http://www.swahilihub.com/image/view/-/4564608/medRes/1974825/-/ldy7vfz/-/wasira.jpg

 

Watanzania milioni 10 wanategemea kilimo kuwaokoa

Dkt Charles Tizeba.

Waziri wa Wizara ya Kilimo nchini Tanzania Dkt Charles Tizeba. Picha/HISANI 

Na ALFRED ZACHARIA, Mwananchi         azacharia@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Thursday, June 14  2018 at  12:01

Kwa Muhtasari

Wadau wameshauri kuwapo kwa mazingira rafiki yatakayoongeza mchango wa sekta ya kilimo kwenye uchumi kunufaisha Watanzania.

 

DAR ES SALAAM, Tanzania

WAKATI Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi ikijipanga kuongeza makusanyo ya mapato kutoka vyanzo vyake mbalimbali, wadau wameshauri kuwapo kwa mazingira rafiki yatakayoongeza mchango wa sekta hiyo kwenye uchumi.

Licha ya kutopokea fedha kutoka Hazina mpaka Machi kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha, wizara hiyo imepanga kukusanya Tsh39.99 bilioni kutekeleza miradi yake ya maendeleo mwaka 2018/19.

Mpaka Aprili, wizara hiyo imefanikiwa kuzidi lengo ililojiwekea baada ya kukusanya Tsh36.1 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 108 ya maduhuli iliyopanga kukusanya kutoka idara ya uvuvi na asilimia 83.4 ya mifugo.

Wakati ufanisi wa wizara hiyo ukivuka malengo iliyojiwekea, mpaka muda huo ilikuwa haijapokea fedha kutoka Hazina, hivyo kumaanisha miradi yote iliyopagwa kutekelezwa ama ilitegemea mapato ya ndani na wafadhili au haikutekelezwa.

Pamoja na hayo, waziri husika, Luhaga Mpina ameliomba Bunge kuidhinisha Tsh56.45 bilioni zikiwamo Tsh12.1 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Bajeti ya wizara hiyo imeongezeka kwa asilimia 58.6 ikilinganishwa na Tsh35.6 bilioni za mwaka huu wa fedha ambapo ilitenga Tsh4 bilioni kwa ajili ya maendeleo.

Mpina anasema wizara hiyo inakusudia kukusanya fedha za kutosha kufanikisha utafiti utakaoongeza uzalishaji na tija ya sekta ya mifugo na uvuvi. Malengo mengine ni ujenzi wa malambo, masoko ya minada na uendelezaji wa mbegu bora.

Pamoja na mipango mizuri ya wizara hiyo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imekwishatahadharisha kuhusu kutotolewa fedha kwa ajili ya miradi ya wizara hiyo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mahmoud Mgimwa alisema wajumbe wake walielezwa ugumu uliopo kwa watendaji wa wizara kutekeleza miradi husika kwa kuwa hawapewi fedha zilizoidhinishwa.

“Mradi ulikuwa uanze lakini hatujapata fedha kutoka Hazina,” alisema Mgimwa huo ukiwa ni mojawapo wa utetezi walioukuta maeneo mengi ambako kamati hiyo ilitembelea kukagua miradi iliyobainishwa kwenye bajeti.

Hata hivyo, wizara inaamini itafanikisha malengo ya mwaka ujao wa fedha ikiwamo miradi ya maendeleo.

“Ninaamini tutafanikiwa kukusanya mapato ya ndani kama tulivyopanga. Tumeboresha mifumo yetu ya ukusanyaji maduhuli,” alisema Mpina alipokuwa akiwasilisha bajeti ya wizara kwa mwaka 2018/19.

Alibainisha kuwa baadhi ya vyanzo ni ada ya leseni ya usafirishaji wa mifugo nje ya nchi, leseni ya samaki na bidhaa zake, vibali vya usafirishaji, ushuru wa soko na minada pamoja na nyaraka za zabuni.

 

Wadau wanasemaje?    

Pamoja na mipango mizuri ya Serikali, wadau wa sekta hiyo wakiwamo wasafirishaji wa mifugo, wachinjaji na wasambazaji wa nyama wamelalamikia vitendo vinavyofanywa na baadhi ya maofisa wa wizara hiyo pindi wanapokagua au kukusanya tozo za aina mbalimbali.

Wadau hao wanasema wizara imeanzisha leseni mpya pamoja faini bila kushirikishwa, hivyo kuleta mkanganyiko kwenye ulipaji.

Mwenyekiti wa Chama cha Wachinjaji (Wavimi), Joel Meshaki anasema waliwahi kushangaa siku moja walipovamiwa machinjioni na kuulizwa kuhusu leseni ambazo hawazifahamu.

