http://www.swahilihub.com/image/view/-/5123034/medRes/2232095/-/vb03ptz/-/kesi+pic.jpg

 

Rufaa ya mbakaji wa mtoto yagonga mwamba mara mbili

Na Daniel Mjema, Mwananchi dmjema@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Monday, May 20  2019 at  10:18

 

Moshi. Mkazi wa Holili wilayani Rombo, Elian Bariki anayetumikia kifungo cha maisha jela kwa kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka minane, amekwaa kisiki kwa mara ya pili akipinga adhabu hiyo.

Awali, Bariki alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa hilo mwaka 2015, akakata rufaa Mahakama Kuu kupinga hukumu hiyo. Hata hivyo, rufaa yake iliposikilizwa, mwaka 2016, aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Aishiel Sumari, aliiongeza kuwa kifungo cha maisha.

Bariki hakuridhia hukumu hiyo, akakata rufaa Mahakama ya Rufani ambako pia imetupwa.

Uamuzi wa kuitupa rufaa hiyo ulitolewa mwishoni mwa wiki na jopo la majaji watatu, Sivangilwa Mwangesi, Dk Gerald Ndika na Ignas Kitusi ambalo lilisema hata hakimu aliyemhukumu miaka 30 alikosea kisheria.

Pia, majaji hao walitoa ushauri kwa majaji wanaochipukia wakiwataka watumie marejeo katika kesi za ndani ya nchi, kabla ya kuvuka mito na bahari kwenda mamlaka za nje ya nchi.

“Tumeona ni muhimu kutoa angalizo hili kwa sababu katika sheria hii ya makosa ya kujamiana iko vizuri zaidi kulinganisha na kesi ambayo Hakimu (aliyehukumu miaka 30) aliifanyia marejeo,” walisema.

Hukumu hiyo iliyotolewa Aprili 11, 2019 na nakala yake kupatikana Ijumaa iliyopita, ilisema ushahidi dhidi ya Bariki ukiwamo wa mwathirika, ulithibitisha shtaka hilo.

Katika hoja zake, Bariki alidai kuwa hati ya mashtaka ilikuwa na upungufu, mashahidi wa upande wa mashtaka walijikanganya pia kulikuwa na ukiukwaji wa mwenendo na sheria haikuzingatiwa.

Hata hivyo, baada ya jopo hilo kupitia hukumu zote mbili na kupitia hoja za Wakili Ignas Mwinuka na Akisa Mhando, waliona hoja za Bariki hazina mashiko na mshtakiwa huyo ataendelea kutumikia kifungo hicho.