http://www.swahilihub.com/image/view/-/5118064/medRes/2345551/-/q21te6z/-/maziwa+pic.jpg

 

Wazalishaji maziwa walia na utitiri wa taasisi za maziwa

Na Fina Lyimo, Mwananchi Flyimo@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Thursday, May 16  2019 at  13:36

 

Moshi. Serikali imeombwa kupunguza taasisi zinazosimamia sekta ya maziwa nchini, kwani ni moja ya vikwazo vya kukua kwa sekta hiyo.

Pia, Serikali imetakiwa kuwasaidia wadau wakuu wa sekta hiyo ili maziwa yanayosindikwa yafike sokoni kwa urahisi na kwa gharama nafuu.

Akizungumza katika uzinduzi wa jukwaa la maziwa mkoani Kilimanjaro, katibu mkuu wa chama cha wasindikaji maziwa Tanzania (Tampa), Yohana Kubini alisema kwa sasa taasisi zinazosimamia sekta hiyo ni 24 ambazo huongeza gharama za uendeshaji.

Kubini alisema maziwa yanayozalishwa kwa mwaka ni lita 2.4 bilioni lakini yanayosindikwa ni lita milioni 35, kwa kuwa ndiyo yanayofika kwenye mfumo rasmi.

“Tampa ilifanya utafiti wa kuangalia gharama za usindikaji maziwa nchini na zilionekana ni kubwa, hivyo iliamua kujikita ndani zaidi kubaini gharama hizo zinaongezwa na utitiri wa taasisi zinazosimamia sekta hii,” alisema.

Kuhusu soko, alisema kwa takwimu zilizopo nchi yanajitosheleza kwa asilimia 50 na yanayosalia yanatoka nje.

Mshauri wa sera kutoka Shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV) Renatus Mbamilo alisema walifanya kazi ya kuunganisha wafugaji wilayani Hai na Siha, kwa kuunda vikundi ambavyo vimeunda chama cha msingi.

Awali, mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira alisema Serikali ina mpango mkakati kuhakikisha suala la lishe bora linafanyiwa kazi.