http://www.swahilihub.com/image/view/-/5119482/medRes/2343155/-/ynlipi/-/sare+pic.jpg

 

Wapinzani wataka uchunguzi sare za jeshi

Na Sharon Sauwa, Mwananchi ssauwa@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Friday, May 17  2019 at  10:59

 

Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imetaka Serikali kufanya uchunguzi wa mchakato wa ununuzi wa sare jeshini ili kujiridhisha kama umezingatia thamani ya fedha baada ya sare za mwaka huu kutokuwa na ubora stahiki.

Akiwasilisha maoni ya kambi hiyo jana kwa niaba ya msemaji wa kambi wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) , Mbunge wa Ndanda (Chadema) Cecil Mwambe alisema sare zilizogawiwa mwaka huu hazina ubora stahiki na haziendani na maumbo ya wahusika.

“Jambo hili limesababisha askari kulazimika kuendelea kutumia sare za zamani ambazo zinaonekana kuwa bora kuliko sare mpya,” alisema.

Alisema sare za zamani ziligawiwa mara ya mwisho mwaka 2014.

Mbali ya sare, Mwambe alisema zipo taarifa kwamba kuna idadi kubwa ya wanaostahili kupandishwa vyeo kutokana na muda waliokaa jeshini na wengine wamefuzu kozi zinazowafanya wastahili vyeo vipya lakini hawajapandishwa mpaka sasa.

“Yapo mazingira ambayo unakuta baadhi ya wanajeshi wamehudumu jeshini kati ya miaka mitano mpaka sita lakini hawakupandishwa vyeo,” alisema.

“Kutokana na utata huo wa kuwapandisha vyeo wanajeshi, kambi rasmi ya upinzani bungeni inataka Serikali kueleza Bunge hili kuna wanajeshi wangapi wenye sifa za kupandishwa vyeo lakini hawajapandishwa?” alisema akitaka pia kujua kuna tatizo gani linalosababisha wasipandishwe kwa wakati na kama jibu ni bajeti finyu.

“Je, Serikali iko tayari kuwaomba radhi wanajeshi ambao wana sifa za kupandishwa vyeo lakini hawajapandishwa na kuwaahidi kuwalipa malimbikizo ya mishahara ya vyeo vipya pindi watakapowapandisha vyeo?” aliuliza.