http://www.swahilihub.com/image/view/-/5119382/medRes/2346343/-/s405vsz/-/uchumi+pic.jpg

 

Ukuaji uchumi Tanzania waikuna bemki ya Afrika

Na Asna Kaniki, Mwananchi akaniki@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Friday, May 17  2019 at  10:29

 

Dar es Salaam. Wakati uchumi wa dunia ukitajwa kukua kwa wastani wa 3.5, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), imeipongeza Tanzania kwa ukuaji wa uchumi wa wastani wa asilimia saba.

Imesema ukuaji huo kwa mwaka unaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi.

Pongezi hizo zilitolewa jana na Rais wa benki hiyo, Dk Akinwumi Adesina baada ya kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam kuhusu ushirikiano kati ya AfDB na Tanzania.

Katika taarifa ya Ikulu iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa ilieleza kuwa Adesina alimtaka Rais Magufuli kuendelea na mwelekeo huo ambao umeendelea kuimarisha uchumi wa Taifa.

Vilevile, alimpongeza kwa ushirikiano na nchi jirani ikiwamo Uganda uliofanikisha ujenzi wa mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi lenye urefu wa kilomita 1,443 kati ya Hoima, Uganda na Bandari ya Tanga. Pia, Dk Adesina alizungumzia kilimo akisema kuwa benki hiyo iko tayari kusaidia kukabiliana na tatizo la masoko ya mazao yanayozalishwa nchini.

Alisema hivi karibuni wameidhinisha ufadhili kwenye miradi ya ujenzi wa barabara za mzunguko jijini Dodoma zenye urefu wa kilomita 110 na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Msalato.

Alipongeza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa kati ya Dar es Salaam na Dodoma kwa kutumia fedha za ndani, na kuahidi kuunga mkono mradi wa ujenzi wa kuanzia Isaka kwenda Kigali nchini Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Kwa upande wake, Rais Magufuli alisema, “(AfDB) imekubali pia kujenga awamu ya pili ya mradi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) kati ya Kariakoo na Mbagala jijini Dar es Salaam.”