Tatizo la uchumi, rushwa zapunguza kura za ANC

Imepakiwa - Wednesday, May 15  2019 at  12:16

 

Johannesburg. Tatizo la kushuka uchumi na rushwa zimeelezwa ni miongoni mwa sababu za chama tawala cha African National Congress (ANC), kupata kura asilimia ndogo ikilinganishwa na chaguzi zilizopita.

Vyanzo vya habari nchini humo, ANC imeongoza kwa kupata asilimia 58 ya kura zote na kufuatiwa na Chama cha Democratic Alliance (DA) kilichopata asilimia 21, wakati chama kilichoshika nafasi ya tatu ni cha Economic Freedom Fighters (EFF), ambacho kimejipatia kura asilimia 11.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kudorora kwa uchumi na rushwa ndivyo vilivyoshusha umaarufu wa chama hicho kikongwe cha ANC.

Baada ya kutangazwa matokeo kiongozi wa ANC, Cyril Ramaphosa, aliwataka wananchi kuungana na kujenga Afrika Kusini yenye umoja.

Alisema kuwa ushindi huo umeonyesha kuwa wananchi wa taifa hilo bado wana imani na ANC tangu ilipoingia madarakani mwaka 1994.

“Na sasa tufanye kazi kwa pamoja, watu weusi, wazungu wanaume kwa wanawake, vijana na wazee kujenga Afrika Kusini yenye umoja ni jukumu letu sote, ” Rais Ramaphosa aliwaambia wafuasi wake mjini Pretoria.

Alisema kwamba anaitaka Afrika Kusini ambayo sio ya kiubaguzi wa rangi, kijinsia, kidemokrasia na kimafanikio.

Taarifa zaidi zinasema kuwa chama hicho kimepata asilimia 65 katika mabunge yote mawili idadi ambayo imeporomoka ikilinganishwa na asilimia 73 ilizopata miaka mitano nyuma.

Idadi ya wapiga kura katika uchaguzi ulioisha ilikuwa ndogo na wachambuzi walisema ni ishara kuwa ANC inahitaji kujiangalia upya na kulenga kutatua matatizo ya wananchi.