http://www.swahilihub.com/image/view/-/5119412/medRes/2346378/-/hu3gj1/-/wizara+pic.jpg

 

Wizara ya ulinzi yaomba Sh 1.8 trilioni ikitaja vipaumbele 12

Na Ibrahim Yamola, Mwananchi iyamola@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Friday, May 17  2019 at  10:41

 

Dodoma. Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi amewasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 ya Sh1.84 trilioni huku akitaja vipaumbele 12 ambavyo anakwenda kuvifanyia kazi katika kipindi hicho.

Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni jijini Dodoma jana, Dk Mwinyi alisema kati ya fedha hizo, Sh1.72 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh128 bilioni ni za maendeleo.

Bajeti hiyo ni pungufu ikilinganishwa na ile aliyoiwasilisha Mei 14, mwaka jana ya Sh1.91 trilioni. Akielezea utekelezaji wa bajeti hiyo, alisema kati ya Sh1.91 trilioni, Sh1.67 trilioni zilikuwa za matumizi ya kawaida na Sh234 bilioni za maendeleo.

Alisema hadi kufikia Aprili, fedha zilizokuwa zimetolewa ni Sh1.61 trilioni (sawa na asilimia 84.28) ya bajeti.

Waziri Mwinyi alisema kati ya fedha hizo, Sh1.44 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh164 bilioni ni za maendeleo, ambapo fedha za matumizi ya kawaida Sh1.31 trilioni zimetumika kulipa mishahara na posho mbalimbali kwa maofisa, askari, vijana kwa mujibu wa sheria na wa kujitolea.

Alisema utekelezaji wa bajeti hiyo umekutana na changamoto mbalimbali.

“Kubwa ikiwa ni ufinyu wa ukomo wa bajeti ambapo kiasi cha Sh1.91 trioni hakikidhi mahitaji halisi,” alisema.

Waziri Mwinyi alisema fedha za maendeleo zilizotolewa kwa kiasi kikubwa zimetumika kulipia mikataba michache ya ununuzi wa zana na utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo.

“Hali hii imesababisha wizara kutoweza kutekeleza mipango yote iliyojiwekea katika mwaka 2018/19.”

Alisema katika azma ya kutekeleza uimarishaji na uzalishaji wa viwanda vipya vya jeshi zipo changamoto za uchakavu wa miundombinu ya viwanda ikiwemo karakana, maabara, barabara, mitambo na majengo.

Alisema karakana nyingi zinatumika teknolojia zilizopitwa na wakati na kuna upungufu wa wataalamu wa kuendesha mitambo, hususan katika mashirika ya Mzinga na Nyumbu.

Waziri Mwinyi alisema hali ya usalama wa mipaka kwa ujuma imeendelea kuwa shwari na kwamba, katika kipindi cha Julai 2018 hadi Aprili 2019 hakuna matukio ya kuhatarisha usalama wa nchi yaliyoripotiwa kati ya nchi zinazopatikana na Tanzania.

Bunge lilipitisha bajeti ya wizara hiyo jana jioni.