http://www.swahilihub.com/image/view/-/5119722/medRes/2346635/-/dbddffz/-/watoto+pic.jpg

 

Sababu watoto kupata tabu zatajwa

Na  Nazael Mkiramweni, Mwananchi nmkiramweni@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Friday, May 17  2019 at  12:39

 

Dodoma. Imeelezwa kuwa, majukumu mengi, ndoa za mitaala, uhusiano wa wapenzi wengi ni miongoni mwa sababu za familia kuparaganyika na watoto kujitafutia mahitaji yao wenyewe mitaani.

Hayo yamesemwa huku kukiwa na wimbi kubwa la watoto wanaobeba mizigo katika soko kuu la Dodoma na wengine kuzunguka mitaani kuomba fedha za kununua chakula.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mkurugenzi wa Idara ya Watoto kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Mwajuma Magwiza alisema kuna baadhi ya wazazi wana majukumu kwa zaidi ya kaya moja na hivyo kushindwa kuwahudumia vyema watoto wao.

“Hii husababisha kutowajibika kikamilifu kwa familia na hivyo kuchangia watoto kuanza kujitafutia mahitaji yao, kwani wanakosa malezi ya pande zote mbili yaani baba na mama,” alisema.

Magwiza alisema pia wazazi wengi wanakabiliwa na changamoto za kielimu ama kuwa na shughuli nyingi au kutofahamu wawasaidie vipi watoto waweze kufanya vizuri shuleni jambo ambalo linawafanya kujitafutia mahitaji.

Alisema familia imara ni ile yenye mshikamano, kujali na kushirikiana katika masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi hivyo kuwa familia yenye furaha zaidi.

Mmoja wa wazazi, Marry Stephano alisema malezi ya mzazi mmoja ni magumu kwa sababu ya majukumu yote kubebwa na mtu mmoja.

“Wewe ndiye unakuwa baba na mama, unatakiwa kuamka asubuhi na mapema kwa ajili ya kuwatafutia watoto riziki hivyo muda wa kukaa na kuzungumza na watoto kama mzazi unakuwa ni mdogo,” alisema.