http://www.swahilihub.com/image/view/-/4755928/medRes/2107450/-/emouyrz/-/mrezo.jpg

 

Dkt Shein ahimiza kuwepo ushirikiano baina ya dini na Serikali

Ali Mohamed Shein

Rais wa Zanzibar, Dkt Ali Mohamed Shein. Picha/MAKTABA 

Na HAJI MTUMWA, Mwananchi

Imepakiwa - Wednesday, September 12  2018 at  13:35

Kwa Muhtasari

Katika ukanda wa Afrika Mashariki dini za kikristo na kiislamu zilianza kuingia Zanzibar kabla ya maeneo mengine ya ukanda huo.

 

hmtumwa@mwananchi.co.tz

VISIWANI ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar, Dkt Ali Mohamed Shein amesema Serikali itaendelea kushirikiana na waumini wa dini zote hapa nchini kama katiba ya pande zote mbili za Muungano wa Tanzania zinavyoelekeza.

Dkt Shein aliyasema hayo Jumanne alipokuwa na mazungumzo na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dkt Maimbo William Mndolwa aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha.

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inawathamini wananchi wake wote pamoja na dini zao kwa kufahamu kuwa kuimarika kwa imani za dini ni kuimarika kwa amani, utulivu, lakini pia ni sehemu ya kuimarika kwa maendeleo endelevu kwa jamii na taifa kwa jumla,” Dkt Shein alisema.

Alisema Zanzibar ina historia kubwa katika masuala ya dini zote kwani inaonyesha kwamba katika ukanda wa Afrika Mashariki dini za kikristo na kiislamu zilianza kuingia Zanzibar kabla ya maeneo mengine ya ukanda huo.

Pongezi

Kwa upande wake, Askofu Mndolwa alimpongeza Rais Shein kwa kuiongoza Zanzibar kwa amani, upendo na uvumilivu na kueleza kuwa kwa niaba ya Kanisa la Anglikana wanatoa shukrani zao na kumtakia heri na baraka katika uongozi wake.

Alisema waumini wa Kanisa la Anglikana Zanzibar wanavutiwa na ushirikiano wanaoupata kutoka serikalini chini ya uongozi wa Rais Dkt Shein na kwamba wataendelea kuunga mkono jitihada za kiongozi huyo kwa kuendelea kuhubiri amani na utulivu.