http://www.swahilihub.com/image/view/-/4564890/medRes/1975052/-/4xysxx/-/tra+pic.png

 

TRA isikilize vilio hivi kwa masilahi ya nchi

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kufafanua shughuli mbalimbali za mamlaka hiyo. Picha na maktaba    

Na Salim Said Salim

Imepakiwa - Wednesday, May 16  2018 at  15:21

Kwa Muhtasari

Mwezi uliopita tulisikia wafanya biashara kadhaa wa Mtwara na Lindi, waliofunga maduka yao kutokana na madai kwamba kodi waliyotozwa ni karibu sawa na mali waliokuwa nayo madukani.

 

Nimewahi kuandika na leo naongezea. Maana haupiti muda mrefu bila ya kusikia wafanyabiashara wakubwa na wadogo na watu wengine wakilalamikia mfumo wa utozaji kodi.

Vilevile malalamiko hayo ni jeuri, kiburi na vitisho vya baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA).

Wapo watu kutokana na kero hizo wanaona hapana faida ya kufanya biashara hapa nchini huamua kufunga maduka na kutafuta njia nyingine za kujikimu na maisha.

Wengine wamehamia nchi za jirani kufanya biashara baada ya kuona mazingira ya hapa kwetu si rafiki kwa biashara na wamekuwa na mafanikio mazuri.

Katika mkutano wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) uliofanyika Morogoro hivi karibuni, wahariri wengi waliwataka viongozi wa TRA waliokutana nao wajirekebishe ili Watanzania waone raha na furaha kulipa kodi.

Wahariri waliwataka viongozi wa TRA kuwa na mfumo rafiki wa kodi ili kupata mapato mazuri yatakayoweza kuchangia maendeleo ya nchi badala ya watu kuona kulipa kodi ni karaha isiyoelezeka.

Niliielezea kwa urefu katika mkutano huo hali ilivyokua mbaya Zanzibar na kugusia tabia ya baadhi ya maofisa wa TRA kubughudhi wafanyabiashara na kupelekea wafanyakazi wote wa TRA hata kuitwa “Miungu watu”.

Nilipokwenda Morogoro nilifikiri bughudha ya maofisa wa TRA ipo Zanzibar tu na ndio maana hata palisikika kelele za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutaka ofisi za TRA zilioko visiwani zifungwe na wafanyakazi wake waliotoka Bara wafunge virago na kurudi walikotoka.

Lakini, niliyoyasikia Morogoro niligundua kwamba sio watu wa visiwani tu wanaoilalamikia TRA, bali hata wenzao wa Bara nao ni taabani kama wao.

Mwezi uliopita tulisikia wafanya biashara kadhaa wa Mtwara na Lindi, waliofunga maduka yao kutokana na madai kwamba kodi waliyotozwa ni karibu sawa na mali waliokuwa nayo madukani.

Hatimaye palitumika busara ya kupunguza kodi kwa kiwango kikubwa na maduka yalifunguliwa baada ya wananchi kupata taabu kutokana ya kukosa huduma muhimu zinazotolea na maduka hayo.

Sasa tumesikia Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa akiwaomba wafanyabiashara wa Tunduma waliohamishia biashara zao Zambia kwa kushindwa kulipa kodi kubwa wanazokadiriwa na TRA, warudi nyumbani kwa kuwa suala la kiwango cha kodi linazungumzika.

Hali iliyojitokeza Tunduma pia imetokea Zanzibar. Wafanya biashara wengi wa visiwani walihamia Bara baada ya kuona hawazimudu bakora za kodi za TRA zinazotozwa visiwani.

Wengine walipoona kwenda kwao Bara ilikuwa sawa na kutoka kwenye kikaango na kutumbukia kwenye moto uliokuwa unakiunguza hicho kikaango, waliamua kwenda nchi jirani na sasa wanafanya biashara huko.

Hivi sasa zipo hisia miongoni mwa Wazanzibari wengi kwamba hizo harakati za TRA za kukusanya kodi badala ya kusaidia kukuza uchumi wa visiwani zinaudhoofisha na kupelekea watu wengi kukosa ajira kutokana na maduka kufungwa. Harakati za biashara Zanzibar siku hizi zimepoa sana na ukiuliza sababu unaambiwa kodi ni kubwa.

Kama wenzangu wengi katika mkutano wa Morogoro nilijaribu kuonyesha athari na hatari za kumkamua mfanyabishara hata akashindwa kupumua.

Nilifurahi kuona viongozi waandamizi wa TRA waliokuja Morogoro wakiniahidi mimi na wenzangu kwamba wangefuatilia taarifa zote walizopata. Lakini wapi…. Kimya kimetanda. Kwa jinsi hali ninavyosikia ikiendelea sehemu mbalimbali Bara na visiwani ambapo kuna mifumo miwili ya kodi, ile ya TRA na ya Mamlaka ya Kodi Zanzibar (ZRB) unalamikiwa, nabaki kujiuliza: Huu mfumo wa kodi unatupelekea wapi?

Wengi tulitarajia viongozi wa TRA kulifuatilia suala hili na kuwasiliana na wahariri ili kuwabana maofisa wao wachache wanaojipangia viwango vya kodi watakavyo wao na baya zaidi wanavyofanya jeuri na kibri na kuwatisha wafanya biashara wa mijini na vijijini.

Lakini, kimya kimetanda na tunaendelea kusikia visa na mikasa maeneo mengi ya nchi. mkuu wa mkoa wa Songwe anatuambia suala la viwango vya kodi linazungumzika, lakini hapa tujiulize kwani hizi kelele za siku zote Bara na visiwani na huko Songwe kulalamikia viwango hivyo hazikusikika kabla?

Mara ngapi wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamelieleza hili na mara ngapi suala hili limeelezwa katika mikutano ya wafanyabiashara na habari zake na maoni kuonekana na kusikika katika vyombo vya habari karibu kila siku.

Hivi karibuni tu nilielezea namna ambavyo wafanyabiashara na watu wa kawada wanavyoteseka hasa katika Bandari ya Dar es Salaam na hili lilielezwa kwa uwazi na wahariri wengi katika mkutano wa Morogoro.

Ni vizuri kwa viongozi wa TRA, kwa kushirikiana na wenzao wa ZRB wakaitafakari hali hii kwa makini. Vinginevyo tutajikuta tumejenga mazingira magumu zaidi ya biashara.

Jingine linalolalamikiwa ni kwamba wafanyabiashara kutoka nje ambao wanaitwa wawekezaji wa kigeni wanapata unafuu kuliko wazawa.

Wakati umefika kwa viongozi wa TRA kutafuta njia itakayomfanya kila Mtanzania, aione TRA ni taasisi rafiki badala ya kuwa na taswira ya kuua biashara nchini.

Mfumo tulionao sasa unachochea rushwa ili umsaidie mtu kulipa kodi ndogo. Hii ni mbaya zaidi kwa uchumi wa nchi.

Haitoshi kwa viongozi wetu kuonekana wanalifahamu tatizo la viwango vikubwa vya kodi viliopo. Kinachotakiwa ni kuchukua hatua kuhakikisha vinalingana na mapato na kupelekea kila mtu kuwa na furaha ya kulipa kodi.