http://www.swahilihub.com/image/view/-/5119364/medRes/2346331/-/hay5knz/-/spika+pic.jpg

 

Spika aanzisha tena kwa CAG

Na Ibrahim Yamola, Mwananchi iyamola@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Friday, May 17  2019 at  10:18

 

Dodoma. Bado bungeni hakujapoa. Wakati wengi wakiamini kuwa sakata la Bunge na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) limepoa, wanaweza kuwa wamekosea.

Jana, Spika wa Bunge, Job Ndugai aliwatangazia wabunge mjini Dodoma kuwa ofisi ya CAG imekaguliwa hesabu zake.

Ndugai alitoa tangazo hilo jana asubuhi baada ya kumaliza dua ya kuliombea Bunge na Taifa, jambo ambalo pengine linaweza kuwa mara ya kwanza katika miaka ya karibuni kwa Spika kutoa taarifa ya kupokea ripoti ya ukaguzi wa hesabu za CAG.

“Baada ya (Kamati ya Hesabu za Serikali, PAC) kukamilisha, watawasilisha ripoti kwangu,” alisema Ndugai.

“Katika masuala ya ukaguzi hakuna anayebaki, hakuna anayejikagua mwenyewe kila watu wanaangaliwa na wenzao.”

Hii ni mara ya kwanza katika miaka kadhaa ya karibuni kwa Spika kulitangazia Bunge kuhusu kuwasilishwa kwa ripoti hiyo ya ukaguzi wa hesabu za CAG licha ya kwamba huwa zinawasilishwa kila mwaka kwa mujibu wa sheria.

Lakini taarifa hiyo ya Spika Ndugai imekuja wakati sakata la CAG na chombo hicho cha kutunga sheria halijaisha baada ya viongozi wa ofisi hizo mbili kuonekana kutofautiana, huku Ndugai akimtaka CAG Mussa Assad ajiuzulu.

alipoulizwa kuhusu kutolewa taarifa ya kupokelewa kwa ripoti hiyo, mwenyekiti wa kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka alisema hilo “muulizeni Spika mwenyewe kwa nini ameamua kutangaza bungeni”.

Aprili 2, Bunge lilitangaza azimio la kutofanya kazi na Profesa Mussa Assad. Azimio hilo lilitokana na CAG huyo kutuhumiwa kulidhalilisha Bunge kwa kuliita ‘dhaifu’ hivyo Ndugai kuiagiza Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kumhoji na taarifa ya kamati ilipowasilishwa bungeni ikamkuta na hatia.

Kauli hiyo ya ‘udhaifu wa Bunge’ aliitoa wakati akihojiwa na kituo cha televisheni cha Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa (UN) akiwa New York, Marekani alikokuwa akihudhuria mkutano.

Aliulizwa na mtangazaji wa kituo hicho sababu za taarifa zake nyingi kutofanyiwa kazi ipasavyo na Bunge.

Alitumia neno ‘udhaifu’ wa Bunge alipokuwa akieleza sababu za kutofanyiwa kazi kwa ripoti zake ambazo zimekuwa zikibainisha ufisadi katika maeneo kadhaa.

Jana, Ndugai alisema kwa mujibu wa kifungu cha 46 (1) cha sheria ya ukaguzi wa umma namba 11 ya mwaka 2008 kinaelezea kuwa hesabu za CAG zinapaswa kukagiliwa angalau mara moja kwa mwaka na kwamba Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ina jukumu la kuteua mkaguzi wa nje kwa ajili ya kukagua ofisi hiyo.

“Hesabu za CAG yaani za ofisi ya taifa ya ukaguzi zinapaswa kukaguliwa angalau mara moja kwa mwaka na kwamba Bunge kupitia PAC huwa ina jukumu la kuteua mkaguzi wa ofisi hiyo. Kwa maneno rahisi, Bunge ndio tunatafuta mkaguzi wa nje ambaye ndio anakagua hesabu za ofisi ya CAG,” alisema Spika.