“Sikumbuki tarehe lakini Jumanne moja ya Aprili, saa 5:30 usiku walikuja watu wanne machinjio ya Vingunguti waliojitambulisha kuwa ni maofisa wa wizara,” anasema Meshaki.

Anasema ujio wa maofisa hao ulisimamisha shughuli za machinjio hayo kwa muda kwa kuwa kila ambaye hakuwa na leseni husika alitakiwa kulipa faini ya Sh500,000 na hakuna aliyekuwa nazo.

“Hatujawahi kusikia kitu kinachoitwa leseni ya uchinjaji ila kila mwenye leseni ya kusambaza nyama anaruhusiwa kuchinja,” anabainisha mwenyekiti huyo.

Kutokana na ujio huo wa ghafla na wenye faini kubwa, Meshaki anasema baadhi ya wamiliki wa mbuzi na ng’ombe walikimbia na kuiacha mifugo yao kutokana na kukosa fedha zilizohitajika.

Hata hivyo, hoja yake kubwa haikuwa kuanzishwa kwa leseni mpya isipokuwa kilichofanywa na maofisa hao kuvamia machinjio usiku na kuwatoza faini.

Mmoja wa wachuuzi wa machinjio hayo, Iddi Maziku anasema wizara inaweka msisitizo mkubwa kwenye ukusanyaji wa mapato bila kujali wajasiriamali wanatumia gharama kiasi gani kufanikisha biashara zao.

Maziku ni miongoni mwa walilazimika kulipa faini ya Tsh500,000 usiku huo licha ya leseni na vibali vingine alivyo navyo kumruhusu kufanya biashara ya mifugo.

“Nina lesseni mbili, moja ya usafirishaji wa mifugo na nyingine ya usambazaji nyama, ila nitatakiwa kutafuta ya tatu,” anasema.

Kutokana na mabadiliko hayo, Iddi na wenzake ambao bado hawajatekeleza masharti mapya ya biashara hiyo watatakiwa kutumia Tsh210,000 kupata leseni hiyo.

 

Ushauri wa wabunge

Licha ya wadau hao, baadhi ya wabunge waliochangia mjadala wa bajeti ya wizara hiyo walihoji umakini wa Serikali kufanikisha miradi ya wafugaji na wavuvi nchini, sekta inayowagusa wananchi wengi.

Mbunge wa Monduli (Chadema), Julius Laizer alisema licha ya malengo ya kukusanya mapato, Serikali inapaswa kuhakikisha inaboresha mazingira yaliyopo kwenye sekta hiyo.

“Inashangaza kuona sekta inayoiingizia Serikali Sh56 bilioni haipewi fedha za miradi ya maendeleo. Serikali inapaswa kutoa ruzuku kwa wafugaji na kufungua milango ya usafirishaji nje ya nchi kwa kuondoa tozo zisizo na msingi ili kuongeza mchango wa sekta hiyo,” alisema Laizer.

Mbunge huyo alihoji kwa nini Serikali inatumia zaidi ya Tsh56 bilioni kuagiza nyama kutoka nje kila mwaka ingawa Tanzania ni ya pili kwa idadi kubwa ya mifugo barani Afrika.

Mbunge wa viti maalumu (CCM), Agnes Marwa anasema utaratibu unaotumiwa na maofisa wa wizara hiyo kukusanya mapato kutoka kwa wavuvi ni wa kinyanyasaji.

“Wote tunatambua kuwa linapokuja suala la kukusanya mapato, kuna nguvu inatumiwa na maofisa wa Serikali suala linalowakatisha tamaa na kushusha morali wa wadau hawa muhimu,” alisema.

Agnes alilishauri Bunge kuunda kamati itakayochunguza mifumo inayotumika kukusanya maduhuli ya wizara tofauti ili kujiridhisha jinsi zinavyozingatia haki za raia na kuhamasisha uwekezaji nchini.

Mwaka jana, sekta ya mifugo ilikua kwa asilimia 2.8 ikilinganishwa na asilimia 2.7 za mwaka juzi wakati ile ya uvuvi ikiongezeka kwa asilimia 2.6 mwaka jana, ikishuka kutoka asilimia 4.2 mwaka uliotangulia.

Mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa (GDP) umekuwa na mabadiliko kwa miaka ya hivi karibuni.

Takwimu zinaonyesha kuwa mchango wa mifugo ulikuwa asilimia 6.9 mwaka jana ukishuka kutoka asilimia 7.7 za mwaka 2016 wakati ule wa uvuvi ukiwa asilimia 2.2 ukilinganishwa na asilimia 2.0 za mwaka juzi.