http://www.swahilihub.com/image/view/-/5116104/medRes/2344062/-/3wqss6z/-/uteuzi+pic.jpg

 

Uteuzi wa Rais haujazuia uhuru wa Ofisi ya Msajili

Na Kelvin Matandiko, Mwananchi kmatandiko@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Wednesday, May 15  2019 at  12:32

 

Zimebakia siku nne kabla ya kufahamu hatma ya chama cha ACT-Wazalendo baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kueleza dhamira ya kuifutia usajili ikidaiwa kukiuka sheria.

Makosa yanayodaiwa kuiweka kitanzini ni madai wafuasi kutumia maneno Takbir, kuchoma moto bendera za CUF na kutowasilisha hesabu za ukaguzi za 2013/2014, ambayo yalijibiwa na Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe.

Kutokana na malalamiko hayo, gazeti hili llifanya mahojiano maalumu na Msajili msaidizi wa vyama vya siasa, Sisty Nyahoza pamoja na mambo mengine kufahamu uhuru ilionao taasisi hiyo ambayo mtendaji mkuu anateuliwa na Rais.

Swali: Ofisi yako inao uhuru kiasi gani katika kutekeleza majukumu yake?

Jibu: Ukisoma sheria ya vyama vya siasa kipengere cha (4) na (5) inasema kutakuwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa itakayokuwa na huru, maana yake hii ni taasisi huru. Haijalishi mtendaji mkuu anateuliwa na nani. Ni sawa na mahakama. Katiba imesema mahakama itafanya kazi zake kwa uhuru lakini majaji wanateuliwa na rais, eeh hawa wana tofauti gani na sisi?

Hata Marekani majaji wanateuliwa na nani, si rais? Hakuna nchi yoyote duniani majaji wanajiteua wenyewe. Uhuru tunaousema katika sheria ni uhuru wa kiutendaji. Lakini lazima serikali iwe moja. Kiutendaji unakuwa huru bila Rais kuingilia.

Swali: Ofisi yako ina uwezo wa kumzuia Waziri mkuu mstaafu Mizengo Pinda aliyekuwa akifanya siasa majukwaani wakati hilo limezuiliwa na Rais John Magufuli?

Jibu: Jinsi mlivyoliona tukio hilo na mnavyolisema, sivyo. Siyo sahihi, kuna upotoshaji, kuna jinsi watu wanavyoripoti ili kujenga hiyo hoja yao, kumbe siyo sahihi.

Swali: Kifungu cha (11)(1) katika sheria ya vyama vya siasa vinaruhusiwa kufanya siasa , je visipofanya siasa maana yake kuna adhabu yoyote sivyo?

Jibu: Suala la msingi ni kuwa kuna chama kisichofanya siasa? Wote wanafanya siasa, mwingine nimesikia anahojiwa BBC, siasa zipo tu, huko kwenye mitandaoni wanafanya siasa.

Swali: Mnaitetea vipi sheria kuhusu zuio la mikutano ya kisiasa?

Jibu: Zuio lilitoka. Ni sahihi, siyo kinyume cha sheria. Walienda (wapinzani) kui-challenge mahakamani wakashindwa, sasa ingekuwa kinyume cha sheria si wangeshinda mahakamani?

Swali: Unadhani kuna haja ya kufanyika mabadiliko kufuta hicho kipengere kinachoruhusu siasa za majukwaa?

Jibu: Mimi naona kuna haja kabisa. Hizi competitive politics (siasa za kiushindani) za kuuza sera za kichama, zifanyike wakati wa uchaguzi hadi uchaguzi mwingine. Hivi unadhani Marekani sasa hivi wanaendelea kufanya siasa? Shughuli ishamalizika wanachapa kazi, sasa kwa nini sisi huku maskini tuanze kupiga siasa tu mwanzo hadi mwisho. Nafikiri utamaduni huo siyo mzuri.

Muda wa kampeni unatosha. Kuna chaguzi nyingi tu, kampeni miezi mitatu, chaguzi serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, fursa ya kufanya siasa na kujijenga wanayo (vyama vya upinzani).

Swali: Mbona kipengere hicho hakijaondolewa katika mabadiliko ya hivi karibuni?

Jibu: Sisi tumeweka hayo ambayo tunaona yanahitajika kwa wakati huu, tukihitaji marekebisho tutatangaza.

Swali: Kuna changamoto gani kulea vyama vya upinzani?

Jibu: Ni kama haya ya ACT Wazalendo, hao mashabiki wanachoma bendera, tumeshawaambia watueleze, wako kimya. Badala ya kusema jamani ehee hao siyo wa kwetu, kimya hadi msajili akatoa tamko kuwaambia jamani viongozi kemeeni suala hilo, kimya. Kimsingi sisi tunawataka watii sheria.

Swali: Madai ya Maalim Seif ni kwamba ofisi ya msajili inamuandama yeye, siyo ACT ni kweli?

Jibu: Si kweli kabisa. Tulianza kuwapa adhabu ndogo ndogo(ACT) ,mwaka jana kipindi kama hiki hiki, tuliwapa notice ,tukawaambia rekebisheni masuala ya hesabu, tukawafungia ruzuku, lakini mpaka mwaka huu hawajajirekebisha,

Kwa hiyo siyo kweli kabisa tutawamwaga tu, tutawaambia wananchi, sisi hatuonei mtu, hayo masuala ya Sief hatunayo, Novemba 2016, tuliweka nia ya kuvifuta vyama 11 na vilipewa barua za kujieleza kwa nini visifutiwe usajili kutokana na ukiukwaji wa sheria ikiwamo makosa mbalimbali ikiwamo kutowasilisha taarifa za ukaguzi wa fedha. Katika uamuzi huo, vyama vya Chausta, APPT-Maendeleo na Jahazi Asilia vilifutiwa usajili.

Mwaka huo ulisikia kuna chama kimeenda kutujibu kwenye media?, Hawakwenda. Walijibu na tulipoona wame-clear tukaachana nao. Sasa utaratibu wa kiofisi tumewaandikia barua.