoni,” alisema Dk Kihamia.

Alisema hata jimbo likiwa wazi hadi Julai mwanzoni mwaka huu, bado uchaguzi unaweza kufanyika kama kawaida.

Kwa mujibu wa taarifa ya Bunge, uamuzi wa Spika umezingatia masharti ya Katiba ibara 71 (1)(c) inayoeleza kuwa, “mbunge atakoma kuwa mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge ikiwa atakosa kuhudhuria vikao vya mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ya ruhusa ya Spika.”

Ibara hiyo imefafanuliwa katika Kanuni ya 146(1) na (2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Januari 2016. Kanuni hiyo inaeleza kuwa, “kuhudhuria vikao vya Bunge na kamati zote ni wajibu wa kwanza wa mbunge. Mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika iliyotolewa kwa maandishi, atapoteza ubunge wake na Spika ataiarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi.”

Chadema wazungumza

Akizungumzia uamuzi huo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema ni mwendelezo wa kukidhoofisha chama hicho.

“Wanataka tuache mambo ya msingi tu-concetrate (tujikite) na jambo moja ambalo haliwezi kukisaidia chama na badala yake kuendelea kukidhoofisha kwa kutumia kila fursa inayopatikana,” alisema Mwalimu.

Hata hivyo, alisema anaamini Bunge lingeweza kutumia busara kwa kufuata taratibu za kiutawala ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na Nassari ili kujua tatizo lake.

“Mzazi akimkuta mtoto wake amevunja birauli hawezi kumpiga tu, busara ni kumuuliza na kumsikiliza kwanza kwa sababu hata mahakama pamoja na mshtakiwa kupatikana na hatia, bado hakimu anatoa nafasi ya mtuhumiwa kujitetea, iweje katika taasisi zetu hilo halifanyiki,” alihoji Mwalimu.

Alipoulizwa kama Chadema ilikuwa na taarifa za mbunge huyo kutohudhuria vikao vya Bunge alisema, “sisi tunajua Nassari alikuwa na matatizo ya kifamilia na kuna wakati alikuwa nje ya nchi kwa masomo ingawa hatujui kama mpaka sasa hajahudhuria vikao vingapi.”

Mwalimu alisema msimamo wa chama chao wa kutohudhuria chaguzi ndogo uko palepale na hata kwa jimbo hilo hawatashiriki.

“Wameamua kutumia mabavu na kuhakikisha wanashinda katika chaguzi zote ndogo hatuwezi kushiriki siyo huu tu, bali hata kama wabunge wetu wote watapoteza sifa hatuwezi kushiriki.”

Msekwa anena

Akizungumzia hatua hiyo, Spika mstaafu, Pius Msekwa alisema kuwatimua wabunge wenye tabia hiyo ni sawa kwa sababu wanaonyesha jeuri.

“Mbunge anatakiwa kuwawakilisha wananchi, sasa wewe huhudhurii vikao, huo ni uhalifu na adhabu yake lazima iwe kali. Ni lazima wabunge waheshimu sheria,” alisema Msekwa.