http://www.swahilihub.com/image/view/-/5119790/medRes/2346699/-/mwlsnb/-/wanafunzi+pic.null

 

Wanafunzi washauri jinsi ya kukabiliana na mimba

Na Rachel Chibwete, Mwananchi rchibwete@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Friday, May 17  2019 at  12:58

 

Dodoma. Wanafunzi wa shule zilizopo wilayani Mpwapwa wamesema miongoni mwa sababu zinazochangia mimba za utotoni ni walezi kutoongea na watoto wao wa kike kuhusu elimu ya afya ya uzazi.

Wakizungumza jana, mwanafunzi wa shule ya msingi ya Kibakwe, Epifania Mwasamila alisema wazazi wao wanaona aibu kuzungumza nao kuhusu afya ya uzazi kitendo kinachosababisha wasichana wengi kujiingiza kwenye mapenzi bila kujua athari zake.

“Wazazi wetu wanatuona bado wadogo kuzungumza nasi afya ya uzazi lakini hawajui ndiyo wanatupoteza. Siku wakijua tumebeba mimba inakuwa ni shida.”

Kauli iliyoungwa mkono na mwanafunzi wa shule ya sekondari Mount Igovu, Anna Kimaro ambaye alisema umefika wakati wa wazazi na walezi kukaa na watoto wao wa kike na kuzungumza nao kuhusiana na elimu ya afya ya uzazi kuliko kuwaachia watu wengine.

Ofisa mradi wa shirika la Utu wa Mtoto (CDF), Clara Wisiko alisema wametoa elimu kwa wanafunzi wa kike 85 kuhusu elimu ya afya ya uzazi ili kuwakinga watoto hao na mimba za utotoni.