TRA yakamata sukari, mafuta yaliyokwepa kodi

Na MOSES MASHALLA, Mwananchi            mmashalla@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Thursday, May 17  2018 at  15:27

Kwa Muhtasari

Magari yaliyokuwa yamebeba mzigo yataifishwa na wahusika watakiwa kulipa Tsh39 milioni.

 

ARUSHA, Tanzania

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imekamata mifuko ya sukari 169 na maboksi 40 ya mafuta ya kupikia, yaliyofungwa katika ujazo tofauti bidhaa zote zikiwa na zaidi ya thamani ya Tsh20 milioni.

Bidhaa hizo zilipaswa kulipwa kodi ya Tsh28.5, lakini kutokana na kuingizwa kinyemela, sasa imeongezeka na adhabu ya Tsh10.7 milioni, hivyo waliokamatwa na mali hizo watapaswa kulipa Sh39.2 milioni kama kodi na faini.

Pia, mamlaka hiyo imetaifisha bidhaa hizo na magari mawili yaliyotumika kuzipakia huku ikisisitiza kwamba vita vya kukamata biashara zinazopitishwa kwa magendo ni endelevu.

Akizungumza Jumatano jijini Arusha, Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere alisema Mei 11 maeneo ya Loliondo wilayani Ngorongoro mkoani hapa mamlaka hiyo ilikamata malori mawili yakiwa yamepakia bidhaa za magendo.

Kichere alisema katika ukaguzi wa magari hayo, walibaini yalikuwa yamebeba bidhaa tofauti huku lori la kwanza likiwa limepakia mifuko 169 ya sukari yenye ujazo wa kilo 50 kila mmoja.

Alisema kwamba lori jingine lilikuwa limepakia bidhaa na maboksi 40 ya mafuta ya kula yaliyofungwa kwa ujazo tofauti.

Kichere alisema wafanyabiashara hao wamevunja kifungu cha sheria nambari 200 na 82 ya Sheria ya Forodha ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 na sheria ya usimamizi wa kodi ya mwaka 2015.

“Wananchi wote na wafanyabiashara mnakumbushwa kuzingatia taratibu za uingizaji wa bidhaa nchini ili kuepuka hasara mamlaka haitasita kutaifisha bidhaa na magari yatakayopakia magendo,” alisema Kicheere.