Rais Magufuli katoa vitambulisho kwa mama Ntilie na Wanachinga

Imepakiwa - Friday, May 17  2019 at  12:32

 

Mwaka jana tulishuhudia Rais John Magufuli akitoa vitambulisho kwa ajili ya wamachinga na mama ntilie nchi nzima kwa wakuu wa mikoa, ambavyo sasa hivi vinaendelea kutolewa kwa walengwa maeneo tofauti nchini.

Wajasiriamali wadogo ni jeshi kubwa ambalo likitumiwa vyema linaweza kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi nchini.

Jeshi hili likipewa elimu ya kina ya fedha likaweza kuzitumia fursa zilizopo sokoni, utakuwa ni muujiza endapo Tanzania haitafanikiwa kupambana na umaskini.

Takriban benki 50 zilizopo nchini zikitumia muda kidogo kuliingiza kundi hili kwenye huduma zake huku wataalamu wa uchumi, biashara na uwekezaji wakilipa elimu stahiki, upo uhakika wa mambo kubadilika.

Hili limefanyika maeneo mengi duniani ambako waliiona haja ya kubadili mfumo wao na sekta nzima ya fedha.

Mapinduzi ya huduma za fedha kwa watu wa kipato cha chini yalianza baada ya kuanzishwa kwa Benki ya Grameen nchini Bangladesh kutokana na ukame ulioathiri mazao na kipato cha wakulima miaka ya 1970.

Mwaka 1983, Benki ya Grameen ilianza kutoa huduma za fedha na kufanikiwa kuwafikia watu wengi maskini, kuzalisha faida na kukuza mtaji ambao umeifanya kuwa na matawi mengi duniani kwa ujumla.

Mpaka sasa hivi mamilioni ya watu wamenufaika na huduma za taasisi hii ambayo inaweza kuwa mfano mzuri kwa taasisi ndogo za fedha nchini kuinua maisha ya Watanzania na kuwaondoa kwenye lindi la umaskini.

Mwanzilishi wa benki alikuwa na imani katika kuwainua wanawake kiuchumi kwa kuwapa nafasi ya upendeleo kwenye huduma, alichokuwa akifanya mwanzilishi huyo ni kwamba benki za biashara zimeelekeza nguvu zake kwa wanaume zaidi na kuwasahau wanawake.

Kwa msimamo huo, yeye na timu yake walithubutu kuanza kutekeleza hilo japokuwa wengi walikuwa na wasiwasi mwanzoni kutokana na imani ndogo kwamba wanawake hawana uwezo wa kumiliki fedha.

Baada ya muda fulani wanawake nchini Bangladesh waliinuka na kuanza kuingia kwenye mifumo ya fedha haraka na kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali ya kiuchumi.

Asasi ndogo za fedha zilikuwa mkombozi wao. Tanzania inalo la kujifunza kwa kuwapa nafasi wanawake kwenye huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi za fedha ili kuinua uchumi wa familia, kaya na Taifa.

Kugundua na kupeleka huduma za fedha kwa watu wenye uhitaji zaidi wa huduma hizo ni muhimu kwa upanuzi wa taasisi husika. Kujitofautisha na benki za biashara nchini Bangladesh katika utoaji wa huduma, kuliipa nguvu Grameen hivyo kujiimarisha zaidi.

Yenyewe iliamini kundi kubwa la watu wenye kipato cha chini ndilo lina mahitaji makubwa ya huduma za fedha, hivyo ilikuwa ni lazima ielekeze huduma na ubunifu wao upande huo.

Taasisi ndogo za fedha nchini zinatakiwa kufikiria kuwafikia watu wenye kipato kidogo badala ya kuendelea kujaza huduma mjini na kuwasahau wenye fursa nyingi waliopo vijijini.

Kutokana na kundi kubwa la wananchi wa Bangladesh kutokuwa na uelewa wa mambo ya fedha na matumizi mazuri sahihi wakati huo, ilikuwa ni lazima kutoa elimu kwa kuwafundisha maana, matumizi sahihi, mikopo midogo na urejeshaji wake.

Haikuwa kazi rahisi lakini walifanikiwa kwa kiasi kwani wanawake wengi waliingia na kuachana na woga waliokuwa nao mwanzaoni. Mazingira haya hayana tofauti na hapa nchini ambapo kuna kundi kubwa la watu ambao hawana elimu sahihi ya masuala ya fedha.

Kugundua uwezo wa wajasiriamali wengi wadogo na kuhakikisha wanatoa ushauri wenye kuleta tija ni jambo muhimu katika kukuza uchumi. Kila mtu anazo chembechembe za ujasiriamali kwa kitu anachokipenda hivyo kuhitaji uwezeshaji utakaofanikisha ndoto zake.

Hilo likifanyika wajasiriamali wengi wadogo watafanikiwa. Uwezeshaji huu utafanikiwa zaidi ukiongezewa elimu na ushauri wa mambo ya fedha kwa kundi hili hususan wanawake watakaosukumwa kuingia kwenye biashara na uwekezaji.

Ni lazima taasisi zetu zifanye haya. Sekta ya asasi ndogo za fedha inahitaji kuiga baadhi ya mambo kutoka Benki ya Grameen ili kiimarike na kukua ili kuwa mhimili kwa watu wenye kipato kidogo. Wamachinga ni jeshi kubwa linalohitaji kuwezeshwa ili kusukuma uchumi wa Taifa mbele.

Endapo mamlaka husika zitaandaa mfumo wa kuliwezesha kundi hili kiuchumi bila shaka uwezekano wa kuibadili sura ya Tanzania kiuchumi itakuwa shirikishi.

Hassan Mnyone ni mtalaamu wa masuala ya taasisi ndogo za fedha anapatikana kwa simu namba; 0657-157122