http://www.swahilihub.com/image/view/-/5117658/medRes/2345160/-/oydivaz/-/tuzo+pic.jpg

 

Tuzo ya Mei Mosi yazua tafrani

Na  Elias Msuya, Mwananchi emsuya@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Thursday, May 16  2019 at  10:31

 

Dar es Salaam. Wakati uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (Trawu) wakikanusha taarifa za kufanya udanganyifu katika kupendekeza majina ya wafanyakazi waliotakiwa kupata tuzo ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi), utata umegubika sababu za kigogo wa TRC kupewa tuzo na Rais John Magufuli.

Utata wa tuzo hizo umekuja huku mkurugenzi wa uendeshaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Focus Sahani akidaiwa kupendelewa kushikwa mkono na Rais John Magufuli siku ya sherehe hizo jijini Mbeya akishindanishwa na wafanyakazi wa ngazi za chini.

Katika mchakato wa kuwapata wafanyakazi bora kutoka TRC na Tazara, wafanyakazi watatu walichaguliwa akiwemo James Kunena na Focus Sahani walioshikwa mkono na Rais Magufuli na Richard Hega kutoka Tazara ambaye hakushikwa mkono.

Hata hivyo, mmoja wa maofisa wa Trawu aliliambia Mwananchi jana kuwa Focus Sahani hakustahili kwa sababu hakuchaguliwa kuwa mfanyakazi bora ila alichaguliwa kuwa mfanyakazi hodari na hivyo hakustahili kushikwa mkono na Rais.

“Huyo mkurugenzi (Sahani) alishindwa kura na kigezo kilichotumiwa ni kwa kuwa yeye ni kiongozi. Huwezi kumshindanisha kiongozi na mfanyakazi wa kawaida, kwa sababu wale wanapewa masilahi makubwa,” alisema ofisa huyo wa Trawu aliyeomba kuhifadhiwa jina lake.

Alisema baada ya kura kupigwa mara tatu, Sahani alishindwa na ndipo viongozi wa Trawu walimweka kwenye kura ya mfanyakazi hodari.

“Kundi la mfanyakazi hodari siyo kubwa, tena anaweza tu kushinkwa mkono na Mkuu wa Mkoa, lakini yeye ndio akapelekwa kushikwa mkono na Rais Mbeya,” alilalamika.

Hata hivyo, akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam jana, mwenyekiti wa Trawu, Lomitu Ole Saitabau alitetea Focus Sahani kushikwa mkono na Rais akisema mfanyakazi yeyote ana haki ya kuchaguliwa kuwa mfanyakazi bora bila kujali ngazi.

“Mkurugenzi naye anastahili kuwa mfanyakazi bora. Utaratibu ni wa kupigiwa kura na wafanyakazi wenzake,” alisema.

Saitabau alisema licha ya kushikwa mkono na Rais na kupewa vyeti, washindi hao watatu walipewa fedha taslimu ya Sh2.5 milioni kila mmoja.

Saitabau pia alisema utaratibu wa kupitisha majina ya washindi ulifuatwa.

“Trawu haihusiki kuchagua majina, bali hupokea majina yaliyopigiwa kura na wafanyakazi na kupeleka Tucta (Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi) kwa hatua zaidi,” alisema Saitabau.

Alisema Trawu ilipokea majina matatu, lakini walioshikwa mkono na Rais ni wawili kwa sababu ya idadi ya uwakilishi.

Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu tuhuma hizo, Sahani alisema hakuwepo kwenye uchaguzi wa wafanyakazi bora, bali aliambiwa tu ameshinda na anatakiwa akapokee tuzo jijini Mbeya.

“Mimi sijayasikia (malalamiko) kwa sababu nilikuwa safari. Labda uwaulize walionichagua kwa sababu mimi sikujichagua,” alisema Sahani.

Alipoulizwa kama anajiona kuwa na sifa ya kupata tuzo hiyo alisema “Sasa mzee mimi ni mwajiriwa, labda mngewauliza chama kwa sababu sikuwepo kwenye uchaguzi na sijui aliyenichagua, nilikuja kuambiwa tu.

“Hayo maswali waliochagua kule upande wa wafanyakazi kwa sababu inashirikisha watu wa chama na wengine, mimi sikuwepo. Mimi niliambiwa niko kwenye mfanyakazi bora, labda naomba uwaulize watu wa chama.”

Hata hivyo, mmoja wa wanachama wa Trawu ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini na aliyezungumza baada ya mkutano wa wanahabari jana alisema msingi wa malalamiko yao si tu kushikwa mkono na Rais, bali ni kumchanganya mkurugenzi (Focus Sahani) na wafanyakazi wa kawaida kugombea tuzo. “Kulikuwa na kura za aina mbili, kwanza tulipiga kura ya kupata mfanyakazi bora na baadaye tukapiga kura ya mfanyakazi hodari.