Tunalaani tukio liliyofanywa na askari hawa

Imepakiwa - Wednesday, March 20  2019 at  09:18

 

Wiki iliyopita mitandao ya kijamii imeanika tukio lingine lisilo la kimaadili lililofanywa na askari wawili wa usalama barabarani wakiwatukana matusi ya nguoni watu waliokuwa ndani ya gari la kubeba mchanga (‘tipa’).

Hili ni tukio la pili kuanikwa hadharani na mitandao ya kijamii katika siku za karibuni linalowahusu askari wa usalama barabarani wakifanya vitendo vya ajabu. Lingine ni lile lililotokea mkoani Songwe ambapo ilishuhudiwa askari wakimshambulia dereva kwa ngumi na mateke.

Wakati tukio la Songwe lilishafikishwa mahakamani tayari, mitandao ya kijamii imeanika hili la wiki iliyopita likiwaonyesha askari, wakiwashusha kwenye gari watu kadhaa huku wakiwatukana matusi ambayo hayaandikiki gazetini.

Vilevile, mmoja wa askari hao anaonekana akimpiga makofi mtu mmoja baada ya kumuomba leseni ya udereva na baadaye yanasikika maneno “ng’oa, ng’oa, ng’oa”. Haijulikani anaambiwa ang’oe nini maana wahusika wote hawaonekani.

Hili ni tukio la kufedhehesha kwa jeshi letu ambalo linapaswa kufanya kazi kwa misingi ya “mteja na muuzaji” kwa maana ya mteja kuwa ni mwananchi na muuzaji wa huduma ni askari husika ambaye anapaswa kumhudumia mteja wake vizuri.

Ni wazi kwamba yapo matukio mengi kama alivyosema Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Yusuf Masauni juzi wakati akizungumzia tukio hili ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na madereva dhidi ya baadhi ya askari ikiwamo kuombwa rushwa na unyanyasaji.

Huko nyuma, mitandao hii ya kijamii iliwahi kuanika matukio mengine ya askari hao waliyofanya dhidi ya madereva. Mathalani, kule Zanzibar askari alionekana akimuomba rushwa raia wa kigeni aliyekuwa akiendesha gari. Tukio hilo lilinaswa na wasamaria wema wanaokerwa na vitendo vya rushwa, na Jeshi la Polisi liliahidi kuchukua hatua.

Si hilo tu, lakini lipo pia tukio ambalo askari mmoja jijini Dar es Salaam alirekodiwa akipokea rushwa kutoka kwa dereva na polisi walitoa taarifa kuwa amechukuliwa hatua ya kufukuzwa na angeshtakiwa kwa kosa la rushwa.

Wakati tunaipongeza Serikali kwa kuchukua hatua kali dhidi ya askari waliofanya tukio la wiki iliyopita ambao Naibu Waziri Masauni amesema wamekwishakamatwa, tunadhani ni vyema hatua zitakazochukuliwa zionekane kwa wananchi ili waendelee kujenga imani na chombo hiki.

Tunasema hivyo kwa sababu mara nyingi matukio yanayohusiana na polisi kwenda kinyume na maadili ya kazi zao dhidi ya raia yamekuwa yakidaiwa kumalizikika kimyakimya bila wananchi kuona hatua zinazochukuliwa, ikiwamo zile za kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa kama ilivyo kwa wahalifu wengine.

Tunadhani katika mkakati wa sasa wa polisi kujenga na kuimarisha huduma bora kwa wateja (wananchi), ni vyema matukio ya aina hii yaanze kuwekwa hadharani bila kuwaonea aibu wahusika ili wananchi waendelee kuliamini jeshi lao.

Tunalaani vikali vitendo vya aina hiyo na vingine wanavyofanyiwa raia na askari wasiozingatia maadili mema ya kazi yao.

Tunauomba uongozi wa jeshi letu kuchunguza mienendo ya askari wake ili kujiridhisha dhidi ya tabia zao na kuchukua hatua mara moja kwa wale wasio na maadili mema, ikiwamo kuachana nao.

Msingi wa Jeshi la polisi Tanzania ni kulinda raia na mali zao, tunaamini kwamba idadi kubwa ya askari wanaufuata. Wito wetu kwa viongozi wenye dhamana ya kusimamia jeshi hili ni kuhakikisha kwamba hawa wachache wanaotaka kulichafua wanadhibitiwa.