Mvua iliyonyesha saa tano Dar ituamshe

 

Imepakiwa - Tuesday, March 5  2019 at  09:03

 

 Mvua zilizoanza juzi alfajiri na kunyesha kwa takriban saa tano zimeacha baadhi ya sehemu za Jiji la Dar es Salaam zikisimamisha shughuli zake kutokana na mafuriko na baadhi ya maeneo kutopitika kwa muda hivyo kuathiri biashara na shughuli nyingine za kiuchumi.

Katika maeneo mbalimbali pia watu waliohitaji kutoka sehemu moja kwenda nyingine ama walilazimika kusubiri au kutumia njia kuzunguka kufika walikokusudia. Hizo ni miongoni mwa athari zilizotokana na mvua tunayoweza kusema ya muda mfupi kwa kuwa ilidumu kwa saa chache.

Ni ndani ya muda huo wakazi wa jiji hilo walikumbushwa mvua kubwa iliyonyesha Machi 2017 ambayo ilisababisha mafuriko, vifo, uharibifu wa mali na watu wachache hususan waliokuwa wakiishi maeneo ya mabondeni kupoteza makazi yao.

Hali hiyo inatokana na ujenzi katika sehemu kubwa ya Dar es Salaam kutozingatia mipango miji kwa ajili ya kufanikisha huduma za kijamii, kama mitaro ya maji ya machafu.

Hata hivyo, licha ya changamoto hizo haiondoi ukweli kwamba kama jamii bado hatujafanya kikamilifu kinachoweza kusaidia kuepusha mafuriko katika maeneo tunayoishi - kuanzia ujenzi wa makazi na hata kuhakikisha kuwa hayatuami. Licha ya maeneo mengi kuwa na makazi holela na ongezeko la watu na makazi ambayo baadhi hayana miundombinu ya kupitisha maji, kila mkazi wa jiji anapaswa kutimiza wajibu na kufanya juhudi za kukabiliana na mafuriko.

Katika baadhi ya maeneo, wajenzi wa barabara hufukia mitaro ya maji machafu iliyo katika makazi na hivyo kusababisha maji yakwame na kufurika wakati wa mvua.

Tabia hiyo ni moja ya sababu za mafuriko ambayo husababisha shughuli za kiuchumi kusimama kwa jambo ambalo linaweza kuepukika.

Pamoja na sababu hiyo, bado wananchi wana wajibu wa kuweka sawa mazingira yao katika maeneo ambayo hakuna ujenzi unaoweza kusababisha mafuriko mitaani.

Kwa mfano, kuwa na siku maalumu kwa mitaa kwa ajili ya kushughulikia usafi katika makazi. Ule mpango wa usafi wa kila Jumamosi haukufanikiwa kutokana na ukweli kuwa haukuwa wa pamoja; kila mtu alifanya usafi kwake na kusahau maeneo yanayotumiwa na jamii kwa ujumla, kama vile barabara na mifereji ya maji.

Hili pia linaweza kufanikishwa na viongozi wa mitaa. Ni wajibu wa viongozi wa mitaa kubuni mbinu za kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za usafi wa maeneo ya umma katika mitaa yao, badala ya kukaa ofisini na kutuma polisi jamii kwa ajili ya kukusanya faini kwa wasiofanya usafi majumbani kwao.

Mbali ya yote hayo, halmashauri za wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam hazina budi kubuni mikakati ya kuondoa kero kwenye maeneo ambayo imekuwa ni kawaida kujaa maji kila inaponyesha mvua kidogo tu.

Mfano maeneo kama Tazara, Maktaba na Mbezi ambako yanaonekana kama ni ya kawaida na hayawezi kuepuka kujaa maji kila mvua inaponyesha. Ni aibu kwamba maeneo hayo na mengine yamekuwa na tatizo hilo kwa miaka mingi, kiasi kwamba watumiaji wa barabara zinazopita maeneo hayo hulazimika kutafuta njia nyingine kila wanapoona mvua hata kabla ya kuambiwa kuwa yamejaa maji.

Hali hiyo ni lazima ikomeshwe kwa kuwa si tu inaathiri shughuli za kiuchumi, bali ni aibu kwa jiji kama la Dar es Salaam kuwa na doa hilo miaka na miaka.