http://www.swahilihub.com/image/view/-/5119800/medRes/2346722/-/hd2bep/-/wazabuni+pic.jpg

 

Wazabuni lawamani ujenzi wa hospitali

Na Nazael Mkiramwani

Imepakiwa - Friday, May 17  2019 at  13:11

 

Dodoma. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Dk Semistatus Mashimba amesema ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo unakabiliwa na changamoto ya wasambazaji wa saruji waliopewa zabuni kutofikisha kwa wakati.

Amesema hayo jana siku chache baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo kusisitiza kuwa ujenzi hospitali 67 za wilaya zote nchini uwe umekamilika mwezi ujao.

Hata hivyo, Mashimba amesema mradi huo ambao unagharimu Sh 1.5 bilioni utakamilika Juni 30 mwaka huu.

Amesema kwasasa ujenzi upo katika hatua ya kuweka kenchi na kwamba kasi wanayoenda nayo utakamilika kwa wakati uliopangwa.

“Mradi huu utakamilika kwa wakati lakini tuna changamoto moja ya wasambazaji wa saruji, unaweza kuagiza lori nne lakini mzigo hautafiki kwa pamoja unakuta leo lori moja baada ya muda tena wanaleta jinguine,” amesema.

Alimewataka wasambazaji kufikishia saruji kwa wakati kama walivyokubaliana katika mkataba ili ujenzi ukamilike kwa wakati. Mkazi wa wilaya hiyo, Aisha Waziri amesema kukamilika kwa ujenzi wa hospitali hiyo kutasaidia kupatikana kwa huduma za afya za uhakika karibu tofauti na ilivyo sasa.