Raia wamtaka Bashir kizimbani

Imepakiwa - Wednesday, May 15  2019 at  13:07

 

Khartoum. Wakati mwendesha mashtaka mkuu wa Serikali ya Sudan, amesema amemfungulia mashtaka mengine, rais aliyeondolewa madarakani, Omar al-Bashir; raia wa nchi hiyo wamesema hawataamimi hadi wamwone kiaimbani.

Mashtaka hayo ya uchochezi na mauaji ya waandamanaji yametokana na uchunguzi uliofanywa kuhusu mauaji ya daktari aliyekuwa akimtibu majeruhi wa maandamano.

Kuuawa kwa daktari huyo ndiko kulichochea kuondolewa kwake madarakani mwezi uliopita baada ya kuitawala nchi hiyo kwa miongo mitatu.

Hata hivyo, Bashir ambaye alikamatwa na yuko kwenye gereza lenye ulinzi mkali, hatima yake haijawekwa wazi.

Pia, kiongozi huyo ambaye ni mwanajeshi anakabiliwa madai ya wizi wa fedha za umma ikiwamo kufadhili makundi ya kigaidi.

Kwa mujibu wa BBC, baadhi ya wananchi wa Sudan walisema hawawezi kuamini kushtakiwa kwake hadi watakapomuona amesimama kizimbani.

Desemba, wananchi wa Sudan walifanya maandamano dhidi ya uamuzi wa a kupandisha mara tatu bei ya mkate.

Maandamano hayo ghafla yalibadilika kuwa hasira iliyosambaa kote nchini dhidi ya kiongozi huyo ambaye anasifika kwa utawala wa mabavu.

Daktari huyo alikuwa akiwatibu waandamanaji waliokuwa wamejeruhiwa nyumbani kwake mjini Khartoum wakati polisi walipofyatua mabomu ya kutoa machozi katika jengo lake.

Takwimu za mwezi uliopita za kamati ya madaktari zinasema watu 90 waliuawa katika maandamano, lakini idadi rasmi inayotolewa na mamlaka ni watu 65. Muasisi wa mtandao wa kigaidi wa Al Qaida, Osama Bin Laden aliishi Sudan kati ya mwaka 1992 na 1996.

Marekani iliiweka Sudan kwenye orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi

Mtu mmoja aliyeshuhudia tukio hilo aliiambia BBC kwamba daktari alikuwa ametoka nje ya nyumba yake huku akiwa ameinua mikono yake juu, akawaambia polisi kuwa yeye ni daktari, lakini walimpiga risasi.

Daktari huyo ni miongoni mwa watu kadhaa waliouawa wakati wa maandamano ya kuipinga serikali ya al-Bashir.

Waandamanaji licha ya vitisho vya polisi, waliamua kuweka makao nje ya makao makuu ya jeshi na kudai jeshi limng’oe madarakani al-Bashir.

Baraza la kijeshi lilichukua mamlaka ya nchi Aprili 11, lakini waandamanaji wanasisitiza kwamba jeshi lazima likabidhi utawala wa nchi kwa raia.

Mazungumzo kati ya jeshi na muungano wa upinzani yamekuwa yakiendelea ili kubuni baraza la mpito la utawala wa pamoja litakaloongoza nchi.

Takwimu za mwezi uliopita za kamati ya madaktari zinasema watu 90 waliuawa katika maandamano haya ya Sudan yaliyoanza Desemba, lakini idadi rasmi inayotolewa na mamlaka ni watu 65.

Marekani iliiondolea Sudan vikwazo vya kibiashara vilivyodumu miaka 20, Oktoba mwaka 2017.Hata hivyo inaendelea kuishikilia katika orodha ya mataifa yanayounga mkono ugaidi wa kimataifa pamoja na Iran, Syria na Korea ya Kaskazini.