http://www.swahilihub.com/image/view/-/5009596/medRes/2270111/-/5tftww/-/uchambuzi+pic.jpg

 

Uchambuzi wa Leo: Mzazi ni mwalimu wa kwanza wa mtoto

Mwalimu akitekeleza majukumu yake ya kufundisha na kulea 

Na Florence Majani

Imepakiwa - Tuesday, March 5  2019 at  09:36

 

 “Ukitaka kumfahamu vyema mzazi, basi mtazame mwanawe”. Huu ni usemi niliousoma kwenye bajaji moja huko mtaani kwangu Kimanga, Tabata jijini Dar es Salaam.

Nimeutafakari msemo huu nikapata jibu kuwa kumbe malezi ya wazazi yanaakisi tabia ya mtoto na ndiyo maana kuna ule usemi usemao “asiyefunzwa na mamaye, hufunzwa na ulimwengu” .

Napenda nizungumzie maadili ya watoto wa kike ambao kimsingi takwimu zinaonyesha kuwa ndiyo wanaoathiriwa zaidi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi, mimba za utotoni na ubakaji.

Hivi karibuni nilimsikia Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akilalamikia ongezeko la mimba za watoto kutoka 21,889 mwaka 2017 hadi 27,390 mwaka jana mkoani Tabora.

Mama Samia aliwataka wazazi kuwalinda watoto wao akisisitiza kuwa baadhi ya wazazi hao wanashindwa kujitokeza kutoa ushahidi hata pale inapojulikana kuwa watoto wao wamepata ujauzito.

Unadhani ni kwa nini Mama Samia alianza na wazazi? Ni kwa sababu, mzazi ndiye mwalimu wa kwanza kwa mtoto na ndiye anayemfahamu kwa undani mtoto wake.

Ninafahamu kwamba wazazi wanayafahamu majukumu yao vilivyo, lakini kila mmoja ajiulize, anawajibika ipasavyo katika makuzi na malezi ya binti yake? Anamuangalia, kumuonya na kumpa mahitaji yake ili asilaghaiwe?

Tatizo la wengi ni kuwa, wamewaachia walimu malezi haya wakiamini huko ndiko malezi sahihi yanakopatikana.

Nachelea kusema kuwa wapo wazazi ambao wanawaacha binti zao walelewe na ulimwengu. Hapa namaanisha kuwa, mama au baba hana muda na binti yake. Hafahamu binti ameingia saa ngapi? Ametoka saa ngapi? Hakagui madaftari wala hafuatilii maendeleo yake shuleni na pengine hajawahi kukanyaga shule anayosoma binti yake.

Wapo wazazi ambao hawajui mabegi ya mabinti zao yana nini ndani wala kufahamu marafiki wanaoongozana na mabinti zao.

Ndiyo maana mwanafalsafa George Santana alipata kusema kuwa “mtoto anayeelimishwa shuleni tu, ni mtoto ambaye hajaelimika.” Alimaanisha kuwa inahitajika nguvu na ushirikiano wa wazazi na walimu, na ndipo watoto watakuwa washindi.

Inasikitisha kuwa wapo wazazi ambao hawajui hata mabadiliko ya binti iwapo ana ujauzito au ameanza uhusiano wa mapenzi. Ni aibu mama au hata baba kugundua kuwa binti ana mimba ikiwa imefikia miezi mitano.

Kuna mkoa mmoja nilipata kutembelea, nikapokea malalamiko kutoka kwa wanafunzi kuwa, wazazi wanawalazimisha kuandika ‘madudu’ kwenye mtihani ili wafeli na wasiendelee na shule.

Hata hivyo, si hivyo tu, bali baadhi ya wazazi walilalamikiwa kuwaweka mabinti zao kwenye mazingira ya kuanza ngono mapema. Kwa mfano, mama anapomwambia binti yake “we’ mwanamke gani unamuachia mama yako atafute mboga kila siku, leo na wewe katafute mboga”. Unadhani katika mazingira haya, binti atafanya nini kama sio kuwekwa kwenye mazingira ya kuanza uhuni?

Ndiyo maana nasisitiza kuwa, mama na baba wana wajibu mkubwa kwenye malezi mabinti. Wazazi wasidhani jukumu la malezi ya mtoto wa kike ni la mwalimu mkuu, wala mwalimu wa nidhamu la hasha. Hawa kazi yao ni kunyoosha tu na kurekebisha pale palipopungua, lakini kiini cha maadili mema ya binti kinaanzia kwa mzazi.

Tupate muda wa kuwakanya watoto kwani mawaidha ya mama yana maana kubwa na yanadumu katika mioyo ya watoto, lakini pia, neno la Mungu lisiachwe bali liwe miongoni mwa mbinu za malezi hayo.

Roma haikujengwa kwa siku mmoja. Hivyo basi hata binti anahitaji mchakato sahihi wa malezi akionywa na kujengwa kila siku ili awe mwanamke mwenye maadili yaliyo mema kwa jamii.

Wengi wetu tupo kama tulivyo leo kutokana na malezi tuliyopewa na wazazi wetu. Namna walivyotukanya, walivyokuwa wanaishi na wengine, mienendo yao na hata namna walivyoishika imani ya dini zao.

Maisha yetu ya sasa yanaakisi mienendo ya wazazi wetu ilivyokuwa na hivyo wanageuka kuwa kioo kwenye maisha yetu. Ewe mzazi unachomchagulia leo mtoto wako ndicho atakachokuja kufanya au kuwa. Lawama hizi zisiende kwa walimu wala Serikali. Mzazi ni mwalimu wa kwanza wa mtoto, timiza wajibu wako kisha muombe Mwenyezi Mungu akuongoze.

Florence Majani ni mtumishi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), anapatikana kwa simu namba 0715-773366